Friday, March 9, 2018

HDIF YAWAWEZESHA WANAWAKE TANZANIA KATIKA NYANJA YA UBUNIFU

Na Humphrey Shao, Globu ya Jamii
SERIKALI imesema inaendelea na utaratibu wa ukarabati wa shule kongwe nchini ikiwemo za sekondari na ufundi ili kuwasaidia wanafunzi kujifunza masuala mbalimbali ya ubunifu kwa kutumia sayansi na teknolojia ya kisasa kulingana na mazingira yanavyobadilika.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na  Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayeshughulikia elimu msingi, Dk.Avemaria Semakafu wakati alipokuwa akizungumzia kongamano la Siku ya Wanawake lililoandaliwa na Mfuko wa  Ubunifu wa Maendeleo ya watu kutoka nchini Uingereza (HDIF).


Dk.Semakafu amesema ni vyema wakajirudisha kwenye mazingira yetu ya kitanzania kwa kuwafanya wasichana kuwa wabunifu kuanzia ngazi ya familia na shuleni ili kupata wasichana viongozi.



Amefafanua Shule za Sekondari Ifunda, Tanga, Mtwara na Moshi ambazo tangu awali zilikuwa zikitoa mafunzo ya ufundi, zinaendelea na ukarabati na wanatarajia mwaka wa masomo 2018,19 kuanza kidato cha kwanza.


Amesema ni kosa kubwa lililofanyika la kufuta shule za sekondari za ufundi kwani mwanafunzi anapomaliza anakuwa hana elimu yoyote kuhusu masuala ya ubunifu.

Ameongeza masuala ya ubunifu yamewekewa mkazo katika elimu ya juu pekee, hivyo inawaacha wanafunzi wengi wa elimu za chini.


"Elimu ni haki ya msingi kwa kila mtanzania na elimu bure imesaidia watoto wengi kuandikishwa elimu ya msingi.Kurudisha shule za sekondari za ufundi kutasaidia uwiano kati ya wanawake na wanaume wanaofanya masuala ya ubunifu," amesema Dk.Semakafu.


Amesema Tanzania ya viwanda itawaacha wengi chini na wengine wenye elimu ya watakaochujwa endapo hawajifunza masuala ya sayansi na teknolojia mapema.


‘’Shule za ufundi zinasaidia watu wengi waliopata elimu hii mapema zaidi na humpa mtoto kuchagua kama anapenda masuala ya ufundi au la. Kuboresha shule hizi kutasaidia sera ya muelekeo wa Tanzania ya viwanda na si kubaki pale ilipo,’’ amesema.

Aidha, amesema udahili shule za msingi wasichana ni wengi kuliko shule za sekondari na vyuo vikuu, hivyo wanapaswa kuweka mikakati kwa kuangalia ni changamoto gani zinazowakabili wanafunzi hao.


Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Idara ya maendeleo ya Kimataifa (DFID), Jane Miller amesema Serikali ya uingereza imesaidia wasichana milioni 5.3 wa shule za sekondari na msingi na kuokoa maisha ya wajawazito na watoto 103,000.



Miller amesema Serikali hiyo imesaidia kuwapatia mtaji wanawake milioni 36 kwa ajili ya kujiinua kiuchumi kwa kutumia ubunifu mbalimbali.


"Serikali ya Uingereza kupitia Mfuko wa Maendeleo ya watu (HDIF) umewekeza hapa nchini zaidi ya Euro milioni 39 kwa ajili ya kusaidia masuala ya ubunifu yanayoleta matokeo chanya katika elimu, afya, maji na usafi wa mazingira,"amesema Miller.

Naye, Naibu Mkurugenzi wa HDIF, Joseph Manirakiza amesema wameandaa kongamano hilo ili kutoa fursa kwa watu kujifunza namna wanawake walivyofanikiwa katika masuala ya ubunifu.


"Tunayo miradi mbalimbali inayowasaidia wanawake kujiinua kiuchumi na lengo ni kuwafikia wanawake wote wa mijini na vijijini ili kuleta usawa wa kijinsia na kushiriki katika maendeleo,"amesema.
 Naibu Kiongozi  Mfuko wa  ubunifu wa Maendeleo ya watu kutoka nchini Uingereza (HDIF), Joseph Manirakiza akizungumza juu ya  kongamano hilo ili kutoa fursa kwa watu kujifunza namna wanawake wamefanikiwa katika masuala ya ubunifu na kuleta maendeleo katika jamii inayoiwazunguka.
 Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayeshughulikia elimu msingi, Dk Avemaria Semakafu  akizungumza katika kongamano la Siku ya Wanawake lililoandaliwa na Mfuko wa  ubunifu wa Maendeleo ya watu kutoka nchini Uingereza (HDIF)

 Mmoja wa watu waliokuwa katika uchangiaji mada aliekuwa mrembo wa Miss Tanzania na kutwa taji la urembo wa Afrika Nancy Sumari akizungumza jambo wakati wa kongamano la Wanawake lililoandaliwa na mfuko wa  ubunifu wa Maendeleo ya watu kutoka nchini Uingereza (HDIF)
 Wadau mbalimbali waliofika katika Kongamano la Wanawake lililoandaliwa na Mfuko wa  ubunifu wa Maendeleo ya watu kutoka nchini Uingereza (HDIF)
 Mtaalamu wa Mawasiliano kutoka shirika la Dot Tanzania, Ndimbuni Msongole akizungumza jambo juu ya ubunifu kaytika nyanja ya mawasiliano wakati wa Kongamano la Wanawake na ubunifu lililoandaliwa na Mfuko wa  ubunifu wa Maendeleo ya watu kutoka nchini Uingereza (HDIF)
 Mkurugenzi wa tasisi ya Empower, Miranda Naiman akizungumzia namna walivyoweza kuwawezesha wanawake na vijana katika kujikwamua wakati wa kongamano lililoanadaliwa na Mfuko wa  ubunifu wa Maendeleo ya watu kutoka nchini Uingereza (HDIF)
 MWanawake kutoka tasisi ya Pink Ijabu walioshiriki katika kongamano hilo lililoandaliwa na mfuko wa  ubunifu wa Maendeleo ya watu kutoka nchini Uingereza (HDIF)
washiriki wa kongamano la siku ya Wanawake Duniani lililoandaliwa na  mfuko wa  ubunifu wa Maendeleo ya watu kutoka nchini Uingereza (HDIF)

No comments: