Saturday, March 10, 2018

UWT YAUNGA MKONO KAULI YA RAIS MAGUFULI KUZUIA MAANDAMANO

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania(UWT)Gaudentia Kabaka(katikati)akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati akielezea maazimio ya Kamati ya Utekelezaji wa Baraza Kuu la jumuiya iliyokutana leo.Picha na said Mwishehe.

*Watangaza vipaumbele vinne watakavyoanza navyo
*Waomba viongozi kutoa kauli za kudumisha mshikamano


Na Said Mwishehe,Globu ya Jamii


KAMATI ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la Jumuiya ya Wanawake Tanzania(UWT)kwa kauli moja wamempongeza Rais John Magufuli kwa kauli yake ya kuzuia maandamano nchini na kusisitiza wanawake wa Tanzania hawapo tayari kuandamana.

Pia wamempongeza Rais Magufuli na Rais wa Zanzibar Dk.Ali Mohammed Shein kwa usimamizi mzuri wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)kwani wamefanikisha uchumi wa Tanzania kuimarika.Pamoja na hayo Kamati hiyo imetangaza kuanza kazi rasmi za UWT ambapo kati ya vipaumbele ambavyo wamepanga kuvifanya kwa kipindi cha miaka mitano ni 18 lakini wametangaza na vipaumbele vinne.

Hayo yamesemwa Dar es Salaam leo na Mwenyekiti wa UWT Gaudentia Kabaka wakati akitangaza maazimio ya kikao cha Kamati ya Baraza Kuu la jumuiya hiyo.

WAKATAA MAANDAMANO

Akizungumzia kauli ya Rais Magufuli ya kuzuia maandamano nchini,Kabaka amesema wanaukanga mkono kauli hiyo na kusisitiza kuwa wanawake wa Tanzania hawapo tayari kushiriki kwenye kufanya maandamano.

Amesema kuwa jukumu la wanawake wa Tanzania ni kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha nchi inapiga hatua kimaendeleo na kwamba wanalaani kauli za baadhi ya viongozi na watu wengine ambao wamekuwa wakitoa lugha zinazoashiria uvunjifu wa amani nchini.

"Tunaomba viongizi wa dini na viongozi wa kimila kuhakikisha wanatoa kauli za kujenga na kuhamasisha umoja,amani ,upendo ,heshima na mshikamano." Tunampongeza Rais Magufuli na Rais Shein kwa kuendelea kukemea watu wasiotakia nchi yetu iwe na amani kwa kutaka kufanya maandamano au matamko ya uchochezi,"amesema Kabaka.

Ameongeza kuwa "Watanzania hatuna muda wa maandamano ,tuna muda wa kufanya kazi ili kujiletea maendeleo ya nchi yetu tajiri,"amesema.

VIPAUMBELE VINNE VYA UWT

Kuhusu vipaumbele ambavyo wataanza kuvitekeleza mapema kadri iwezekanavyo,Kabaka amesema Kamati ya utekelezaji ya baraza kuu la UWT  limechambua kwa kina vipaumbele 18 vilivyo na kupata vinne watakavyoanza navyo.

Ametaja vipaumbele hivyo ni kwamba UWT itafuatilia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015 hadi mwaka 2020 kwa kuungana na Serikali kupitia idara ya maendeleo ya jamii kuanzia ngazi ya kata mpaka taifa kwa kuhoji na kufuatilia huduma za jamii.

Pia UWT itajiimarisha kiuchumi kwa kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuendelea vyanzo vilivyopo kuanzia ngazi ya kata hadi Taifa."Vipo vyanzo vingi vya mapato ambavyo UWT hawajaviibua na kusisitiza wamejipanga kuanza kujipambanua upya ili kuwa na tija kwa jamii," amesema Kabaka.

Kabaka ametaja kipaumbele cha tatu ni kuongeza wanachama kuanzia ngazi ya chini hadi juu hasa kwa kuzingatia UWT ni chombo cha kisiasa lengo lake pia ni kushika dola.,"Hivyo wanachama hao wapya ni mtaji wa uchaguzi wa kuanzia Serikali za mitaa mwakani na uchaguzo mkuu mwaka 2020,"amesema Kabaka.

Wakati kipaumbele cha nne ni kuwajengea uwezo viongozi,watendaji,wanachama,vikundi vya wanawake vya kiuchumi na kijamii wakiwamo watoto katika masuala mbalimbali ."Katika eneo hili tutaangalia mbinu za uongozi,uchumi na ujasirimali,mapambano dhidi ya rushwa ,mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa wanawake na watoto," amesema Kabaka.


WAMPONGEZA MAGUFULI,SHEIN


Pia Kabaka amesema kuwa kwa kauli moja wanampongeza Rais Magufuli na Rais Shein kwa usimamizi na utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM ambapo hali ya uchumi na maendeleo ya Jamii yameendelea kuimarika.

"Tubashuhudia kukamilika kwa ufanisi mkubwa kabisa wa mipango na miradi ya maendeleo hapa nchini ikiwamo ujenzi wa reli ya standard gauge ya kisasa,umeme wa Stigliers Gorge ,"Ambapo utaongeza kiwango cha upatikanaji umeme kwa maendeleo ya viwanda na kuongeza ushirika wa wakulima wadogo wanawake kwenye viwanda

" Kwa Zanzibar hatua za kupeleka umeme katika visiwa vidogo kama Fundo ,pia tunapongeza kwa fursa iliyotolewa kwa kuwapa wazee pensheni bila kujali itikadi za kisiasa na utolewaji wa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha sita Zanzibar,"amesema Kabaka.

Pamoja na pongezi hizo UWT inashauri Serikali kuandaa muswada wa sheria kwenda bungeni na baraza la wawakilishi la Zanzibar ili utoaji wa asilimia 10 za vijana na wanawake zinatolewa na halmashauri zipate nguvu ya kisheria tofauti na ilivyo sasa.

No comments: