NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
WANAWAKE visiwani Zanzibar wameshauriwa kutumia vizuri fursa ya ujasiriamali kwa lengo la kujiongezea kipato na kujiajiri wenyewe.
Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi wa Taasisi ya New Vision Consortium (NVCT) Pily Khamis Lapda, amesema wanawake wengi hapa nchini wamekuwa wakifanya shughuli za ujasiriamali kwa mazoea jambo linalopelekea kushindwa kufikia malengo yao ya kumiliki mitaji mikubwa ya kibiashara.
Amesema zipo njia mbali mbali za kuwakomboa wanawake kiuchumi zikiwemo kupenda na kuamini shughuli za ujasiriamali kama nyenzo ya kujikomboa kiuchumi.Amewashauri wanawake nchini kujiamini pindi wanapoanzisha biashara zao sambamba na kujiwekea malengo ya kudumu ya kibiashara yatakayowasaidia kumiliki mitaji mikubwa ya kibiashara.
Mkurugenzi huyo Pily, akizungumzia malengo ya taasisi yake inayoendesha na kusimamia mafunzo ya kuyajengea uwezo wa kitaaluma makundi mbali mbali ya kijamii ili kupata uwezo wa kutumia ipasavyo fursa za ujasiriamali wenye maendeleo.“Wanawake tuwe mstari wa mbele kujifunza mbinu mbali mbali za kujikwamua kiuchumi, pia tujitume na kuwa wabunifu katika biashara zetu ili nasi tuwe miongoni mwa wajasiriamali wa kimataifa.”, amesema Mkurugenzi huyo.
Akitoa mada ya Uvumbuzi binafsi, mtaalamu wa Saikolojia na maendeleo ya vijana, Joseph Mrindo amesema wanawake waliopo katika sekta ya ujasiriamali wanatakiwa kuondokana na dhana ya ujasiriamali mdogo mdogo kwani hali hiyo inasababisha kudumaa kiakili na kushindwa kufikia malengo yao ya kumiliki biashara kunwa na makapuni.
Ameeleza kuwa Zanzibar ni sehemu muhimu yenye fursa za kibiashara hivyo wanawake wanatakiwa kutumia nafasi hiyo kujiongeza kibiashara.Mtaalamu huyo, amewasihi wajasiriamali kufuata maelekezo na mbinu mbali mbali za maendeleo ya kibiashara ili wawe na mitaji mikubwa itakayowawezesha kupewa mikopo kwa wakati na benki mbali mbali nchini.
Naye mshiriki wa mafunzo hayo, Munawar Sleiman Mbarouk amesema miongoni mwa changamoto zinazowakabili wajasiria mali ni ukosefu wa mitaji na ujuzi wa kufanya biashara zenye tija kwa mjasiria mali mmoja mmoja na vikundi.Mafunzo hayo ya siku mbili yanatolewa na taasisi ya New vision consortium (NVCT)iliyopo Zanzibar na jumla ya washiriki 200 kutoka taasisi binafsi na za umma wanapewa ujuzi huo wa ujasiriamali.
Wadhamini wa mafunzo hayo ni pamoja na NMB, ZSSF, ZURA na IQUITY BANK
MKURUGENZI wa New vision consortium Pily Khamis Lapda(aliyekaa katikati) akifungua mafunzo ya siku mbili ya ujasiriamali kwa wanawake wa Zanzibar yaliyofanyika katika Skuli ya Haile-Sela-ssie.
BAADHI ya washiriki katika mafunzo hayo kutoka taasisi binafsi na za umma wakifuatilia kwa makini mada mbali mbali zilizowasilishwa katika mafunzo hayo, huko Skuli ya Haile-Sela-ssie.
MSHIRIKI wa mafunzo ambaye pia ni mjasiria mali kutoka U.WT. jimbo la Mwera Salama Mohamed Tahir akichangia mada ya uvumbuzi binafsi.
No comments:
Post a Comment