Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Emmanuel Kibona akitoa elimu ya
Kinga na Tahadhari Dhidi ya Majanga ya moto kwa Walimu na Wanafunzi wa Shule ya
Secondari Azania (Picha na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji)
Na Nasibu Mgosso.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ndicho chombo chenye jukumu la kuzuia na
kukabiliana na majanga mbalimbali kama mafuriko , Tetemeko la Ardhi,
ajali za vyombo vya usafiri na usafirishaji, kuporomoka kwa majengo,
migodi, pamoja na matukio ya moto.
Mara kwa mara, majanga ya moto yamekuwa yakitokea katika jamii yetu
kwa sababu moto ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Utafiti
umethibitisha kwamba, vyanzo vingi vya moto ni sisi wenyewe
(binadamu) kutokana na uzembe, hujuma au kutokukuwa na elimu ya
Tahadhali na Kinga Dhidi ya Moto.
Aidha, matukio ya moto yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika shule
za bweni hapa nchini hususani shule za sekondari, na kusababisha
uharibifu wa miundo mbinu kama vile Mali, majengo na wakati mwingine
majeraha au vifo kwa wanafunzi wetu na kuleta simanzi na sintofahamu
kwa Wananchi na Taifa kwa ujumla .
Picha ni sehemu ya bweni iliyoathirika na moto na kuteketeza mali za Wanafunzi.
Uchunguzi wa moto (Fire Investigation) umebaini sababu za matukio
hayo ni matumizi mabaya ya umeme yanayofanywa na wanafunzi kwa
kujiunganishia nyaya za umeme wenyewe bila kuwa na weledi iliwapate
sehemu za kuchaji simu na heater za kuchemshia maji kwa kificho kwa
sababu Wanafunzi hawaruhusiwi kuwa na simu wala heater pindi
wanapokuwa shuleni.
Lakini pia sababu nyingine ni matumizi ya mishumaa, unapokatika umeme
wakati wa kujisomea. Shule nyingi zinajaribu kuzuia mabweni kutumika
kama sehemu za kujisomea, lakini bado wapo baadhi ya Wanafunzi
wanaamua kujisomea ndani ya mabweni bila kuchukua tahadhari
yoyote na wanapopitiwa na usingizi, uacha mishumaa inaendelea kuwaka
na hatimaye kusababisha ajali ya moto.
Utakumbuka miaka kadhaa iliyopita matukio kama haya ya kuungua kwa
shule yalileta majonzi makubwa kwa kuangamiza maisha ya Wanafunzi
wengi. Kuungua kwa shule ya Shauritanga Mkoani Kilimanjaro mwaka
1994 ambapo zaidi ya wanafunzi 40 walipoteza Maisha pamoja na Mali.
Mwaka 2009 shule ya sekondari Idodi Mkoani Iringa iliteketea kwa moto na
zaidi ya wanafunzi 20 walipoteza Maisha pamoja na Mali. Hiyo ni mifano tu
lakini matukio ya kuungua kwa shule ni mengi sana hapa nchini.
Ili kupunguza matukio hayo, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeanzisha Fire
klabu katika shule mbalimbali za Msingi na Sekondari ili kupata wajumbe
watakaoliwakilisha katika shule na makazi yao.
Kwa kutumia fire klabu, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limejenga ukaribu
mkubwa na Wanafunzi wa shule hizo, hatua inayosaidia kuwapa elimu
stahiki ya kukabiliana na majanga ya moto.
Changamoto iliyopo ni mapokeo ya baadhi ya Viongozi wa shule
kutokuwa tayari kuruhusu shule zao kuanzisha klabu za Zimamoto
zinazosimamiwa na kuratibiwa na Jeshi hilo ambapo mpaka sasa ni shule
100 ndizo zilizofungua klabu hizo kwa nchi nzima.
Kama nilivyo eleza hapo mwanzo, lengo la klabu hizo ni kuwapa fursa
wanafunzi kuwa familia moja na wataalamu wa Zimamoto. Ukaribu huo
hutumika kwa wazimamoto kuwapa mbinu mbalimbali za kuzuia na
kukabiliana na vyanzo vya moto.
Lakini kwa upande wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, ni kupanua wigo wa
kuwa na idadi kubwa ya watu, wanaoifahamu vyema elimu hiyo na
kuwa mabalozi wazuri watakao liunganisha Jeshi na jamii kwa kufikisha
elimu hiyo, Mijini na Vijijini na hatimaye kuweza kupunguza na
kutokomeza kabisa majanga.
Wito wangu kwa wamiliki wa shule, walipokee jambo hili kama ukombozi
kwao kupunguza majanga ya moto katika shule zao.
Tukishirikiana tutapunguza majanga ya moto, na Taifa litakuwa salama.
Mungu ibariki Afrika Mungu ibariki Tanzania.
No comments:
Post a Comment