Na Stella Kalinga, Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka ametoa wito kwa wananchi na Viongozi Mkoani humo kutoa ushirikiano kwa wadadisi na wataalam wa Takwimu katika utafiti wa mapato na matumizi ya kaya binafsi unaoendelea hapa nchini ili kuwezesha upatikanaji wa takwimu halisi na sahihi Mkoani humo.
Mtaka ameyasema hayo katika Mkutano wake na waandishi wa habari, wataalam wa Takwimu na Viongozi wa madhehebu ya dini uliofanyika Februari 28 Mjini Bariadi.
Amesema Utafiti huo utatoa makadirio ya uchumi jumla(macroeconomic), hususani matumizi ya kaya kwa ajili ya Pato la Taifa (Gross Domestic Product-GDP), kupata mwenendo wa matumizi ya moja kwa moja ya kaya ili kuwezesha uchambuzi wa hali ya soko na kupata taarifa za umilikaji wa vifaa vya kudumu pamoja na nyenzo za uzalishaji wa kipato.
Amesema kwa mujibu wa sheria namba 9 ya mwaka 2015 kila mwananchi anawajibika kushiriki katika utafiti kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati ili kuiwezesha Serikali kupata takwimu rasmi ambazo zitatumika kupanga na kutekeleza miradi mbalimbali ya Maendeleo.
“ Lengo mama la utafiti huu ni kujua hali ya kipato kwa kaya zetu asije mtu akapotosha kuwa watafiti wana agenda nyingine, ndiyo maana nimeona viongozi wa Dini nao walifahamu hili ili wasaidie kuwaeleza kwa ufasaha waumini wao; Serikali inahitaji takwimu sahihi ili ipange bajeti na kuweka mipango ya maendeleo, niwaombe wananchi na viongozi tutoe ushirikiano” alisema Mtaka.
Aidha, amemuagiza Meneja wa Takwimu mkoani humo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ushiriki wao katika utafiti huu hususani kaya zilizochaguliwa na akamtaka yeye na wataalam wa Takwimu wa Mkoa huo kufanya mikutano katika minada na magulio pamoja na maeneo ya yenye idadi kubwa ya watu yakiwemo ya Makao Makuu ya Wilaya na miji midogo(centers) ili kujenga uelewa kwa wananchi.
Meneja wa Takwimu Mkoa wa Simiyu, Nestory Mazinza amesema tangu utafiti huu uanzae Desemba Mosi 2017 jumla ya kaya 102 zimeshafanyiwa utafiti kati ya 408 zinazotarajiwa kufikiwa mpaka kumalizika kwa zoezi hilo mwezi Novemba 2018.
Naye Bi.Joyce Luhende Mdadisi kutoka Wilaya ya Meatu amesema wanapofanya utafiti huu wanakutana na changamoto mbalimbali na kubwa ikiwa ni baadhi ya wanakaya kuogopa kutoa taarifa zinazohitajika wakati wakihojiwa hali inayopelekea kukosekana kwa taarifa sahihi.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa Dini, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikiristo Tanzania(CCT) Mkoa wa Simiyu, Mchungaji Martine Samson Nketo amesema kupitia ibada watasaidia kuwahamasisha wananchi kushiriki katika utafiti huu na kuwaeleza umuhimu wake katika mipango ya maendeleo inayopangwa na Serikali.
Kaya zilizochaguliwa k kufanyiwa utafiti huu zinatoka katika maeneo 34 (Vijiji/Mitaa) kwenye Wilaya zote tano za Mkoa wa Simiyu yaliyopo katika kata za Nkindwabiye, Nyangokolwa, Sakwe, Nyakabindi, Dutwa, Matongo,Gilya, Sima,Mwamtani, Mwaswale, Mwamapalala, Nhobora, Zagayu, Kinang’eli, Mwanhuzi, Mwandoya, Sakasaka, Mwabuma, Lubiga, Ng’oboko, Busilili, Seng’wa, Masela, Mwamashimba, Buchambi, Badi, Nyalikungu, Kiloleli,Kalemela, Mkula na Ngasamo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na waandishi wa Habari, Viongozi wa Madhebu ya Dini na Wataalam wa Takwimu (hawapo pichani) katika kikao kilichofanyika Ofisini kwake Mjini Bariadi.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Donatus Weginah akifafanua jambo katika kikao cha Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka na waandishi wa Habari, Viongozi wa Madhebu ya Dini na Wataalam wa Takwimu kilichofanyika Mjini Bariadi.
Meneja wa Takwimu, Mkoa wa Simiyu, Ndg.Nestory Mazinza akifanyiwa mahojiano na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kikao cha Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka na waandishi wa Habari, Viongozi wa Madhebu ya Dini na Wataalam wa Takwimu kilichofanyika Mjini Bariadi.
Baadhi ya Viongozi wa Madhehebu ya Dini wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (hayupo pichani) katika kikao kati yake na waandishi wa Habari, Viongozi wa Madhebu ya Dini na Wataalam wa Takwimu katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi.
Mmoja wa Wadadisi akifanyiwa mahojiano na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kikao cha Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka na waandishi wa Habari, Viongozi wa Madhebu ya Dini na Wataalam wa Takwimu kilichofanyika Mjini Bariadi.
Baadhi ya Wadadisi na Waandishi wa habari wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (hayupo pichani) katika kikao kati yake na waandishi wa Habari, Viongozi wa Madhebu ya Dini na Wataalam wa Takwimu katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (wa tatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Meneja wa Takwimu, Mkoa wa Simiyu, Ndg.Nestory Mazinza(wa pili kulia) na baadhi ya Viongozi wa Madhehebu ya Dini mara baada ya kumalizika kwa kikao kati yake na waandishi wa Habari, Viongozi wa Madhebu ya Dini na Wataalam wa Takwimu kilichofanyika Mjini Bariadi.
No comments:
Post a Comment