Thursday, March 8, 2018

MBOZI KUPATIWA MKOPO WA SHILINGI BILIONI 1.2 KWA AJILI YA UJENZI WA VITUO VYA AFYA


Na WAMJW. Songwe

Halmashauri  ya Mbozi imekubaliwa kupatiwa mkopo wa shilingi bilioni 1.2 toka Mfuko wa Bima ya Taifa (NHIF) kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maboma yapatayo 49 ya huduma za wagonjwa wa nje(OPD) pamoja na nyumba za watumishi.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya,maendeleo ya jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati wa ziara yake ya kikazi  kwenye halmashauri hiyo .Waziri Ummy alisema bado kuna changamoto ya vituo vya kutolea huduma za afya nchini hivyo ameridhia kuwalete  mkopo huo ili kuweza kukamilisha majengo hayo na kuweza kutumika kutoa hudma za afya kwa wananchi.

“Hatuwezi kujenga vituo vya afya kila kata zote 29, muhimu ni kuangalia jiografia ya eneo husika,idadi ya watu pamoja na changamoto za magonjwa,kwahiyo tunataka uhalisia ili kuona wapi tunataka kuweka kituo cha afya na tujenge pale palipo na mahitaji makubwa”Alisema Waziri Ummy.

Kwa upande mwingine waziri huyo aliwapongeza Viongozi wa Wilaya hiyo kwa ongezeko la wanawake wanaojifungua katika vituo vya tiba kwa kufukia asilimia 89 ambapo ni kiwango cha juu kwa takwimu za Taifa katika kuendeleza afya ya mama na mtoto ambapo Kitaifa inatakiwa kufikia asilimia 80 mwaka 2020 ya wanawake wajawazito kujifungulia kwenye vituo vya tiba.

Aidha,amewapongeza kwa ushiriki wa wanaume katika masuala ya  afya ya mama na mtoto,”hili niwapongeze sana kwani nimelipenda jambo hili kwani ushiriki wa wanaume lazima uwepo kama kunata kufikia kuboresha afya ya mama na mtoto lazima tuwashirikishe wanaume”.

Hata hivyo amewataka kuendelea kuhamasisha ujenzi wa vyoo bora kwenye kayapamoja na taasisi zilizopo wilayani hapo” nimeona ni asilimia 37 hivyo muendelee kuhimiza wananchi kuboreshe vyoo vyao kwa sababu tumekua taifa la kulilia dawa dawa na sio kuwekeza kwenye kinga .

Naye Mbunge wa Jimbo la Mbozi Mhe.Pascal haonga alitaja changamoto inayowakabili wilaya hiyo ni ukosefu wa watumishi,gari ya kubebea wagonjwa pamoja na kukosekana kwa kitengo cha watoto njiti kwa Mkoa huo ambapo hivi sasa watoto wanaozaliwa  kabla ya muda wao mara nyingi hukazimishwa kupelekwa hospitali ya Rufaa Mbeya hivyo wakati mwingine hufariki njiani. 

Akisoma taarifa ya Wilaya hiyo Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mbozi Dkt. Abdul Msuya Alisema  wamefanikiwa kufunga mfumo wa kielectroniki wa kukusanya mapato na taarifa za magonjwa  katika hospitali ya wilaya  na tangu kuanza kutumika februari 2017 wastani wa mapato umeongezeka kutoka shilingi 55,000,000 hadi 75,000,000 .
 Msafara ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe.Chiku Galawa(wakwanza) na Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu (watatu) wakati alipofanya ziara ya ukaguzi katika chuo cha Uuguzi wa Afya ngazi ya jamii Mbozi.katikati ni Mkuu wa chuo hicho.
 Wanafunzi wa chuo cha Uuguzi wa Afya ngazi ya jamii Mbozi, wakifuatilia kwa makini ujumbe na maelekezo ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu  wakati alipofanya ziara ya kukagua chuo hicho.
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu  akiwajulia hali wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi. Pembeni yake ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe. Chiku Galawa 
Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu  akisisitiza jambo mbele ya wanafunzi wa chuo cha Uuguzi wa Afya ngazi ya jamii Mbozi Mkoani Songwe na watumishi wa chuo hicho pindi alipofanya ziara ya kukagua chuo hicho.


No comments: