Monday, March 19, 2018

WAIMBAJI MAHIRI WA NYIMBO ZA INJILI KUTIKISA KANDA YA ZIWA TAMASHA LA PASAKA APRILI MOSI


Na Said Mwishehe, Globu ya jamii
KADIRI kengele inavyogonga kuashiria sikukuu ya Pasaka ipo jirani, ndivyo dhahiri kuwa siku za kuelekea Tamasha la Pasaka zinahesabika. Ni Aprili Mosi, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.
Tumezoea mara nyingi kushuhudia Tamasha la Pasaka likifanyika jijini Dar es Salaam lakini waandaaji wa tamasha hilo wameamua mwaka huu iwe zamu ya Kanda ya Ziwa. Hivyo Pasaka hii, watu wa Kanda ya Ziwa watahemewa kwa burudani ya nyimbo zenye kumsifu na kumtukuza Mungu na litanenwa neno la Mungu.
Hivyo Aprili Mosi ni CCM Kirumba, Aprili Pili Tamasha la Pasaka litachukua nafasi kwenye Uwanja wa Halmashauri, mkoani Simiyu. Hakuna ubishi tena katika sikukuu ya Pasaka mwaka huu wakazi wa Kanda ya Ziwa, eneo ambalo litakuwa sahihi kwao kuisheherekea siku hiyo ni kwenye Tamasha la Pasaka.
Wakati siku zikikaribia kuelekea Tamasha la Pasaka kwa mkazi wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa jumla ni kuendelea kumuomba Mungu ili aendelee kukupa uzima na afya njema.Waandaaji wa tamasha hilo, Kampuni ya Msama Promotion, mwaka huu wameamua kuweka vionjo tofauti ili kuhakikisha tamasha hilo linafanyika na  kuacha historia kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa.
 Kila mwanamuziki aliye kwenye chati, nyimbo zake za kumsifu na kumtukuza Mungu zikiwa zinatamba na kusikika, atakuwemo kuburudisha mashabiki wake.Kwa mujibu wa waandaji wa Tamasha la Pasaka, kati ya wengi watakaofanya kweli, atakuwepo mwanamuziki maarufu nchini Rose Mhando na wengine zaidi ya 15 kutoka ndani na nje ya nchi.Inafahamika kuwa Rose Muhando huwa hahitaji utambulisho. Ni mwanamuziki mwanamuziki mkubwa ambaye Muumba wa Mbingu na Ardhi amemjaalia kipaji cha kuimba kilichoambatana na sauti maridadi. Muziki wa Rose Mhando unapopigwa wapo ambao wanasimamisha shughuli zao kwa muda.
Natamani kutaja baadhi ya nyimbo zake atakazoimba siku hiyo lakini acha nikae kimya. Sitaki kukumalizia uhondo. Vema ufike CCM Kirumba kisha Uwanja wa Halmashauri, Simiyu ili macho na masikio yako yapate kumuona na kumsikiliza Rose Mhando. Uwezo wake wa kuimba umemfanya awe nyota ya muziki wa Injili.Kwa Rose Mhando mwenyewe anajua ukubwa wa Tamasha la Pasaka. Wakati anazungumzia tamasha hilo ameeleza wazi amejiandaa vya kutosha. Hivyo atakuwa Kanda ya Ziwa kwa ajili ya kuonesha kile ambacho amewaandalia. Na siku hiyo ataitumia kuzindua albamu yake mpya inayoitwa Jipe Moyo.
Imekuwa kawaida kwa matamasha ya Pasaka kuleta wanamuziki kutoka nje ya nchi. Kwa taarifa tu ni kwamba atakuwepo Ephrem Sekeleti kutoka zambia. Mashabiki wa muziki wa Injili wanamfahamu vema Sekeleti na ubora wa kazi zake.Mkazi wa Mwanza na Simiyu ni zamu yako mwaka huu kupitia Tamasha la Pasaka kuweka historia ya kumshuhudia mwanamuziki Sekeleti akitoa burudani tena ndani ya ardhi ya Tanzania. Karibu Sekeleti wakazi wa Mwanza na Kanda ya Ziwa wanakusubiri kwa hamu kubwa.
Kwa kuwa nimeamua kukutajia baadhi ya wanamuziki, naomba niendelee kwa kumtaja pia mwanamuziki Solomon Mkubwa ambaye anatoka nchini Kenya. Sitaki kumzungumzia zaidi mwanamuziki huyo kwa sababu kazi zake zimesababisha awe mwenye kufahamika na walio wengi nchini kwetu.Mkurugenzi wa Msama Promotion, Alex Msama kwa kutaka wakazi wa Mwanza wapate burudani inayostahili hasa kwa kuzingatia ndiyo mara ya kwanza Tamasha la Pasaka kufanyika Kanda ya Ziwa, alisema aliona itampendeza Mungu pia mkali Christine Shusho akiwepo.
Hakuishia hapo alisema lazima awepo Martha Baraka, Clement Paul, Beatrice Mwaipaja, Upendo Nkone, John Lisu, Christopher Mahangila, John Mlelwa, Jescar Honore, BM na wengine wengi.John Lisu alipokuwa analizungumzia tamasha hilo, aliwahakikishia wakazi wa Mwanza na Simiyu kuwa wamejipanga vema kutoa burudani inayoambana na neno la Mungu kwa ajili yao.
Akawaomba wasikose kwani wanamuziki wote ambao watakuwepo siku hiyo watasafiri kutoka majumbani kwao na kuwafuata wakazi wa Kanda ya Ziwa ili kuwapa burudani yenye tani nyingi.Kuhusu maandalizi ya Tamasha la Pasaka, Msama ameeleza vema kuwa kila kitu kipo sawa. Usalama wa wananchi na mali zao kwa watakaofika siku hiyo upo wa kutosha.Msama amewaomba wakazi wa Mwanza kujitokeza kwa wingi kwenye tamasha hilo ambalo kimsingi mbali ya wanamuziki wa Injili kutoa burudani pia linasambaza ujumbe unaohusu umoja, upendo na mshikamano.
Msama alisema, jambo kubwa la kuenezwa katika tamasha hilo ni kila mmoja kutambua wajibu binafsi wa kuhakikisha amani iliyopo nchini inaendelea kutunzwa.Alisema, mapato ya Tamasha la Pasaka kwa sehemu kubwa yanakwenda kusaidia makundi ya watu wenye uhitaji maalum. Alifafanua: “Miongoni mwa makundi hayo ni watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu na yatima. Hivyo ushiriki wako kwa namna moja au nyingine utakufanya uwe miongoni mwa waliosaidia jamii yenye uhitaji maalum.”

No comments: