Mtendaji-Mahakama ya Hakimu Mkazi-Musoma, Bi. Zilliper Geke akiongea jambo katika mahojiano maalum. (Picha na Mary Gwera, Musoma-Mara)
Muonekano wa sehemu ya jengo la Mahakama Kuu-Musoma likiendelea kujengwa.
Mafundi wakiendelea na ujenzi.
Wahandisi wa Mradi huo wakitoa maelezo ya hatua ya ujenzi waliyofikia kwa katika ujenzi wa jengo hilo.
Mafundi wakiendelea na kazi ya ujenzi wa ghorofa ya kwanza ya jengo hilo litakalokuwa na ghorofa mbili.
Wahandisi wa Mradi huo wakitoa maelezo ya hatua ya ujenzi waliyofikia kwa katika ujenzi wa jengo hilo.
Na Mary Gwera
KAMA ilivyo kwa huduma nyingine katika jamii, huduma ya upatikanaji wa HAKI ni miongoni mwa huduma ambazo wananchi wanahitaji kwa wakati bila longolongo, kufuatia uhitaji huu wa Wananchi, Mahakama ya Tanzania imekuwa na inaendelea katika jitihada za kuboresha huduma ya upatikanaji wa haki kwa kujenga na kukarabati miundombinu bora na wezeshi ya kutolea haki.
Tukiangazia Mkoa wa Mara ambapo kwa kipindi kirefu wananchi wake wamekuwa na wanaendelea kupata shida hususani katika upatikanaji wa huduma ya haki kwa ngazi ya Mahakama Kuu ambapo Mwananchi mwenye kesi anatakiwa kusafiri kwa kilomita zipatazo 218 kwenda Mahakama Kuu Mwanza ili kutafuta haki yake.
Kulingana na uhitaji mkubwa wa huduma ya Haki nchini, Mahakama ya Tanzania imekuwa ikifanya ujenzi na matengenezo ya majengo yake kwa awamu kulingana na hali ya bajeti, kwa sasa Mahakama ya Tanzania imeanza ujenzi wa Mahakama Kuu katika mikoa miwili ambayo ni Mara na Kigoma.
Katika mahojiano maalum na Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma, Bibi. Zilliper Geke yaliyofanyika ofisini kwake Mahakama ya Mkoa-Musoma, Februari 13, Bi. Zilliper anasema kuwa ujenzi wa Mahakama Kuu unaoendelea katika Kanda hiyo umeleta faraja na ukombozi mkubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Mara kwani wamekuwa wakisumbuka kwa muda mrefu kusafiri kilometa kadhaa kwenda mkoani Mwanza kutafuta haki zao kwa ngazi ya Mahakama Kuu.
“Kwakweli wananchi wa Mkoa huu na hata wateja wanaokuja katika Mahakama ya Mkoa, wanaonekana kufurahia ujenzi wa Mahakama Kuu Musoma ambapo pindi itakapokamilika itawaondolea usumbufu wa kusafiri hadi Mwanza kupata huduma” alieleza Mtendaji huyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya D.F MISTRY& CO (1974) LTD, Kampuni ambayo imepata tenda ya ujenzi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Musoma, Eng. Bhavesh anasema ujenzi wa Mahakama hiyo ulioanza rasmi Novemba 11, 2017 unaendelea vizuri kama ratiba ilivyopangwa.
“Ujenzi wa Mahakama Kuu Musoma umepangwa kumalizika ndani ya miezi 18 ambao ni sawasawa na mwaka mmoja na nusu, hivyo kwa hatua tuliyofikia sasa tuko mbele zaidi hali ambayo inaridhisha kuwa ujenzi huu tutamaliza ndani ya muda kama hakutakuwa na changamoto yoyote,” alisema Mkurugenzi huyo.
Aidha Eng. Bhavesh anabainisha juu ya hatua ya ujenzi iliyofikiwa kwa sasa kuwa ni ujenzi wa ghorofa ya kwanza ‘first floor’ ya jengo hilo ambayo anasema kuwa itachukua muda wa takribani mwezi mmoja hadi kukamilika kwa hatua hiyo.
“Hatua hii ya ujenzi itatuchukua takribani mwezi mmoja toka sasa, kwa sasa tunakwenda vizuri, hivyo mara baada ya kukamilika kwa hatua ya ujenzi ya ghorofa ya kwanza tutaendelea na ghorofa ya pili, na kazi hii ya ujenzi wa jengo zima la Mahakama Kuu Musoma inatakiwa kukamilika ifikapo Aprili 19, 2019,” alieleza Eng. Bhavesh.
Akionyesha kufurahishwa na ujenzi wa Mahakama hiyo, kwa upande wake Wakili wa Kujitegemea-Mkoani Mara, Bw. Thomas Makongo anaeleza kuwa uamuzi wa Mahakama ya Tanzania kujenga Mahakama Kuu-Musoma utasaidia kuharakisha ‘speed up’ mashauri na kuipunguzia mlundikano wa Mashauri Mahakama Kuu-Kanda ya Mwanza.
“Hata hivyo naweza kusema kuwa, ujenzi wa Mahakama Kuu Mara umechelewa sana kwa sababu mkoa huu una mashauri mengi ya Jinai hususani ya mashauri ya Mauaji, kwahiyo kukosekana kwa Mahakama Kuu katika Mkoa huu kumechangia ucheleweshaji wa mashauri haya kusikilizwa na kumalizwa kwa wakati,” alisema Wakili Makongo.
Aidha, Wakili huyo anaendelea kusema kuwa kuwepo kwa Mahakama Kuu Mara kutasaidia pia kushughulikia migogoro dhidi ya Watendaji wa Mahakama kwa ukaribu zaidi.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Ujenzi, Mahakama ya Tanzania, Mhandisi Khamadu Kitunzi amesema kuwa ujenzi wa Mahakama Kuu Musoma ambao unasimamiwa na ‘HAB Consult’ na ‘Mbega Associates’ unaenda sambasamba na Ujenzi wa Mahakama Kuu Kigoma.
“Kukamilika kwa Mahakama Kuu hizi mbili kutafanya idadi ya kuwa na jumla ya Kanda za Mahakama Kuu 16 kati ya mikoa 26, na hivyo uhitaji utakaobaki ni wa Majengo 10 tu,” alieleza Mhandisi Kitunzi.
Hata hivyo, Mhandisi Kitunzi anasema kuwa taratibu za ujenzi wa Mahakama Kuu katika baadhi ya mikoa iliyobaki zinaendelea, na Mahakama hizo zitajengwa chini ya Fedha za Mradi wa Benki ya Dunia (WB) Mikoa itakayojengewa Mahakama Kuu/Vituo vya Haki ‘Justice centre’ ni pamoja na Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Singida, Mwanza na Arusha.
Aidha; kwa upande wa ujenzi wa Mahakama za Hakimu Mkazi, Mhandisi Kitunzi anabainisha kuwa ujenzi wa Mahakama hizo pia unaendelea katika mikoa ya Geita, Njombe, Lindi, Katavi na Simiyu.
Azma ya Mahakama ya Tanzania ni kusambaza huduma za Mahakama nchi nzima ili hata mwananchi aliyepo katika ngazi ya Kata aweze kupata huduma ya Haki.
Mbali na ujenzi pia kumekuwa na ukarabati wa majengo ya Mahakama ya mara kwa mar azote zikiwa ni jitihada za kuhakikisha kunakuwa na miundombinu ya majengo bora ya kutolea haki.
Hivi karibuni katika Maadhimisho ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria nchini jumla ya Majengo mapya matano (5) ya Mahakama yalizinduliwa rasmi; majengo hayo ni pamoja na Kituo cha Mafunzo na Habari za Mahakama kilichopo Kisutu Dar es Salaam, Mahakama ya Wilaya Bagamoyo, Mahakama ya Wilaya Kigamboni, Mahakama ya Wilaya Mkuranga pamoja na Mahakama ya Mwanzo Kawe.
No comments:
Post a Comment