Thursday, March 8, 2018

Mradi wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi II unaotarajia kuzalisha megawati 240

Na Ismail Ngayonga. 
WAWEKEZAJI wa ndani na nje ya Tanzania wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuwekeza katika miradi mikubwa ya ujenzi wa viwanda nchini kwani kwa sasa mradi wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi II unaotarajia kuzalisha megawati 240 umekamilika kwa asilimia 90.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Meneja Miradi wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), Mhandisi Stephen Manda wakati wa ziara ya wajumbe wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kukagua miradi mbalimbali inayosimamiwa na Bodi hiyo nchini.

Alisema kuwa hadi sasa jumla ya mitambo minne kati ya mitambo nane ya mradi huo tayari imeanza kufanya kazi, ambapo katika gridi ya taifa mitambo hiyo inapekeka megawati, hivyo TANESCO imejipanga kuhakikisha kuwa ifikapo Septemba mwaka huu mitambo yote ya mradi huo imeanza kufanya kazi ili kuyafikia mahitaji yote ya umeme nchini.

Manda alisema kukamilika kwa mradi wa umeme wa kinyerezi II ni moja ya mipango na mikakati ya TANESCO ya kuongeza kiwango cha upatikanaji wa nishati ya umeme nchini, hatua inayolenga kujenga mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa sekta ya viwanda nchini.

Mhandisi Manda alisema kukamilika kwa mradi wa umeme wa kinyerezi II ule wa kinyerezi I wenye umwezo wa kuzalisha megawati 150, na kufanya miradi hiyo kuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 390  na hivyo kutasaidia kurahisisha upatikanaji wa sekta ya nishati ambayo kwa sasa mahitaji yake ni megawati 1100 nchini kote.

"Tukikamilisha miradi yote hii, kutawezesha Tanzania kuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 1500 ikilinganisha na mahitaji yetu halisi ya megawati 1100, hivyo tuwaomba wawekezaji waje kujenga viwanda kwani kwa sasa tuna umeme wa kutosha kupitia vyanzo vyetu mbalimbali ikiwemo makaa ya mawe, gesi na upepo" alisema Mhandisi Manda.

Kwa mujibu wa Manda alisema malengo ya Serikali kwa sasa ni kuzalisha kiwango cha megawati 4000 za umeme kupitia vyanzo mbalimbali pindi miradi mbalimbali ya umeme itapokamilika ikiwemo mradi wa stiegler's gorge unaotarajia kuzalisha megawati 2100 za umeme.

Aidha aliongeza kuwa sasa matumizi ya makubwa ya umeme yapo katika Mkoa wa Dar es Salaam unaotumia kiasi cha Megawati 600 za umeme sawa na asilimia 60% ya umeme wote unaozalishwa nchini kutokana na Mkoa huo kuwa na idadi kubwa ya viwanda.

"Mkoa wa Dar es Salaam ndio kinara wa matumizi ya umeme nchini, lakini mikoa kama ya Arusha, Mwanza, na mingineyo hutumia asilimia 50-55 ya umeme wote nchini, hivyo tumejipanga katika kuhakikisha kuwa tunakuwa na nishati ya uhakika katika kufanikisha dhana ya uchumi wa Viwanda" alisema Barozi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya ERB, Prof. Ninatubu Lema alisema ERB imeridhishwa na maendeleo ya mradi pamoja na juhudi zilizofanywa na TANESCO katika kuhakikisha kunakuwepo na Wataalamu wengi wazalendo katika mradi huo.

Aliongeza kuwa mradi wa kinyerezi II ni miongoni mwa miradi mikubwa ya sekta ya nishati inayosimamiwa na Serikali, hivyo ni wajibu wa TANESCO kuhakikisha kuwa maslahi ya Taifa yanasimamiwa na kuzingatiwa ikiwemo shughuli za kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani katika kuendesha mfumo wa mitambo mbalimbali ya mradi huo.

Naye Kaimu Msajili wa Bodi ya Wahindisi Nchini (ERB), Mhandisi Patrick Barozi alisema Mradi wa Kinyerezi II ni miongoni mwa miradi mikubwa ya maendeleo ya sekta ya nishati iliyopewa kipaumbele na  Serikali ya Awamu ya Tano katika kutekeleza dhana ya uchumi wa viwanda.

Mhandisi Barozi aliwataka wataalamu wa ndani ikiwemo Wahandisi kusimamia kwa kikamilifu viwango vya utekelezaji kwa kuzingatia kuwa mradi huo unatumia vifaa na teknolojia ya kisasa ambayo uchafuzi wa mazingira na hivyo kuongeza ufanisi.
 Wajumbe wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi(ERB), wakiongozwa na Mwenyekiti wao Prof. Ninatubu Lema (mwenye miwani kushoto) wakifuatilia maelezo kuhusu Mradi wa Ujenzi wa Mitambo ya Umeme wa Kinyerezi II,240 MW kutoka kwa Meneja Miradi wa Tanesco Mhandisi Steven Manda wakati wa ziara yao katika mradi huo leo jijini Dar es Salaam.
Meneja Miradi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mhandisi Steven Manda(watatu kutoka kushoto) akiwapa maelezo kuhusu mradi wa ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia wa Kinyerezi II,wajumbe wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi(ERB), wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Prof. Ninatubu Lema (mwenye miwani) wakati wa ziara yao katika mradi huo leo jijini Dar es Salaam. Wapili kushoto ni Kaimu Msajili wa Bodi ya hiyo Mhandisi Patrick Barozi. Mradi huu utazalisha umeme megawati 240 pindi utakapokamilika.
 Mmoja wa Wahandisi wa Shirika la Usambazaji Umeme Tanzania (Tanesco) akionyesha namna wanavyosimamia uongozaji wa mitambo ya kuzalisha umeme katika mradi wa Kinyerezi II walipotembelewa na wajumbe wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi(ERB), wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Prof. Ninatubu Lema (mwenye miwani) leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Kaimu Msajili wa Bodi ya hiyo Mhandisi Patrick Barozi. Mradi huu utazalisha umeme megawati 240 pindi utakapokamilika.
Picha ikionyesha baadhi ya mitambo iliyopo katika mradi wa kuzalisha umeme kutumia gesi asilia wa Kinyerezi II utakaozalisha jumla ya megawati 240 pindi utakapokamilika.
 (Picha na: Frank Shija)

No comments: