Saturday, April 21, 2018

CCM Z’BAR YAWATAKA WANANCHI KUFUATA MAELEKEZO YA SMZ


NYUMBA ya Farid Issa iliyoezuliwa na upepo na mvua katika shehiab ya Pwani mchangani.
KATIBU wa NEC, Idara ya organazesheni Bakari Hamad Khamis akionyeshwa nyumba za shehia ya sebleni zilizoathiriwa na mvua.

SHEHA wa shehia ya sebleni Khalfan Salum(wa kwanza kushoto) akitoa maelezo ya athari za nyumba zilizopata maafa katika eneo la shehia ya Kwa wazee.
NYUMBA zilizoingiliwa na maji katika shehia ya Kwa wazee Wilaya ya Mjini Unguja.

……………….

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimewataka wananchi kufuata maelekezo na ushauri wa Serikali juu ya kujikinga na maafa yanayotokana na mvua za masika.

Rai hiyo imetolewa na Katibu wa Idara ya Organazesheni CCM Zanzibar Bakar Hamad Khamis, alipotembelea maeneo mbali mbali yaliyoathiriwa na mvua katika Mikoa ya Mjini na Kaskazini Unguja.

Alisema kila mwananchi anatakiwa kuchukua tahadhari kwa kufuata maelekezo ya Serikali hasa kuepuka kujenga katika maeneo hatarishi kwa lengo la kujikinga na madhara hayo yanayosababishwa na mvua za masika zinazonyesha kila mwaka nchini.

Bakari alisema lengo la ziara hiyo ni kuwafariji wananchi wote waliopata majanga sambamba na kuitaka serikali kupitia mfuko wa maafa iharakishe misaada kwa wananchi ambao nyumba zao zimebomolewa na mvua hizo.

Akizungumza Katibu wa Wilaya ya Mjini Fatma Shomari, alisema katika Wilaya hiyo jumla ya nyumba 68 zimeathiriwa na mvua hizo pamoja na kusababisha kifo cha mtoto Ramadhan Juma Khamis (4) katika shehiya ya Sebleni.

“Bado tunaendelea kukusanya taarifa za wananchi mbali mbali waliopata maafa katika Wilaya yetu ili tuziwasilishe kwa serikali kwa ajili ya hatua stahiki za misaada”, alisema Katibu huyo.

Kwa upande wake sheha wa shehia ya Kwa wazee Khalfan Salum alieleza kuwa jumla ya nyumba 130 zenye wakaazi wanaokisiwa kufikia 1300 zimeathiriwa na mvua hizo na wananchi wa maeneo hayo wamehama na kutafuta hifadhi kwa majirani waliopo katika maeneo salama.

Akizungumza mkaazi wa eneo hilo Haji Makame ‘London’ aliiomba serikali kupitia Manispaa ya mjini kuharakisha mradi wa ujenzi wa mtaro mkubwa utakaokuwa ukisafirisha maji yanayotwaama katika maeneo hayo ambayo kwa sasa ni makaazi ya kudumu kwa wananchi.

Aidha Katibu wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mulla Othaman Zubeir alisema zaidi ya nyumba 18 na boti sita za uvuvi aina ya mtando na ngwanda zimeharibiwa na mvua zilizonyesha katika maeneo mbali mbali ya mkoa huo na kuathiri mali za wananchi.

Mbali na maafa hayo Mulla alifafanua kuwa maafa hayo yamesababisha kifo cha mtoto wa mwaka mmoja aliyetumbukia katika shimo la takataka katika shehia ya Chaani kubwa Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja.

Akiwafariji wananchi wa Mkoa huo Katibu wa NEC, Idara ya Organazesheni CCM Zanzibar Bakari Hamad aliuagiza uongozi wa CCM Mkoa huo kusaidia shughuli za ujenzi wa nyumba ya Mkaazi wa shehia ya Mwange Mbaki Makame Ali (54), ambaye nyumba yake imeanguka kutokana na mvua zinazonyesha nchini.

Katibu huo wa Organazesheni Bakari aliwasihi wananchi waliopata maafa kuwa wavumilivu kwa kipindi hichi, huku Chama Cha Mapinduzi kikiendelea kuisimamia serikali iharakishe misaada kwa wananchi waliopata maafa hayo.

Naye mkaazi wa shehia ya Mkwajuni Kero Chumu Juma alikipongeza Chama Cha Mapinduzi kwa kuendeleza utamaduni wa waasisi wa ASP waliokuwa wakiwatembelea wananchi mara kwa mara kwa lengo la kuratibu changamoto zao na hatimaye kuzitafutia ufumbuzi kupitia serikali.

“Nimefurahi sana kuona uongozi wa CCM umekuja kunifariji kwani utamaduni huu ulikuwa umepotea kwa muda mrefu na kwa sasa naona umerudi kwa kasi kubwa, hii inaonyesha wazi kuwa Chama kinarudi kwa wananchi wake”, alisema Mkaazi huyo ambaye ukuta wa nyumba yake ulianguka kutokana na mvua hizo.

Maeneo yaliyotembelewa katika ziara hiyo ni shehia ya Sebleni, Kwa wazee, eneo la Mtumwa jeni, Pwani mchangani, Chaani kubwa, shehia ya Kibeni, Shehia ya Mwange, shehia ya Mkwajuni na Mwanga pwani.

No comments: