Tuesday, April 17, 2018

UAMUZI KESI MBOWE, WENZAKE KUPELEKWA MAHAKAMA KUU AU LAA KUJULIKANA MEI 15


Na Ripota Wetu, Globu ya jamii

UAMUZI wa kesi inayowakabili viongozi 9 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) akiwemo Mwenyekiti wao Freeman Mbowe ya kufanya maandamano/mkusanyiko usio halali unatarajiwa kutolewa Mei 15 mwaka huu kama iende Mahakama Kuu au laa.

Hatua hiyo inatokana na mvutano wa hoja za kisheria zilizotolewa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Wakili wa utetezi, Peter Kibatala kisha kujibiwa leo na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.

Hata hivyo majibu yake Wakili Nchimbi ameiomba Mahakama hiyo kutupilia mbali hoja za utetezi zilizotolewa na Kibatala kwa madai zitasababisha ucheleweshaji wa shauri hilo.Nchimbi amefafanua kwa kudai mazingira ya mwenendo wa kesi hiyo toka ilipoanza hadi leo hakuna swali lolote la msingi lililoibuliwa na upande wa utetezi ambalo linajikita na uvunjifu ama ukiukwaji wa haki ya kikatiba.

Ameongeza anaeleza hivyo kwani akiaangalia msingi wa hoja zilizowasilishwa na upande wa utetezi jana zimejikita katika mashtaka yanayowakabili washtakiwa.Ameongeza ukiangalia mlolongo wa hati ya mashtaka ni hati ambayo washtakiwa wamesomewa mashtaka zaidi ya mara moja au mbili ikiwamo jana."Washtakiwa waliyasikia mashtaka, wakayaelewa ndiyo maana wakaenda mbele wakayakanusha.

Kama kweli washtakiwa waliona mashtaka haya si halali, hati  ya mashtaka ilitolewa mapema hoja zilizowasilishwa na upande wa utetezi zingewasilishwa kabla"amesema Nchimbi.Amedai  ni rai ya upande wa mashtaka yote yaliyoongelewa na upande wa utetezi hayawezi kuitwa ni maswali ya kikatiba ambayo yangeilazimu Mahakama kupeleka kesi hiyo Mahakama Kuu na kudai hakuna suala la kikatiba hapo.

"Ukiendelea kufuatilia hoja za utetezi hawajashambulia vifungu vya kisheria vilivyotumika kuwashtaki washtakiwa hao.Hata hivyo Wakili Kibatala ameiomba Mahakama kuwa mchakato wa kijinai ni mchakato mtakatifu ambao haukukusudiwa kuwashtaki watu ambao wanatekeleza majukumu yao kikatiba.

"Tunaka kwenda Mahakama Kuu  kwa lengo la kupata tafsiri ya  je  ni kweli mtu akiwa anatekeleza majukumu yake ya kikatiba ashtakiwe kijinai,"amesema Kibatala.Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 15 mwaka huu.Wengine wanaoshtakiwa kwenye kesi hiyo ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu, Naibu katibu Mkuu Bara na Mbunge wa Kibamba John Mnyika na Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa.

Pia Mbunge wa Tarime mjini Esterher Matiko, Katibu wa chama hicho Dk.Vicenti  Mashinji, Mbunge wa Kawe Halima Mdee, Mbunge wa Tarime vijijini John Heche na Mbunge wa Bunda Ester Bulaya.

No comments: