Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (kushoto) akimkabidhi funguo ya gari, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania, Thobias Andengenye katika hafla iliyofanyika janao kwenye Kituo cha Zimamoto cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania, Thobias Andengenye akiwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela wakiwa katika picha ya pamoja na maafisa wa kikosi hicho na menejimenti ya TAA.
Gari aina ya Toyota Hilux alilokabidhiwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania, Thobias Andengenye na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela litakalotumiwa na Kamanda wa Kikosi cha ZImamoto na Uokoaji wa Viwanja vya Ndege Tanzania, Christom Manyoroga.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani cha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bi. Irene Sikumbili (kushoto) akiagana na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini, Thobias Andengenye jana baada ya kukabidhiwa gari litakalotumiwa na Kamanda wa kikosi cha Zimamoto cha Viwanja vya Ndege Tanzania. Wengine kulia ni Mkuu wa Idara ya Manunuzi na Ugavi Bw. Mtengela Hanga na (katikati) Mkuu wa Idara ya Udhibiti Viwango Bw. Paul Rwegasha.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (kulia) akiagana na makamanda wa kikosi cha zimamoto na Uokoaji baada ya kukabidhi gari jana.
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) jana imekabidhi gari aina Toyota Hilux kwa Idara ya Zimamoto na Uokoaji ya Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), ili kuchocheo ufanisi wa kazi.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Richard Mayongela akikabidhi gari hilo katika hafla fupi iliyofanyika jana katika Kituo cha Zimamoto na Uokoaji cha JNIA, alisema litasaidia usafiri wa haraka kwenye matukio kwa Kamanda wa Zimamoto wa Viwanja vya Ndege Tanzania, Kamishna Msaidizi, Christom Manyoroga, ambaye awali alikuwa na gari kuukuu.
Bw. Mayongela alisema kuwa gari hilo lenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 80, mbali na kusaidia usafiri wa haraka kwenye matukio ya ndani ya kiwanja na nje endapo watatakiwa kutoa msaada, pia litasaidia shughuli mbalimbali za zimamoto na uokoaji.
Alisema Zimamoto ni miongoni mwa taasisi kubwa inayofanya kazi na TAA, hivyo ni jukumu la mamlaka kuhakikisha wanawezeshwa kwa vifaa na vitendea kazi ili waweze kufanya kazi kwa weledi.Pia Bw. Mayongela alisema mbali na msaada ya gari hilo TAA itatoa fedha kiasi Sh milioni 120 kwa ajili ya kuwapatia mafunzo wafanyakazi wa vituo vya Zimamoto vya viwanja vya ndege, ili weaweze kwenda na mabadiliko yanayotokea duniani.
“Mafunzo haya kwa askari wa Zimamoto ni muhimu sana ukizingatia hawa wanatumia mitambo haya magari hakuna wazimamoto wengine wanaoweza kutumia zaidi hawa wa viwanja vya ndege, hivyo wanahitaji kwenda na wakati na kujifunza mambo mapya, kwani wapo waliopata mafunzo kwa muda mrefu na wengine hawajapata mafunzo kabisa,” alisema Bw. Mayongela.Aliongeza …“TAA itaendelea kudumisha ushirikiano baina yao na kwa karibu zaidi na idara Zimamoto na uokoaji,”.
Naye Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania, Thobias Andengenye, aliishukuru TAA kwa msaada wa gari hilo, ambalo litachochea ufanisi mkubwa wa kazi wa askari kwa kuwa Mkuu wao atakuwa na usafiri wa kumfikisha maeneo mbalimbali.
Alisema viwanja vya ndege ndio lango kuu la kuingilia wawekezaji na watalii, ambapo kuimarisha idara hiyo kutasaida kutimiza lengo la Tanzania ya Viwanda na kufikia malengo ya mwaka 2025 kuwa na viwanda vitakavyowekezwa na wawekezaji wazawa na wageni kutoka nje ya nchi.
Kamishna Jenerali Andengenye alisema bila usalama wawekezaji na watalii watashindwa kuingia nchini kwa kuogopa usalama wao na mali zao.
No comments:
Post a Comment