Friday, April 13, 2018

WAZIRI MHAGAMA AUPONGEZA UONGOZI WA KANISA LA BAPTIST KWA KUENDELEA KUIOMBEA NCHI YETU.


Waziri wa Nchi Ofisi anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ameupongeza uongozi wa Kanisa la Baptist nchini kwa kuendela kuliombea Taifa ili kudumisha Amani na Utulivu uliopo.

Ametoa pongezi hizo hii leo alipokutana na Uongozi wa Kanisa hilo Bungeni Dodoma ili kujadili na kuipongeza Serikali kwa juhudi inazozifanya kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na amani na utulivu kwa kuzingatia sheria na miongozo iliyopo.

“Niwapongeza sana uongozi wote wa Kanisa la Baptist nchini kwa kuendelea kutuombea na kuikumbuka nchi yetu kwani bila uwepo wa amani na utulivu maendeleo hayawezi kuwepo.”Alisema Waziri Mhagama

Aliongezea kuwa pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuhakikisha inaboresha na kuleta maendeleo ya nchi yake bado kuna umuhimu wa kuendelea kuwa na ushirika mzuri na viongozi wetu wa dini na kuunga mkono jitihada za Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli katika kufikia azma yake ya “Tanzania ya Viwanda”.

“Kipekee niwashukuru kwa kuona umuhimu wa kutuweka mikononi mwa Mungu Uongozi wote wa nchi, kuanzia kwa Mhe. Rais wetu, Baraza la Mawaziri na Viongozi wote kwa ujumla wao ili kuhakikisha tunakuwa na hekima na weredi wa utekelezaji wa majukumu yetu kuhakikisha Watanzania wanapata maendeleo.”Alisisitiza Waziri Mhagama

Pamoja na hilo aliuomba uongozi huo kuendelea kuchangia katika Huduma za kijamii hususan kupitia mchango wanautoa kwa jamii wa kuwa na Shule, Vyuo na Zahanati zinazohudumia Wananchi wanaochangia katika uzalishaji na maendeleo ya nchi yao.

“Ni vyema sasa mkawa na mipango endelevu ya kuboresha Taasisi zenu ikiwemo Chuo cha Mount Meru na shule zenu ili kuendelea kutoa huduma za kielimu, afya ili kuwa na Watanzania wenye uzalendo katika kutekeleza majukumu yao.”Alisisitiza Waziri.

Aidha kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa la Baptist nchini Arnoid Manase ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa hatua kubwa iliyoifanya katika kuleta mabadiliko ya kimaendeleo tangu ilipoingia madarakani na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa hali na mali ili kuona nchi inaendelea na kuondokana na baadhi ya changamoto zilizopo.

“Binafsi ninaipongeza Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli kwa juhudi zake pamoja na uongozi wote na tunaahidi kuendelea kuwaweka mikononi mwa Mungu ili kuwa na nchi yenye Amani, Upendo, Mshikamano na Utulivu.”Alisisitiza Askofu Manase.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe.Jenista Mhagama akizungumza jambo kwa baadhi ya viongozi wa Kanisa la Baptist nchini walipomtembelea katika Ofisi yake Bungeni Dodoma Aprili 12, 2018.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe.Jenista Mhagama akisalimiana na baadhi ya viongozi wa Kanisa la Baptist nchini.
Askofu wa Kanisa la Baptist nchini Arnoid Manase akifanya maombi kwa kifupi walipomtembelea Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe.Jenista Mhagama kuzungumza masuala yao na kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa jitihada za kukuza uchumi na maendeleo kwa ujumla.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe.Jenista Mhagama akipata maelekezo ya hati ya pongezi (ya Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli) kutoka kwa Askofu wa Kanisa la Baptist nchini Arnoid Manase
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe.Jenista Mhagama akiwashukuru viongozi wa Kanisa la Baptist nchini walipomtembelea Ofisini kwake Bungeni Dodoma.(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU – DODOMA)

No comments: