Tanzania, Rwanda Zang’ara EAC Vita ya Rushwa .
MISIMAMO thabiti ya Rais John Pombe Magufuli katika masuala mbalimbali ya maendeleo ya Taifa imezidi kuleta mafanikio ambapo ripoti mpya katika mapambano dhidi ya rushwa imeonesha Rwanda na Tanzania kuongoza katika ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika mapambano dhidi ya rushwa kwa mwaka 2017.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Tathmini ya Hali ya Rushwa (Corruption Perception Index) iliyotolewa jana Februari 21, 2018 na Taasisi ya Transparency International, juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano Tanzania chini ya Dkt. John Pombe Magufuli katika kupambana na rushwa zimezidi kuzaa matunda katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Taarifa hiyo iliyokusanya takwimu za mwaka mzima wa 2017 zinaonesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zilizopanda kwa kiasi kikubwa katika kupambana na rushwa huku nyingi nyingi zikishuka au kubaki pale pale.
Wakati mwaka 2016 Tanzania ilikuwa ya 116 duniani, katika ripoti hiyo mpya Tanzania imepanda kwa nafasi 13 na kuwa ya 103 huku ikizizidi kwa mbali nchi kadhaa kubwa duniani katika utafiti huo uliohusisha mataifa 180.
Aidha, kwa eneo la Afrika Mashariki, Tanzania imekuwa nchini ya pili baada ya Rwanda iliyoongoza kwa kupunguza rushwa ambapo katika alama za mtazamo wa rushwa Tanzania imepata 36, alama ambazo ni nyingi kuwahi kufikiwa na nchi katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa Tanzania, kufikia nafasi hiyo ya juu, imeonesha kufanikiwa katika kufanyiakazi mianya mingi ya rushwa, kwa mujibu wa vigezo vya rushwa kupungua katika taasisi mbalimbali za Serikali na kwa mujibu pia wa mtazamo wa wafanyabiashara na wawekezaji.
Ripoti hii inakuja ikiwa ni hivi karibuni tu Tanzania chini ya juhudi kubwa za Serikali ya Awamu ya Tano ilitajwa na ripoti ya jarida la The Economist kuongoza katika EAC kwa utawala bora na demokrasia (Democracy Index).
Akizungumzia ripoti hii jijini Dar es Salaam jana, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, alisema ripoti hiyo ni sehemu tu ya kuonesha kuwa vita dhidi ya rushwa na ufisadi nchini inafanikiwa.
“Unaweza kuyapima mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna nyingi katika kupambana na rushwa, ripoti hii kuonesha tumepanda kwa kuzipita nchi 13 katika mwaka mmoja ni moja tu ya ishara kuwa vita yetu hii ya haki ni ya haki kweli na inapaswa kuendelea,” alisema.
Dkt. Abbasi aliongeza: “Kama nchi tutaendelea kutekeleza. Tutaendelea kuhakikisha kile kidogo wanachokichangia wananchi kinatumika kwa maendeleo ya Taifa kama mnavyoona namna tunavyotekeleza miradi mikubwa na ya kihistoria karibu katika kila sekta.”
Hivi karibuni Ripoti nyingine ya Taasisi ya Kiuchumi Duniani (World Economic Forum) iliitaja Tanzania kuwa ya pili Afrika na ya kwanza katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara katika nyanja za uchumi jumuishi.
Mafanikio yote haya yanakuja wakati ambapo Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais aliyeahidi na anayetekeleza mageuzi, Dkt. John Pombe Magufuli, ikiwa inaendelea kwa kasi kusimamia maendeleo ya Taifa.
No comments:
Post a Comment