Monday, March 5, 2018

MANGULA AONYA VIONGOZI WA DINI, WANASIASA WANOVURUGA AMANI NCHINI

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Bara, Philipo Mangula amewataka Watanzania kujenga na kuilinda amani nchini na kushangazwa na viongozi wa dini wanaobariki chuki kuwa wanamkosea Mungu.

Pia aliwaonya wanasiasa wanaochochea chuki na kusababisha vurugu na kuwashauri waache kwa kuwa siasa ni uvumilivu na kuumiliana.
Mangula alitoa kauli hiyo jana mjini Musoma alipozungumza na viongozi na wana wana chama wa CCM kwenye ukumbi wa mikutano wa Chama mjini humo.

Alisema kuwa turufu kubwa iliyobaki kwa CCM na watanzania ni amani iliyodumu nchini kwa miaka dahari na hivyo wakati wote wazungumzie taratibu na kutunza amani ya nchi ili kue[uka machafuko vurugu na migogoro inayosababishwa na kuchochewa na wanasiasa.

“Siasa ni kuvumiliana na uvumilivu ndiyo hujenga umoja.Wanasiasa wanapoleta vurugu  wajue wanaoumia ni watoto na wanawake na hivyo tuache chuki tujenge amani ya nchi yetu bila kufanya hivyo hatuwezi kupata maendeleo,”alisema Mangula na kuongeza kuwa;“Nashangaa na kushitushwa na viongozi wa dini wanapojiingiza na kubariki chuki, wanamkosea Mungu.

Machafuko yakishatokea hakuna atakayesalimika kwa kusema mimi ni kiongozi wa dini."Alieleza kuwa kazi ya serikali ni kuwajengea nyumba bali  mazingira mazuri wananchi ili wajijenge na kujifanyia maendeleo.

Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM bara alieleza zaidi kuwa yapo mabadiliko makubwa ya maedeleo mkoani Mara na yote hayo yanafanyika kwa kuwa nchi ina utulivu kwani bila amani ni vigumu kupata maendeleo na hivyo amani kwanza taratibu na kanuni zifuatwe baadaye.

Alisisitiza wanasiasa kuwa wanapochochea chuki na vurugu wanakuwa na passports (hati za kusafiria) mikononi na yakichafuka wanaondoka na kuwaonya wana CCM wasijiingize kwenye migogoro  hasa vijana wa CCM wasijiingize humo.Aidha, Mangula aliwapongeza wabunge wa CCM mkoani Mara walio karibu na wanaotekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM na ahadi kwa wananchi na wapiga kura wao.

Awali Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara Samuel Kiboye Namba Tatu alisema Mangula ni miongoni mwa viongozi waadilifu waliobaki ndani ya CCM na Tanzania.Alimpongeza kwa kumsaidia Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais John Magufuli na kuiwezesha CCM kurudisha heshima kwa wananchi na akawataka wana CCM kumuombea maisha marefu.

“Nakupongeza kwa kumsaidia Rais Magufuli na sisi huku chini hatutamvumilia mtu yeyote asiye na nidhamu wala maadili.Wabunge wa CCM nao wamejitahidi kutekeleza ilani ya Chama hasa mbunge wa Musoma Mjini jimbo  ambalo ni gumu kisiasa,”alisema Namba Tatu.

Kwa mujibu wa habari ambazo gazeti hili imezipata Mangula atakuwa na ziara ya siku tatu katika wilaya za Tarime, Serengeti na Bunda ambako atafanya vikao na viongozi wa serikali na jumuiya za CCM.
Jumanne na Jumatano atakuwa Tarime, Alhamisi na Ijumaa  atakuwa Serengeti kabla ya kuhitimisha ziara yake jumapili wilayani Bunda.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Philipo Mangula akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM wa Mkoa wa Mara jana alipowasili mkoani humo kwa ziara ya kikazi.Kushoto bi Mwenyekiti wa CCM mkoani Mara Samuel Kiboye Namba Tatu na wa pili kutoka kulia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ( NEC) Mkoa wa Mara Christopher Gachuma. Picha zote na Baltazar Mashaka.


 MWENYEKITI wa CCM Mkoa wa Mara, Samuel Kiboye Namba Tatu (kulia), akizungumza na baadhi ya viongozi na wana CCM waliojitokez kumpokea Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Philipo Mangula wa pili kutoka kushoto.

No comments: