Saturday, April 21, 2018

RC TABORA: VIONGOZI WA DINI TUASAIDIENI KUWAHIMIZA WATOTO WAKIKE WAJE KWENYE CHANJO YA HPV VACCINE JUMATATU

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri akifungua jana semina ya siku moja ya Kamati ya Huduma ya Afya ya Msingi ya Mkoa huo ikiwa ni maandalizi ya chanjo ya kukinga saratani ya mlango wa kizazi itakayoanza tarehe 23 Mwezi huu mkoani kote.

Viongozi wa dini mbalimbali na wageni waalikwa wakiwa katika semina ya siku moja ya Kamati ya Huduma ya Afya ya Msingi ya Mkoa huo ikiwa ni maandalizi ya chanjo ya kukinga saratani ya mlango wa kizazi itakayoanza tarehe 23 Mwezi huu mkoani kote.Picha na Tiganya Vincent


NA TIGANYA VINCENT,RS TABORA

SERIKALI ya Mkoa wa Tabora imewaomba viongozi wa dini mbalimbali kusaidia kuwaelimisha waumini wao juu ya umuhimu wa watoto wenye umri wa miaka 14 kupatiwa chanjo ya kuwakinga na saratani ya mlango wa kizazi ili wajitokeza kwa wingi kupatiwa huduma hiyo kuanzia wiki ijayo.


Kauli hiyo imetolewa jana mjini hapa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati anafungua semina ya siku moja ya Kamati ya Huduma ya Afya ya Msingi ya Mkoa huo.Alisema viongozi hao wanayo nguvu kubwa na wafuasi wengi wakitumia fursa hiyo watasaidia kufikisha ujumbe sahihi na kwa wakati na hivyo kuokoa maisha ya wanawake hapa baadaye.

Mwanri alisema ugunduzi wa Chanjo hiyo ya kukinga saratani ya mlango wa kizazi (HPV Vaccine) ni habari njema ambayo inapaswa kuwafikia wananchi wengi ili waweze kuwapeleka watoto wao wa kike kwa ajili ya kuwakinga na ugonjwa wa saratani ya mlango ambao umekuwa ukisababisha upotevu wa maisha ya wanawake wengi.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa ametoa wito kwa watoto wa kike kutojihusisha na vitendo vya ngono katika umri mdogo kwa sababu vinaweza kuharatisha maisha yao na kujikuta wakipata saratani yamlango wa kizazi.Aliongeza kwa watu wazima ni vema wakawa na mpenzi mmoja kwa ajili ya kuwakinga wakinamama kupata tatizo hilo.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa ametoa wito kwa wananchi kujenga tabia ya kwenda mara kwa mara kupima afya zao ili kuweza kujikinga mapema kabla ya tatizo halijawa kubwa.Alisema mara nyingi watu wamekuwa na tabia ya kwenda Hospitali wanapokuwa wanauma na ndio wanapokuta tatizo limeshakuwa kubwa zaidi .

Naye Sheikh wa Mkoa wa Tabora Ibrahim Mavumbi ameipongeza Srikali ya Mkoa wa Tabora kwa kuwashirikisha katika utoaji elimu juu ya umuhimu wa kuwahimiza waumini wao kuhakikisha wanawapewa watoto wanatakiwa kupatiwa chanzo ili waweze kuchanjwa kwa ajili ya kuwakinga na saratani ya mlango wa kizazi.

Aidha aliitaka jamii kuendelea kutii maagizo ya Mwenyezi Mungu ambayo yanakataza zinaa kwa njia na umri wowote ikiwa ni hatua ya awali nay a msingi ya kuwakinga watoto wa kike kupata maambukizi ambaye yanaweza kuwapelekea kupata tatizo hilo.

Kwa upande wa Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tabora Askofu Elias Chakupewa alisema kuwa wao wakiwa viongozi wa Kiroho watajitahidi kutumia nafasi yangu katika kuungana na Serikali katika kuhakikisha wanaelimisha juu ya wananchi kuwapeleka watoto wenye umri kupatiwa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi ili kuokoa maisha yao ya baadaye.

Alisema wao kama kanisa pamoja na jukumu lao la kufundisha mafundisho ya kiroho pia wanalo jukumu la kuangalia maendeleo ya waumini wao na wananchi wengine ya kielimu na kiafya kwa maendeleo ya Taifa.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora(RMO) Gunin Patrick Kamba alisema katika uzinduzi wa chanjo unaonza mapema wiki ijayo mkoani kote zaidi wasichana elfu 30 wenye umri wa miaka ( 14 ) wanatarajiwa kupata chanjo ya kinga ya Saratani ya mlango wa kizazi .

Alisema kuwa chanjo hiyo maalumu kwa watoto wa kike wenye umri wa miaka 14 itazinduliwa Aprili 23 mwaka huu katika Manispaa ya Tabora na Mkuu wa Mkoa kwa niaba ya maeneo mengine mkoani humo.

Chanjo hiyo ya kukinga saratani ya mlango wa kizazi (HPV Vaccine) hapa nchini ilizinduliwa hivi karibuni na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwenye viwanja vya Mbagala Zakhem jijini Dar es Salaam.

No comments: