Na Maura Mwingira, Dodoma
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Palamagamba Kabudi ( Mb) amesema, Wizara yake pamoja na Taasisi ambazo zipo chini yake, imeendelea kutekeleza ahadi zote za Ilani ya Chama cha Mapinduzi zinazoambatana na na matarajio ya wananchi kutoka kwenye sekta ya sheria.
Waziri Kabudi ameyasema hayo mwishoni mwa wiki, wakati alipokuwa akiwasilisha Mpango na Makadirio ya Bajeti ya Wizara hiyo na Taasisi zake mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria mjini Dodoma.
"Wizara yangu imekuwa ikiwajibika vilivyo katika kuhakikisha kuwa inatekeleza ahadi zote za Ilani zinazoambatana na matarajio ya wananchi kutoka kwenye sekta ya sheria" ameeleza Mhe. Waziri
Akazitaja ahadi hizo kati ya nyingi, kuwa ni, kuendeleza vita dhidi ya adui rushwa na ubathirifu wa mali ya umma, kukuza, kulinda haki za binadamu na utawala wa sheria katika ngazi zote za uongozi, kuimarisha mfumo wa utoaji wa haki na kukamilisha mchakato wa Katiba mpya. Akiwasilisha Mpango na Bajeti ya Wizara na Taasisi zake nane, Waziri aliiomba Kamati hiyo kupitisha zaidi ya Sh. 183.223.058,000bn/- zikiwa ni fedha za mishahara, matumizi mengineyo na miradi ya maendeleo kwa Wizara na Taasisi zake.
Pamoja na kuwasilisha Mpango na Makadirio ya bajeti kwa mwaka 20018/2019, Waziri Kabudi alianisha baadhi ya mafanikio ya Wizara hiyo na taasisi zake katika bajeti ya 2017/2018. Ameyataja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni pamoja na wananchi kupata haki zao kwa wakati kutokana na kupungua kwa mlundikano wa mashauri katika mahakama ya Tanzania kufika chini ya asilimia kumi.
"Mhe. Mwenyekiti mafanikio yaliyopatikana kutokana na utekelezaji wa vipaumbele hadi kufikia tobo ya tatu ya mwaka wa fedha 2017/2018 na kwa kuzingatia Ilani ya Chama cha Mapinduzi, ni pamoja na kuimarisha mifumo ya ulinzi na matumizi ya utajiri na rasilimali za nchi kutokana na kuwekewa miongozo ya kisheria" akabainisha Waziri Kabudi.
Akayataja mafanikio mengine kuwa ni huduma za mahakama kutolewa karibu zaidi na wananchi kwa kujengwa kwa mahakama mpya, kuimarika na kukua kwa mifumo ya ufikiaji wa haki za kisheria na haki za binadamu, kuendelea kuimarika kwa viwango vya usajili kitaifa hususani kwa watoto wa umri chini ya miaka miaka mitano.
Mafanikio mengine ambayo Mhe Waziri ameyaelezea wakati wa uwasilishaji wa Mpango na Makadirio ya Bajeti kuwa ni pamoja na, kuogezeka kwa uelewa wa wananchi kuhusu haki zao, namna ya kudai haki zao na uwezo wa serikali katika kuwapatia huduma ya msaada wa kisheria. Kama hiyo haitoshi, Mhe Waziri Kabudi ameileza Kamati kwamba, katika utekelezaji wa mpango na bajeti ya mwaka 2017/2018, Wizara kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, katika uendeshaji wa mashauri ya daawa ( madai) hadi kufika mwezi february 2018,ili pata ushindi katika mashauri 82 yaliyokuwa na thamani ya shilingi 1,064,581,955,743bn/-.
Kwa mujibu wa Waziri wa Katiba na Sheria ushindi huo umewezesha pamoja na mambo mengine, maamuzi ya serikali pamoja na sheria za nchi kutobadilishwa kwa msingi ya kuikuka Katiba. Mafanikio mengine ambayo yametajwa na Waziri Kabudi ni pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama sehemu ya utelelezaji wa Ilani ya CCM,kuendelea na utoaji wa ushauri wa kisheria kwenye mikataba na makubaliano mbalimbali yanayofanywa na Wizara Idara na Taasisi za Serikali .
Katika eneo hilo , hadi kufikia mwezi February, 2018 Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ilifanya uhakiki na kutoa ushauri wa mikataba 691 yenye thamani ya Shilingi 1,720,026,713,823bn/- na Dola za Kimarekani 1,0884,472,366, mikataba hii ilihusu ununuzi , ukarabati wa majengo, utoaji wa huduma za jamii na ujenzi wa barabara.
Katika uendeshaji wa kesi za jinai, Waziri wa Katiba na Sheria aliieleza Kamati ya kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kwamba, katika kipindi kinachoishia February 2018. Ofisi ya Taifa ya Mashtaka iliendelea na uratibu wa shughuli za upelelezi wa makosa ya jinai mahakamani
Mashauri ya jinai yaliyoshughulikiwa ni pamoja na yaliyohusu wanyamapori, dawa za kulevya, uhujumu uchumi, rushwa na mauaji. Ambapo washtakiwa waliotiwa hatiani walipewa adhabu mbalimbali zikiwamo vifungo, faini na mali kutaifishwa ambapo jumla ya shilingi za kitanzania 2,169 ,983,500 zilitozwa kama faini kutoka kwa washtakiwa.
Aidha kwa upande wa mali zilizotaifishwa ni pamoja na kilogramu 24.5 za dhahabu yenye thamani ya Shilingi 2,012,357,164 na fedha za kigeni kutoka mataifa 15 zenye thamani ya shilingi 908,019,979. Mali nyingine zilizotaifishwa ni pamoja na magari matano ya kifahari aina ya Range Rover Vogue na moja aina ya Audi yaliyokamatwa katika banari ya Dare s Salaam yakisafirishwa kama nguo za mitumba.
Mali nyingine zilizotaifishwa katika kipindi hicho ni pikipiki, mifugo, mafuta na basi la abiria lililokuwa likitumika kusaifirishia meno ya tembo yanazokadiriwa kuwa na thamani ya jumla ya shilingi 3,242,787, 915.
Kwa upande wa uandishi wa Sheria, Wizara kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, iliandaa jumla ya miswaada 15 ya sheria ambayo iliwasilishwa Bungeni na kupitishwa na kuwa sheria. Hali kadharika, iliadaa sheria ndogo na matamko mbalimbali ya serikali yapatayo 164 ambayo yalichapishwa kwenye gazeti la serikali.
Mafanikio mengine ni pamoja na kuanzishwa kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.
Katika kikao cha Ijumaa mafungu yaliyopitishwa na Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Sheria na Katiba ni yale ya Wizara, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka .
Kikao hicho cha uwasilishaji wa mpango na bajeti ya Wizara kilihudhuriwa pia na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Adelardus Kilangi, Katibu Mkuu Profesa Sifuni Mchome , Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Paul Ngwembe, Mkurugenzi Mkuu Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Bw. Biswalo Mganga, pamoja na wawakilishi kutoka Taasisi nyingine zilizo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria.
Taasisi ambazo zipo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria ni Mahakama ya Tanzania, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Tume ya Utumishi wa Mahakama, Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo na Chuo cha Uongozi wa Mahakama-Lushoto.
Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Palamagamba Kabudi amesema Wizara yake pamoja na Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo imeendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi katika sekta ya sheria, ambapo pamoja na mambo mengine, wananchi wanauelewa mkubwa wa namna ya kutafuta na kupata haki yao kisheria. Ameyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati alipokuwa akiwasilisha Mpango na Makadirio ya Bajeti ya Wizara hiyo na Taasisi zake kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria.Pamoja naye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk. Adelardus Kilangi.
No comments:
Post a Comment