Monday, February 5, 2018

WAZIRI MKUU USO KWA USO NA WADAU WA PAMBA FEBRUARI 15-16 JIJIN MWANZA


WAZIRI Mkuu Kassimu Majaliwa, ameitisha kikao cha wadau wa pamba nchini, ili kujadili namna bora ya kuongeza tija ya zao hilo.

Kikao hicho kitakachofanyika jijini Mwanza Februari 15 hadi 16, 2018, kinatarajiwa kuondoa sintofahamu iliyogubika sekta ya pamba, kuhusu mustakabari wa kilimo cha mkataba kutokana na kusudio la Serikali kuanzisha ununuzi wa pamba kwa njia ya mnada kupitia vyama vya ushirika.  

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya kuonesha kusudio la kusitisha kilimo cha mkataba, na uwezekano wa pamba kuuzwa kwa njia ya mnada.Kulingana na taarifa iliyotolewa jana na Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba, kikao hicho muhimu kimelenga kuondoa hali ya sintofahamu, juu ya kilimo cha mkataba na uuzwaji wa zao hilo kwa njia ya mnada.Kusudio hilo la Serikali la kuuzwa pamba kwa njia yamnada, limeonekana kuleta wasiwasi kwa makampuni yaliyowekeza kwenye sekta hiyo muhimu katika uchumi wa nchi. 
Mkoa wa Tabora Agrey Mwanri akifafanua jambo kwa Waziri wa Kilimo Charles Tizeba kabla ya kuanza ziara ya kuona utekelezaji wa kilimo cha Pamba na uzalishaji wa mbegu bora za pamba za UKM08 Msimu 2017/2018 uliofanyika jana tarehe 04 feb 2018.
Afisa Kilimo wilaya ya Igunga Erasto Konga akiwasilisha taarifa ya wilaya kwa Waziri wa Kilimo.
Akiwa ameambatana na mwenyeji wake Mkuu wa mkoa huo Agrey Mwanri, Waziri Tizeba pia alipata nafasi ya kuzungumza na baadhi ya wakulima na kugundua kuwa bado elimu ya unyunyiziaji dawa haijakaa sawa.
Na hapa ikawa nafasi ya kutoa darasa upya kwa mkulima huyu.
"Tunakwenda kujadiliana nao wanunuzi hawa wa pamba, hususani walioingia kilimo cha mkataba. Asilimia 40 ya Watanzania wote wanategemea uchumi wao kupitia pamba," alisema Waziri Tizeba.Alikuwa akizungumza muda mfupi baada ya kuwasili kwa ziara ya kukagua mafanikio ya zao la pamba, Wilaya ya Igunga mkoani Tabora.
Waziri Tizeba akitizama namna mkulima wa pamba ambaye ni Mwalimu wa Shule ya msingi , Bw. Faustine Francis anavyo nyunyizia dawa. 
Afisa ugani Kata ya Mbutu Iddi Uledi akitoa maelezo kwa Waziri Tizeba.
Shamba la zao la Pamba wilayani Igunga.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Gaki Investment inayojihusisha na ununuzi wa pamba, Gasper Gaki, alisema: “Tunakingoja kwa hamu sana kikao hiki na Waziri Mkuu, naamini kitakuwa na mafanikio.”

Katika hatua nyingine, Waziri huyo mwenye dhamana ya Kilimo alisifu juhudi za kilimo cha pamba, ambapo Mkoa wa Tabora umevuka lengo lake la uzalishaji zao hilo.

Zaidi ya kilo milioni 187 zinatarajiwa kuvunwa mwaka huu mkoani hapa, kwamba kasi ya kilimo hicho inaleta tija kiuchumi na pato la taifa.

Idadi hiyo ni kiwango cha juu, kuliko matarajio ya awali ya kuvuna zaidi ya kilo milioni 136 za pamba, msimu huu.

Waziri Tizeba alisema kuwa, takribani sh. Bilioni 50 zinahitajika kwa ajili ya manunuzi ya dawa za kuuwa vijidudu vya mazao.

"Haijawahi kutokea. Tumepata mafanikio makubwa sana ya kilimo cha pamba mwaka huu. Viongozi na wananchi hongereni sana, mtauza kwa bei nzuri.

Waziri huyo aliagiza maofisa kilimo 30 waliopo wizarani kwake, na wengine 30 kutoka Kituo cha Utafiti cha Ukiriguru kuanzia wiki ijayo, kusambazwa Mikoa ya Tabora, Simiyu, Shinyanga na Mwanza.

Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba nchini, Marco Mtunga, alisisitiza wakulima wa zao hilo kupulizia dawa kwa kufuata ushauri wa wataalamu wa kilimo.

"Ukipuliza dawa mchana hautauwa hawa wadudu. Muda wa kupuliza ni asubuhi, mwisho saa 3:00 asubuhi, baadaye tena jioni," alisema Mtunga.
Awali, Ofisa Kilimo Mkoa wa Tabora alizitaja wilaya nyingine za mkoa huo na idadi ya uzalishaji kilo kwenye mabano kuwa ni Kaliua (kilo 11,554,000).

Nzega (kilo 16,300,000), Urambo (4,307,000) na Uyui inayotarajia kuzalisha zaidi ya kilo milioni 6.81.

No comments: