Sunday, February 4, 2018

Rasimu ya Katiba Mchezo wa Ngumi ya kabidhiwa kwa Waziri Mwakyembe

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (kushoto) akizungumza na wadau wa ngumi (hawapo pichani) kuhusu mchakato wa kukamilisha rasimu ya katiba ya kusimamia mchezo wa ngumi nchini maara baada ya kukabidhiwa jana jijini Dar es Salaam,kulia kwake ni Msajili wa Vyama vya Michezo Nchini kutoka Baraza la Michezo la Taifa Bw. Ibrahim Mkwawa.
Katibu Mtendaji Baraza la Michezo la Taifa Bw.Mohamed Kiganja (kulia) akitoa taarifa kuhusu mchakato wa kuundwa kwa rasimu ya katiba ya mchezo wa ngumi kwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (kushoto) kabla ya makabidhiano ya rasimu hiyo jana jijini Dar es Salaam,wapili kulia ni Msajili wa Vyama vya Michezo Nchini kutoka Baraza la Michezo la Taifa Bw Ibrahim Mkwawa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kuunda rasimu ya Katiba ya kusimamia mchezo wa Ngumi nchini Bw.Emmanuel Salehe akikabidhi rasimu ya katiba hiyo kwa Mheshimiwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe () jana jijini Dar es Salaam katikati ni Katibu Mtendaji  Baraza la Michezo la Taifa Bw.Mohamed Kiganja.
Mmoja wa wanakamati waliyoandaa rasimu ya Katiba ya kusimamia mchezo wa ngumi Bw.Ally Champion akitoa maoni yake na kuwasihi wadau wangumi kuacha tofauti zao za vikundi vyao waungane kwa lengo la kuimarisha mchezo wangumi kwa taifa jana katika mkutano wa kukabidhi rasimu hiyo kwa Mheshimiwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (hayupo pichani).
Baadhi ya wajumbe waliyoandaa rasimu ya Katiba ya kusimamia mchezo ngumi wakiwa katika picha ya pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (wanne kulia)mara baada ya kumkabidhi rasimu hiyo jana jijini Dar es Salaam,watatu kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kuunda rasimu hiyo Bw.Emmanuel Salehe na watatu kulia ni Katibu Mtendaji Baraza la Michezo la Taifa Bw.Mohamed Kiganja.
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (kushoto) akimsikiliza bondia wa kike Bi.Feriche Mashauri (kulia) alipokuwa akimweleza changamoto za mchezo wa ngumi nchini jana jijini Dar es Salaam baada ya Waziri kukabidhiwa rasimu ya mchezo wa ngumi .

……………………………………………………………………………………

Na Anitha Jonas – WHUSM-Dar es Salaam

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe ameipongeza Kamati iliyoandaa rasimu ya katiba ya mchezo wa ngumi nchini kwa kumaliza kazi hiyo kwa wakati.

Mheshimiwa Mwakyembe ametoa kauli hiyo alipokuwa akikabidhiwa rasimu ya katiba hiyo jana jijini Dar es Salaam mara baada kukamilika kwa kuandaliwa kwake na kamati maalum iliyokuwa na wajumbe 13 wakuteuliwa ambao walifanya kazi ya kuzunguka kwa wadau wa ngumi na kukusanya maoni.

“Nitateuwa watu wasaba kutoka katika kamati hii iliyounda rasimu watakao uungana na Baraza la Michezo la Taifa kuboresha rasimu hii ili tuweze kuitisha kikao kikubwa cha wadau wote wa mchezo wa ngumi na tuweze kuipitisha rasimu hii,”Dkt.Mwakyembe.

Akiendelea kuzungumza katika makabidhiano hayo Waziri Mwakyembe alieleza kuwa ataendelea kupokea maoni ya wadau hao ndani ya miezi mitatu kwa kuzingatia sheria ili kufanikisha kikao cha kupitisha rasimu hiyo ambacho kitaitishwa kwa mujibu wa sheria ili kufanikisha lengo la kuboresha sekta ya mchezo wa ngumi nchini.

Pamoja na hayo waziri huyo alisisitiza kuwa na mapema wiki ijayo atamuagiza Katibu Mtendaji Baraza la Michezo la Taifa Bw.Mohamed Kiganja kutangaza wajumbe atakao kuwa amewateuwa kuungana na BMT katika kuboresha rasimu hiyo.

Akizungumza katika sherehe za makabidhiano ya rasimu hiyo ya katiba ya kusimamia mchezo wa ngumi nchini Mwenyekiti wa Kamati hiyo Bw.Emmanuel Salehe alieleza kuwa pamoja na kukamilisha rasimu hiyo kamati hiyo iliunda pia kanuni za kusimamia mchezo wa ngumi kwa lengo la kuhakikisha misingi imara inawekwa katika kuboresha sekta ya mchezo huo.

Kwa Upande wa Katibu Mtendaji Baraza la Michezo la Taifa Bw. Mohamed Kiganja alisema kuwa ofisi yake iko tayari kuungana na wajumbe watakaoteuliwa na Mheshimiwa Waziri kukamilisha mchakato wa kuboresha rasimu hiyo kabla ya kupitishwa.

Pamoja na hayo naye bondia wa zamani aliyekwisha kushinda katika mikanda ya kimataifa Bw.Rashid Matumla alitoa maoni yake pamoja na kuipongeza serikali kwa kufanya maamuzi ya kuunda chombo imara kitakacho simamia mchezo wa ngumi kwa kuzingatia sheria tofauti na awali huku akiwasihi wadau wangumi kuacha tofauti zao na kuangalia suala la msingi kuboresha mazingira ya mchezo huo na kuufanya uwe na tija kwa zaidi pamoja na kuondoa mazingira yenye utata katika uendeshaji wa mchezo huo.

No comments: