Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MKUU wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo, amewahimiza wawekezaji wenye uwezo wa kujenga viwanda vya kubangua korosho na kutengeneza magunia ,kujenga viwanda hivyo ili kuwarahisishia wakulima wa zao hilo .
Aidha amewaasa maafisa ugani mkoani hapo, kuacha kujibweteka maofisini kupigwa viyoyozi na badala yake watoke na kwenda kwa wakulima kutoa elimu mbalimbali za kilimo cha kisasa na chenye tija cha zao hilo.
Alkadhalika, Ndikilo amewataka wakulima wa zao la korosho kufufua mashamba ya korosho pamoja na kupanda miche mipya ya mikorosho ili kuinua zao hilo kimkoa.
Akizindua upandaji wa miche mipya ya mikorosho Ruvu JKT ,Vikuruti wilayani Kibaha Vijiji, alieleza msimu uliopita ulikumbwa na changamoto ya upungufu wa magunia hivyo kuna kila sababu ya kujengwa viwanda hivyo ili mkulima aweze kuwa na uhakika wa kupata magunia.
Mkuu huyo wa mkoa alisema, miaka ya 60/70 mkoa wa Pwani ulikuwa ukizalisha kwa wingi lakini kwasasa mashamba mengi yametelekezwa hivyo kusababisha kushuka kwa kilimo hicho .
“Baadhi ya wakulima walishindwa kupalilia,kuweka dawa na mashamba mengi yalitelekezwa, kutokana na hilo nachukua fursa hii kutoa rai kwa maafisa ugani, mtoke maofisini, mkawaelimishe wakulima wetu kuhusiana na kilimo chenye tija,na muwahimize wapande miche mipya”
“Tumeamua kufanya uzinduzi huu ili kuonyesha umuhimu wa zao hili kimkoa na kitaifa kama mjuavyo serikali yetu ya awamu ya tano imeliingiza zao hili kuwa moja ya mazao ya kimkakati ikiwemo pamba, kahawa ,tumbaku na chai”, Katika kipindi hiki cha kujenga uchumi wa kati na viwanda ili kuinua pato la Taifa “alifafanua Ndikilo.
Hata hivyo ,Ndikilo aliwataka viongozi wa vitongoji na vijiji kuanzisha madaftari ya wakulima kwa lengo la kupata takwimu zao na kuwafuatilia katika mipango mbalimbali ya masuala ya kilimo.
Awali afisa kilimo wa mkoa wa Pwani, Specioza Kashangaki alieleza , kutokana na umuhimu wa zao la korosho, serikali kupitia bodi ya korosho Tanzania imesambaza mbegu bora ili miche itakayopatikana isambazwe bure kwa wakulima.
Alisema kupitia utaratibu huo mkoa huo ulipokea kilo 7,182 zinazokadiriwa kutoa miche milioni.1.039,687 ambazo inatarajiwa kupandwa kote mkoani kipindi cha mvua za masika.
Specioza alitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni kutokuwepo na kumbukumbu sahihi za miche mipya inayopandwa kuanzia ngazi ya kijiji hadi mkoa na kutokuwepo kwa maghala bora ya kuhifadhia korosho hali inayoathiri ubora wa korosho.
“Anabainisha”Kumekuwepo na udanganyifu mkubwa unaofanyika katika maghala ya kuhifadhia korosho ambapo baadhi ya AMCOS zimebainika kusabababisha uzito wakati wa mazao kutofautiana na uzito wa korosho wakati mnunuzi anakabidhiwa korosho zake.
Akitoa taarifa ya uendelezaji wa zao hilo,katika shamba la Ruvu JKT ,meneja wa shamba , Godfrey Mwakabole alisema kitaalamu mikorosho inatakiwa kupandwa kwa nafasi mita 12 kwa mita 12, na kupata miche 28-30 kwa hekari moja.
Kwa mujibu wa Mwakabole alisema, wamepanda miche mipya katika hekari 50 ambapo wamechanganya na zao la mahindi na shamba jingine la hekari 50 wamepanda miche hiyo na wanakaribia kuanza palizi.
Miche ya mikorosho inatakiwa kutunzwa kwa kupaliliwa, kutengenezewa visahani, kupogolea,kudhibiti magonjwa na wadudu ambapo inashauriwa mikorosho ikiwa midogo kuchanganya mazao ya muda mfupi ili wakulima wapate mazao na kipato kwenye eneo moja.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Mhandisi Evarist Ndikilo ,akipanda mche mpya wa zao la mkorosho ,wakati wa uzinduzi wa upandaji wa miche mipya ya mikorosho Mkoani hapo ,uliofanyika ,Ruvu Jkt,huko Vikuruti Kibaha Vijijini.
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo ,alhaj Majid Mwanga ,akipanda mche mpya wa zao la mkorosho ,wakati wa uzinduzi wa upandaji wa miche mipya ya mikorosho Mkoani hapo ,uliofanyika ,Ruvu Jkt,huko Vikuruti Kibaha Vijijini. Picha na Mwamvua Mwinyi
No comments:
Post a Comment