Thursday, April 19, 2018

TCAA YAAGIZWA KUSIMAMIA USAFIRI WA ANGA

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (wa pili kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari wakati akitoa maelezo ya awali kabla ya ufunguzi wa Baraza la wafanyakazi la Mamlaka hiyo, mjini Dodoma.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akisisitiza jambo wakati wa ufunguzi wa Baraza la wafanyakazi la Mamlaka hiyo, lililofanyika mjini Dodoma. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kulia) akimkabidhi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari nyaraka mbalimbali mara baada ya kulifungua mjini Dodoma. 
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Baraza la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) lililofanyika mjini Dodoma. 


……………


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, ameitaka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), kusimamia usafiri wa anga kwa kuzingatia taratibu na kanuni za usafiri huo ili kuweka uwiano wa haki kwa waendeshaji na abiria wanaotumia usafiri huo.


Ametoa kauli hiyo mjini Dodoma wakati akizindua rasmi Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka hiyo na kuwapongeza kwa kuamua kuweka mikakati ya kununua rada nne kwa kutumia fedha za ndani.


“Lazima msimamie kanuni na taratibu zilizopo, wajibu wenu ni kutoa haki kwa watumiaji na abiria kwa usawa, hatutaki kusikia mnakandamiza watumiaji wa usafiri na mkisimamia vizuri eneo hili mtafanya idadi ya watumiaji kuongezeka na makampuni kuendelea kuwekeza zaidi kwenye usafiri” amesisitiza Prof. Mbarawa.


Waziri Prof. Mbarawa amesema yeyote anaevunja taratibu zilizowekwa kwenye usafiri wa anga Mamlaka hiyo ichukue hatua stahiki kulingana na taratibu zilizopo ili usafiri huo uweze kuwa na nidhamu.


“Kila Kampuni mkiiachia ifanye inavyotaka hatutafika popote na malalamiko kwenye usafiri wa anga yataendelea kuwepo, hivyo naomba msimamie makampuni haya kwa ukaribu mkubwa,’ amesisitiza Prof. Mbarawa.


Ameongeza kuwa ili mamlaka ifikie lengo na kufanikiwa lazima Menejimenti ishirikishe watumishi kwa karibu ili kutimiza malengo iliyojiwekea.


Prof. Mbarawa amesisitiza umuhimu wa TCAA kuwawezesha watumishi wake kitaaluma na kimaslahi ili kuongeza tija katika kazi na kufikia malengo ya utendaji Kitaifa na Kimataifa.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Bw, Hamza Johari, amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa TCAA imejipanga kutekeleza miradi mbalimbali kwa kutumia vyanzo vya ndani ili kuvutia makampuni ya ndege ya ndani na nje ya nchi.


“Nikuhakikishie kuwa tumejipanga kutekeleza miradi mingi zaidi kwenye usafiri wa ndani ili kuchochea kasi ya usafiri huo lakini pia kutimiza amza ya kuboresha usafiri huo, ”amesema Johari.


Ameongeza kuwa kwa sasa mamlaka iko kwenye hatua za awali za utekelezaji wa mradi wa kufunga vifaa maalum vya kuwezesha ndege kwa usalama katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Zanzibar ambapo mradi huo ukikamilika utaimarisha huduma za kuongozea ndege katika kiwanja hicho.

No comments: