Thursday, May 3, 2018

DC KIGAMBONI AWAONDOLEA TAHARUKI WANANCHI WA KIBADA KUBOLEWA NYUMBA ZAO

Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mh.Hashim Mgandilwa ameondoa hali ya taharuki iliyokuwa imetanda miongoni mwa wananchi wa Kata ya Kibada waliowekewa alama ya kubomoa majengo yao na  wakala wa barabara (TANROADS) mbali na kununua viwanja hivyo kihalali kutoka wizara ya ardhi.

Akizungumza na wananchi hao kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika jana kwenye ofisi za Kata ya Kibada Mh.Mgandilwa amesema kuwa ofisi yake na wataalamu hawapo tayari kuona wananchi wao wanaonewa.

Aliongeza kuwa mgongano huo umebainika kwenye mradi wa ujenzi wa barabara uliopo kwenye hatua za awali na ubainishaji wa mipaka wa Tanroads unaolenga kujenga barabara kiwango cha lami kuanzia Kibada-Somangila hadi Kimbiji.

Mgandilwa alisema kuwa wizara ya ardhi ilikuwa na mradi wa viwanja ishirini elfu vilivyouzwa kwa wananchi kihalali ambapo baada ya Tanroads kubainisha mipaka yake ndipo ilipobainika kuwa wizara ya ardhi iliuza viwanja vyake hadi kwenye hifadhi ya barabara.

"Viwanja hivi vilinunuliwa wizara ya ardhi ambapo wananchi walikuwa na uhakika wa usalama wa viwanja vyao kutokana na kununua kwene wizara husika, leo hii kuja kuwawekea alama ya kubomoa sio haki, mwananchi anakuwa anawajibishwa kwa kosa ambalo si lake ndiomaana tumekutana hapa ili tuweze kuona namna gani tunaweza kufikia muafaka" Alisema Mkuu wa Wilaya.

Aliongeza kuwa wao kama Serikali wameona ni bora kuzungumza na wananchi  kwasababu Serikali haipaswi kukinzana na sheria badala yake inaangalia mahali ambapo pamekosewa na kurekebisha.

Aidha Mkuu wa Wilaya aliwataka wananchi wote waliowekea alama za kubomoa majengo yao ndani ya siku 90 kufika ofisini kwake siku ya jumamosi tarehe 5/5/2018 ambapo kutakuwa na wataalamu kutoka wizara ya Ardhi na Tanroads ili kuona namna bora ya kufikia muafaka.

Wakati huohuo Mkuu wa Wilaya amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye hamasa na kuthaminiwa hususani wananchi ambao watapitiwa na ujenzi wa mradi wa kituo cha kupoozea umeme ambapo italazimika kusimika nguzo za umeme ambazo hazitaruhusu uwepo wa makazi ya aina yeyote.

Mkuu wa Wilaya alisema kuwa, ni vyema wakajitokeza ili kuondoa malalamiko na adha zinazazoweza kuzuilika kwenye hatua za utambuzi na uthamini ili kulipwa fidia kwasababu nishati ya umeme inahitajika kwa kiwango kikubwa kutokana na Wilaya ya Kigamboni kukosa umeme wa uhakika, na kuwa waathirika wa kwanza pindi inapotokea hitilafu kidogo kwenye vituo vinavyotegemewa kwa sasa.

"Nawaomba ndugu zangu mjitokeze pindi mtakapohitajika kwenye zoezi la utambuzi na uthamini, Wilaya ya kigamboni tunahitaji umeme wa uhakika ili tuweze kuwa na viwanda na uwekezaji wenye tija kutokana na kuwepo kwa umeme wa uhakika" Alisema Mh.Mgandilwa

Mradi wa kituo kidogo cha kuupozea umeme kinajengwa Dege kata ya Somangila ambapo  hadi kufikia mwaka 2020 unatarajiwa kuwa umeanza kazi huku Kata tatu za Kibada,KisaraweII na Somangila kwenye mitaa 6 inatarajiwa kupitiwa na nguzo hizo zenye umeme mkubwa ambao hauruhusu kuwepo kwa makazi yeyote kwa usalama wa wananchi wa maeneo hayo.

 Imeandaliwa na:
Kitengo cha Teknolojia, Habari na Mawasiliano
Halmshauri ya Manispaa ya Kigamboni
03/05/2018

  Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni  Mh.Hashim Mgandilwa mwenye kofiaakizungumza na wakazi wa Kibada kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika jana.
 Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mh.Hashim Mgandilwa akisistiza kuwa Sheria itafuatwa kuhakikisha wananchi wanapata haki yao.
 Mkuu wa wilaya ya Kigamboni Mh.Hashim Mgandilwa na wananchi wa kibada wakisoma ra,mani ili kubaini mipaka .
 Diwani wa Kata ya Kibada Mh.Amin Sambo  akishiriki kuchimba eneo linalodaiwa kuwa na jiwe la mpaka kwenye eneo la mkazi wa Kibada wakati walipokuwa wakitafuta mawe ya Mipaka.
 Kamati ya ulinzi na usalama na waanchi wakizulu kwenye moja ya nyumba iliyowekwa alama ya kubomoa na wakala wa barabara Tanroads ili kubaini mpaka uliopo.
  Mthamini wa Manispaa ya Kigamboni Bw.Mpoki Daimon  akifafanua taratibu za uthamini na ulipwaji fidia kwa wananchi wa Kata ya Somangila Mtaa wa Dege.
Baadhi ya wananchi na wataalamu mbalimbali  walishirki kwenye mkutano huo wa hadhara Kibada.

No comments: