Tuesday, May 15, 2018

MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERUKALI (CAG) AZUNGUMZIA MAFANIKIO YA OFISI YAKE

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG), Profesa Mussa Juma Assad amesema ofisi yake imefanikiwa kutoa taarifa kwa wakati, kila inapofika Machi 30 ya kila mwaka licha ya kukabiliwa na changamoto ya ufinyu wa bajeti.
Profesa Assad ameeleza hayo leo jijini Dodoma kwenye mkutano wa Baraza la wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, ambao unalenga kupitisha bajeti ya mwaka na kujadili masuala ya kiutendaji ambayo yanawasilishwa na kuitishwa na wajumbe.
Akizungumza katika mkutano huo, CAG amesema ufinyu huo unaosababisha shughuli za kiofisi kutofanyika pamoja na kushindwa kutekeleza majukumu ya dharula yanayoibuka nje ya ukomo wao wa bajeti.
“Baraza hii limekuwa na ufanisi mkubwa katika kusimamia majukumu yake kama yalivyoainishwa kwenye mkataba,”amesema Prof. Assad.
Amesema pamoja na mafanikio mbalimbali ambayo ofisi hiyo imeyapata, bado zipo changamoto mbalimbali zinazoikabili na zinahitaji utatuzi wa kina.
Amezitaja changamoto nyingine kuwa ni kushindwa kukamilisha ujenzi kwa ajili ya Ofisi katika mikoa iliyolengwa kutokana na kutotolewa kwa fedha za maendeleo kama ilivyopangwa na kwa wakati.
Aidha amesema katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa Fedha 2017/18 hadi kufikia Machi, 2018 Ofisi ilishindwa kuwajengea uwezo watumishi kulingana na viwango vya kimataifa vya ukaguzi kutokana na ufinyu wa bajeti.
“Kuna changamoto ya mwenendo wa upatikanaji wa fedha za matumizi mengineyo na maendeleo kutoka mfumo mkuu wa serikali kutoendana na mahitaji halisi ya majukumu ya Taasisi hususani ukaguzi na mafunzo kwa watumishi,”amesema.
Akifungua mkutano huo, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais ,Utumishi, Dk.Laurean Ndumbaro ameitaka ofisi ya Taifa ya ukaguzi kutekeleza agizo la serikali kuhamishia shughuli zake mkoani Dodoma.
Dk. Ndumbaro amesema tayari viongozi mbalimbali wa serikali walishahamia, hivyo ni mategemeo yake kuwa Ofisi ya Taifa ya ukaguzi nayo pia ipo katika mkakati wa kuhamishia shughuli zake jijini Dodoma kama ambavyo taasisi nyingine zimefanya.

 Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Juma Asaad (kushoto) akiwa na  Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi Dk.Laurean Ndumbaro (kulia)wakifurahia jambo wakati aliokuwa kimsindikiza mara baada Katibu Mkuu huyo kufungua mkuatano mkuu  wa Baraza la Wafanyakazi Ofisi ya CAG uliofanyika mjini Dodoma leo.
 Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi Dk.Laurean Ndumbaro akizungumza wakati wa kufungua mkutano mkuu wa Baraza la Wafanyakazi Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) lililofanyika mjini Dodoma leo .
 Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi Dk.Laurean Ndumbaro akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa baraza la wafanyakazi Ofisi ya CAG.
 Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Prof Musa Asaad akitoa taarifa ya Ofisi yake wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya CAG lililofanyika leo jijini  Dodoma .
 Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi Dk.Laurean Ndumbaro akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa baraza la wafanyakazi Ofisi ya CAG.
wajumbe wa mkutano wa Baraza la wafanyakazi wa Ofisi ya Ukaguzi

No comments: