Thursday, February 8, 2018

UNICEF YATOA MSAADA WA LAPTOP 200 KWA WIZARA YA AFYA ZANZIBAR

Waziri wa Afya wa Zanzibar Mahmoud Thabit Kombo kushoto na akikabidhiwa Msaada wa Laptop 200 zenye thamani ya zaidi ya Shil.Millioni 400 kutoka kwa Mwakilishi wa UNICEF Zanzibar Francesca Morandin ili kuimarisha usimamizi wa mfumo wa taarifa za Afya kwa wizara hiyo. Picha na Abdallah Omar-Maelezo Zanzibar


Mwakilishi wa UNICEF Zanzibar Francesca Morandin akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya Msaada wa Laptop 200 zenye thamani ya zaidi ya Shil.Millioni 400 kwa Wizara ya Afya Zanzibar ili zisaidie kuimarisha usimamizi wa mfumo wa taarifa za Afya kwa wizara hiyo. Picha na Abdallah Omar-Maelezo Zanzibar


Waziri wa Afya wa Zanzibar Mahmoud Thabit Kombo akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya Msaada wa Laptop 200 zenye thamani ya zaidi ya Shil.Millioni 400 kutoka shirika la UNICEF ili kuimarisha usimamizi wa mfumo wa taarifa za Afya kwa wizara hiyo.

Picha na Abdallah Omar-Maelezo Zanzibar

……………..

Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF limetoa msaada wa Komputa aina ya Laptop 200 kwa Wizara ya Afya ya Zanzibar ili kuimarisha usimamizi wa mfumo wa taarifa za Afya kwa wizara hiyo.

Laptop hizo zenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 400 zimetolewa ikiwa ni mwendelezo wa UNICEF kuiunga mkono Serikali katika kuimarisha huduma za matibabu hasa ya akinamama na watoto.

Akikabidhi Msaada huo katika Ukumbi wa Wizara hiyo Mnazi mmoja Mwakilishi wa UNICEF Zanzibar Francesca Morandin amesema upatikanaji wa taarifa sahihi ni jambo muhimu linalofaa kupewa kipaumbele.

Amesema uwepo wa taarifa sahihi za Wajawazito na watoto huisaidia Serikali kujua idadi ya ongezeko la watu wake hali inayopelekea kupanga mipango vyema ya matibabu kulingana na idadi ya watu husika.

Amewataka Watendaji kwa ujumla kuunga mkono juhudi zinazotolewa na UNECO ili kuhakikisha afya za Watoto na Wajawazito zinaimarika.

Francesca ameongeza kuwa Shirika hilo la UNICEF litaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika juhudi zake za kimatibu na kuipongeza Srikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendelea kutoa matibabu bure kwa wananchi wake.

Amefahamisha kuwa Zanzibar inapiga hatua mbele kwa upande wa Matibabu na kupongeza juhudi zinazofanywa na Serikali kuwashajiisha Wajawajizito kushiriki huduma hizo muhimu katika maisha yao. “Zanzibar zaidi ya asilimia 99 ya Wajawazito hushiriki katika Kliniki mbalimbali walau mara moja katika kipindi chao cha ujauzito. Hii inawezekana kwamba imechangiwa na juhudi za Serikali za kuyafanya matibabu bure”Alipongeza Francesca.

Kwa upande wake Waziri wa Afya wa Zanzibar Mahmoud Thabit Kombo amelishukuru Shirika la UNICEF kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar hasa katika sekta ya Afya.

Amemuahidi Mwakilishi huyo kwamba Msaada uliotolewa utatumika vyema ili kutimiza malengo ya Shirika hilo.

“Cha bure mara nyingi vitu vya bure havitunzwi vyema lakini Laptop hizi lazima tujitahidi kuutumia vyema..Laptop ziendelee kudumu na taarifa zinazohitajika zote kuanzia Dawa, Wajawazito, Watoto nakadhalika zote ziwekwe kwenye mfumo unaotakiwa”Alisema Waziri Kombo.

Waziri Kombo amesema Zanzibar inaendelea kupokea pongezi kutoka pande zote za Dunia kwa namna Serikali inavyojitahidi katika kutoa huduma bora za matibabu na hivyo msaada huo utazidi kuimarisha huduma hizo.

Laptop hizo zitagawiwa katika Vituo vyote vya matibabu Unguja na Pemba ili kuimarisha usimamizi wa mfumo wa taarifa za Afya kwa wizara hiyo.

IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR

No comments: