WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk.Mwigulu Nchemba ametoa rai kuwa ili kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani ni vema jamii ikaacha kufanya matukio ya uhalifu nchini.
Dk.Mwigulu ametoa kauli hiyo leo Bungeni mjini Dodoma wakati anatoa ufafanuzi kuhusu madai ya uwepo wa msongamano wa wafungwa katika magereza mbalimbali yaliyopo nchini ambapo amelieleza Bunge si kweli kwamba magereza yote yana msongamano.
Amesema yapo baadhi ya magereza idadi ya wafungwa ni wengi na hiyo inatkana na wingi wa matukio ya uhalifu kwenye eneo husika na kule ambako hakuna uhalifu mwingi basi nako kwenye magereza hakuna msongamano mkubwa wa wafungwa.
Dk.Mwigulu amesema alifanya ziara katika gereza la Mkoa wa Lindi na baada ya kufuka huko ameshuhudia idadi ndogo ya wafungwa kuliko uwezo wa gereza lenyewe ambalo linao uwezo wa kuhifadhi wafungwa wengi na kufafanua udogo wa wafungwa unatokana na kutokuwepo na matukio mengi ya kihalifu ambayo husababisha mhusika kufungwa.
Ameongeza maeneo ambayo uhalifu ni mwingi unapoenda kwenye magereza nako utakuta idadi ya wafungwa ni kubwa, hivyo ili kuondoa hali hiyo ni jamii kuacha kufanya uhalifu tu."Nitoe rai kuwa ili kupunguza msongmano kwenye magereza yetu njia ni moja tu kuacha kufanya uhalifu.Hiyo itasaidia kuondoa malalamiko kwenye magereza yetu idadi ya wafungwa ni kubwa,"amesema Dk.Mwigulu.
Ameongeza Serikali haipendi kufunga watu ili wakajaze magaerezani bali msongamano huo unasababishwa na watu kufanya matukio ya uhalifu na matokeo yake kufungwa na kusababisha msongamano ambao unaelezwa kuwepo.
Wakati huo huo,Mbunge wa Tarime Mjini Estar Matiko(Chadema) ameelezea namna ambavyo wafungwa na mahabusu wanawake ambavyo wanateseka magaerezani na kuomba wale wenye kesi ndogo waachiwe kwani wapo ambao wamefungwa kwa makosa madogo madogo yakiwamo ya fedha ambapo , kiwango cha fedha anachotumia gerezani ni kikubwa kuliko makosa yake.
Amesema akiwa magereza ya Segerea ameshuhudia kuna mwanameke ambaye amefungwa na anatatizo la kuvuja damu, hivyo kila siku lazima apelekwe hospitalini ambako gharama inakuwa kubwa.Hata hivyo Wizara hiyo imejibu kinachofanyika sasa ni kwa mujibu wa sheria na hivyo kama inaonekana ni tatizo basi ni vema Matiko akapeleka hoja bungeni ili sheria ibadilishwe.
No comments:
Post a Comment