Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB) imeazimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kuendesha mafunzo ya kilimo kwa wanawake wakulima wa Chama cha Ushirika Ruvu (CHAURU) ili kuwajengea uwezo ili Kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.
Akizungumza na wanawake hao, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TADB, Bibi Rosebud Kurwijila alisema kuwa moja ya malengo ya kimkakati ya TADB ni kuhamasisha kilimo cha kisasa na cha kibiashara kwa wakulima wadogo wadogo hasa wanawake na vijana nchini.
Aliongeza kuwa Benki ya Kilimo ina mikakati ya dhati katika kuwasaidia wakulima wanawake nchini ili hasa katika kutekeleza kwa vitendo Kauli mbiu ya kitaifa ya Siku ya Wanawake Duniani Mwaka huu 2018 isemayo ”Kuelekea uchumi wa viwanda tuimarishe usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake vijijini.’’
“Katika hili TADB inatambua mchango wa wanawake katika sekta ya kilimo ambao wengi wao wako vijijini na ndio wazalishaji wakubwa wa chakula katika taifa letu,” alisema.
Bibi Kurwijila alisema kuwa kulingana na takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu asilimia 69 ya wanawake nchini wanajishughulisha na shughuli za kilimo hivyo kiwango hiki kinazidi kiasi cha wanaume wanaojishughulisha na kilimo ambao ni asilimia 64 tu.
Kuhusu changamoto zinazowakabili wakulima nchini, Bibi Kurwijila alisema kuwa mwaka 2017 TADB iliunda sera rasmi inayotoa mwongozo wa namna ya kuwafikia wanawake katika utoaji mikopo ya kilimo na huduma nyingine za kibenki ikiwemo utoaji mafunzo.
“Kwa mujibu wa sera hii angalau asilimia 20 ya mikopo na huduma za kibenki zinazotolewa kwa wakulima zinatakiwa kuwanufaisha wakulima wanawake,” alisema.
TADB ilitumia nafasi hiyo kwa kuwapatia hundi ya shilingi milioni nne kwa ajili ya ununuzi mashine ya kusukuma maji ili kutatua changamoto za maji ya umwagiliaji mboga mboga iliyokuwa inawakabili wakulima hao.
Katika wiki muhimu tunayoelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, na kama mdau mkubwa wa kilimo, TADB iliandaa mafunzo kwa wakulima wanawake walio chini ya mwavuli wa CHAURU na Faraja Women’s Group kwa ajili ya kutambua mchango wa wanawake katika kilimo nchini.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TADB, Rosebud Kurwijila akizungumza na wanawake wanaojishughurisha kilimo walio chini ya mwavuli wa CHAURU na Faraja Women’s Group (hawapo pichani).
Afisa Biashara Mwandamizi wa TADB, Eunice Mbando akizungumza na wanawake kuhusu fursa za mikopo nafuu kwa wakulima itolewayo na Benki ya Kilimo nchini.
Baadhi ya wanawake wanaojishughurisha kilimo walio chini ya mwavuli wa CHAURU na Faraja Women’s Group wakifuatilia kwa makini mafunzo yaliyotolewa na Benki ya Kilimo nchini.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TADB, Bibi Rosebud Kurwijila (aliyekaa kwenye kiti) akiwa katika picha ya pamoja na wanawake wanaojishughurisha kilimo walio chini ya mwavuli wa CHAURU na Faraja Women’s Group.
Wanawake wanaojishughurisha kilimo walio chini ya mwavuli wa CHAURU na Faraja Women’s Group wakionesha mfano wa hundi waliyoabidhiwa kwa ajili ya kununulia mashine ya maji.
No comments:
Post a Comment