Saturday, April 7, 2018

RAIS DKT MAGUFULI ATANGAZA AJIRA MPYA 1500 POLISI,ATAKA JKT WAPEWE KIPAUMBELE ,SI WATOTO WA VIGOGO

Na Ripota Wetu,Globu ya jamii

RAIS Dk.John Magufuli ametangaza nafasi 1500 za ajira mpya kwa Jeshi la Polisi nchini huku akitoa maelekezo, anataka vijana wa JKT ndio wapewe nafasi hizo na si kutafuta ndugu,jamaa na marafiki wa makamanda wa wilaya na mikoa.

Amesema kuna tabia imejengeka  pale inapotokea nafasi za ajira kwa ajili ya jeshi la polisi,baadhi ya makamanda wanatafuta watu wao na hivyo hata wakienda kwenye mafunzo wanapewa mafunzo kwa kuangalia waliowapeleka.

Rais Magufuli ametoa tangazo hilo wakati anazungumza na wananchi wa Mkoa wa Arusha baada ya tukio la kuzindua nyumba npya za Polisi zilozojengwa kwa ushirikiano wa Serikali na wadau wa maendeleo wa mkoa huo.Ambapo ameagiza nyumba hizo wapewe askari wa vyeo vya chini.

Amesema kutokana na kutambua na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na Jeshi la Polisi nchini kwa kuhakikisha nchi inakuwa salama hivyo ameamua kutoa ajira mpya 1500 na kufafanua anataka kuona wanaopata ajira hiyo ni watoto wa masikini na si vinginevyo.

"Nataka hizi nafasi ambazo nimezitangaza hapa leo hii zielekezwe kwa JKT ambazo waliamua kujitolea kupata mafunzo na kwa sehemu ni vijana ambazo hawana ndugu, kamanda wa Polisi,mkoa au kiongozi wa serikali." Bali ni vijana ambao wanatoka familia masikini.Hivyo niombe kipaumbele cha ajira hiyo kielekezwe kwa vijana waliopita JKT.Tabia  ya kusikia wanaopewa nafasi ni ndugu wa wakubwa hapana,"amesema Rais Magufuli.

Pia amezungumzia namna ambavyo Jeshi la Polisi linafanya kazi vizuri ya kulinda usalama wa raia na mali zao huku akielezea wakati ameingia madarakani kuliibuka mauaji katika wilaya ya Kibiti na Mkuranga mkoani Pwani.Amefafanua katika mauaji hayo watu 59 wamepoteza maisha na kati yao wamo askari 17 ambao wamepoteza maisha wakati wakilinda usalama wa wananchi wa maeneo hayo.

 Dk.Magufuli amesema askari waliopoteza maisha Kibiti walikuwa na nia ya kuhakikisha nchi inakuwa salama na kimsingi ni Polisi ambao ni watoto wa watanzania masikini.Hivyo amesema hata hivyo polisi wamefanya kazi kubwa ya kuhakikisha mauaji hayo yanakoma na leo kuko salama na hata kama waliokuwa wanatekeleza mauaji  hayo bado wapo Polisi wamejipanga na wanaendelea kuimairisha ulinzi.

"Nakumbuka wakati wa mauaji ya Kibiti yakiendelea hali ilikuwa mbaya,wananchi waliokuwa wanaogopa kufanya shughuli za maendeleo,hata shamba kukawa hakuendeki.Nilitoa maagizo ambayo Jeshi la Polisi wameyafanyia kazi.Hivyo kutoka moyoni kwangu nawapongeza.

" Endeleeni na majukumu yenu na kila ambacho mnakifanya ili nchi ibaki salama mimi nawasapoti.Hivyo huu uamuzi wa kutoa ajira mpya ni kuonesha namna navyotambua majukumu yenu,"amesema Rais Magufuli.

Kuhusu changamoto zinazowabili Polisi amesema anatambua wanakabiliwa na changamoto nyingi za kimaisha na kwamba hata mkewe Mama Janet Magufuli amekuwa akimueleza kwani baba yake ni Polisi."Baba mkwe wangu ni Polisi,mke wangu anajua shida ambazo Polisi hasa wa chini wanazipata,amekaa kota za Polisi Moshi na zile za Ukonga.Baba yake alikua askari Polisi wa vyeo vya chini.Hivyo Polisi mimi ni shemeji yenu na najua shida zenu," amesema Rais Magufuli.

Kuhusu wanaostahili kupandishwa vyeo,Rais ameahidi kulishughulikia hill ingawa ametoa angalizo kwenye sifa za kupanda vyeo wapandishwe badala ya watu kupewa vyeo kwa upendeleo.Amesema kutoa vyeo kwa upendeleo kutakatisha tamaa wengine,hivyo utakapofika wakati haki itendeke na atafuatilia.

Akizungumzia ujenzi wa nyumba hizo amesema umegharimu kati ya Sh.milioni 700 hadi Sh.milioni 800 na swali analojiuliza je akitoa fedha ili zijengwe nyumba kama hizo kwa kila mkoa itawezekana maana hayo ndio mashaka yake kila siku.Ametoa mwito kwa wafanyabiashara nao kuiga mfano wa wenzao wa Arusha ambao wamechangia ujenzi wa nyumba za Polisi huku akiwataka wabunge kupitia fedha za mfuko wa maendeleo ya jimbo kuchangia ujenzi wa nyumba za Polisi.

Amesema akiwa mbunge Jimbo la Chato alichanga Sh.milioni 25 kwa ajili ya nyumba za Polisi na baada ya yeye kuchanga wakatokea wengine nao wakamsaidia katika kufanikisha ujenzi katika jimbo lake la Chato.

No comments: