Na Zuena Msuya, Dodoma.
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amewateua Wahandisi Saba(7) kutoka Wizara ya Nishati watakaoshirikiana na wakandarasi wanaotekeleza Mradi wa REA III katika kila Kanda ili kuboresha na kurahisisha utekelezaji wa Mradi huo kwa ufanisi.
Dkt. Kalemani alifanya uteuzi huo baada ya kufanya mkutano na Wadau mbalimbali wanaotekeleza Mradi wa REA III wakiwemo, Wakandarasi, Wawekezaji wenye Viwanda vya kutengeneza miundombinu ya umeme kama vile Trasfoma, Mita, pamoja na nyaya za umeme , Mameneja wa Kanda, na Wahandisi wanaosimamia Mradi ya REA III nchi nzima.
Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Hazina ulipo Makao Makuu ya Nchi Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine ulilenga kujadili hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu pamoja na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa Mradi huo.
Dkt.Kalenani alisema Wahandisi walioteuliwa watashirikiana na Wakandarasi wa REA III kutafanya kazi mbalimbali pamoja na kuwa na mpango kazi wa kila wiki wa kila Mkandarasi katika eneo husika ili kusisimamia kwa ukaribu utekelezaji wake.
Pia watarahisisha mawasiliano yamoja kwa moja kutoka kwa wakandarasi hao na Wizara ya Nishati ili kufahamu hatua waliofikia na changamoto watakazokuwa wakikabiliana nazo kwa Lengo la kuzitafutia ufumbuzi wa haraka.
Awali akizungumza katika mkutano huo Dkt.Kalemani aliwataka wakandarasi hao kutumia busara na uzalendo zaidi katika kuwaunganisha Wananchi na Huduma ya Umeme Vijiji kupitia Mradi wa REA III.
Alifafanua kuwa mbali na kuwepo kwa mikataba inayawaongoza wakandarasi hao kutekeleza majukumu yao, lakini Kuna maeneo ambayo wanapaswa kuyafikia pasipo kuangalia makubaliano ya mkataba.
" Nawasihisi Sana wakandarasi mtumie burasa na uzalendo kuunganisha Wananchi kwa mfano utakuta Kijiji kina Shule au Zahanati lakini hakuna umeme ila kimepitiwa na mradi wa umeme lakini kijiji hicho hakipo kwenye orodha ya vile vijiji mlivopewa katika mkataba, nawasihi sana kwa hili,tumieni busara, najua inawezekana kuunganisha ili Watanzania wenzetu wapate huduma Bora za afya au watoto wetu wapate mazingira mazuri ya kujisomea", alisema Dkt. Kalemani
Aidha aliwataka Wakandarasi hao kuendelea kutumia bidhaa za ndani katika kutekeleza Mradi huo pia kununua bidhaa kutoka viwanda tofauti hapa nchini ili kuweka ushindani wa kibiashara pamoja na bei.
Kwa upande wa wenye viwanda , Dkt. Kalemani, aliwataka kuzalisha bidhaa zenye ubora na zenye viwango vinavyotakiwa ili kuendelea kukuza soko la ndani na nje pia kuuza bidhaa hizo kwa Bei nafuu zaidi.
Hata hivyo aliwaahidi wakandarasi hao kuwa kwa sasa Serikali itaharakisha ulipaji wa madeni wanayoidai tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Kwa upande wa TANESCO na REA, Dkt. Kalemani aliwataka kutimiza wajibu wao na kuacha kufanya kazi kwa mazoea kwani bado wananchi wengi wanahitaji kuunganishwa na huduma ya umeme hivyo waongeze juhudi na kufanya kazi kwa kuzingatia weledi.
Aliwataja wa Wahandisi walioteuliwa kusimamia Mradi wa REA III kuwa Ni
Mhandisi Salum Inegeja atakayesimamia Kanda ya Ziwa, Mhandisi John Kitonga Kanda ya Nyanda za Juu, Mhandisi Juma Mkobya Kanda ya Magharibi, na Mhandisi Ahmed Chinemba Kanda ya Kati.
Wengine ni Mhandisi Samuel Mgweno Kanda ya Kaskazini,Mhandisi Christopher Bitesigirwe Kanda ya Pwani pamoja na Mhandisi Styden Rwebangira Kanda ya Kusini.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani( katikati) na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ( kushoto) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Hamis Mwinyimvua( kulia) wakisikiliza maoni ya wadau wanaotekeleza mradi wa REA III katika ukumbi wa hazina wakati wa mkutano wa wadau hao uliofanyika mkoani Dodoma.Washiriki wa mkutano wa wadau wakiwa kwenye mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa hazina Mkoani Dodoma.
Watendaji wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake wakimsikiliza waziri wa nishati Dkt. Medard Kalemani( hayupo pichani) akizungumza wakati wa mkutano wa wadau wanaotekeleza mradi wa REA III uliofanyika katika ukumbi wa hazina Mkoani Dodoma.
wakisikiliza.
No comments:
Post a Comment