Monday, February 12, 2018

PWANI YAWATAKA WAFANYABIASHARA , KUSAJILI TIN NUMBER KWA TRA PWANI

Na Mwamvua Mwinyi,Pwani

SERIKALI mkoani Pwani,imewaasa wafanyabiashara, wawekezaji na wenye viwanda ,kuhakikisha wanasajili namba za utambulisho ya mlipa kodi (TIN no) kwa meneja wa mamlaka ya mapato (TRA) mkoani humo, ifikapo machi 30 mwaka huu.

Hatua hiyo itasaidia mkoa huo kunufaika na wafanyabiashara hao ambao wengi wao kwasasa wanalipa kodi katika maeneo ya mikoa waliojisajili .Mkuu wa mkoa huo,mhandisi Evarist Ndikilo alitoa agizo hilo ,mjini Kibaha wakati wa mkutano wa baraza la biashara la mkoa .

Alisema kutokana na wafanyabiashara wengi mkoani hapo kulipia kodi nje ya Mkoa kunasababisha kudidimiza uchumi wa mkoa."Kila mmoja abebe mzigo wake,mchango wetu kama mkoa hauonekani,na hatunufaiki ,unakuta tuna miviwanda mingi lakini wamekata TIN no.Kinondoni, Ilala ,jijini Dar es salaam ,mapato yake yote yanahesabika huko"

"Kwa mujibu wa takwimu za kitaifa mkoa wa Pwani unachangia asilimia 1.6 ya pato la taifa ambalo liko chini, kumbe wafanyabiashara na makampuni hawatulipi kodi kwenye mkoa jambo ambalo sio sawa," alisema Ndikilo.

Ndikilo alisema makampuni na wafanyabiashara hao, wamekuwa hawalipi malipo mbalimbali kwa kudai wanalipia Dar es Salaam.Aidha Ndikilo ,aliwaasa wawekezaji kuwa na lebo kwenye bidhaa zao zinazoonyesha zinazalishwa Mkoani Pwani ili kuutangaza mkoa .Pamoja na hayo ,alizitaka taasisi wezeshi kushirikiana na jumuiya ya wafanyabiashara (TCCIA), ili kuona kama kuna urasimu katika idara mbalimbali ikiwemo maji ,umeme na kuangalia namna ya kuondoa ama kupunguza urasimu uliopo.

Ndikilo alisema ,kila mmoja apambane na rushwa pasipo kuiachia TAKUKURU pekee ,kwani kwa kuiachia TAKUKURU peke yake kamwe rushwa haitoisha.Aliwasisitizia wakuu wa wilaya na wakurugenzi kwenda kuundwa mabaraza ya uwekezaji ndani ya wilaya zao.

Nae mkuu wa wilaya ya Rufiji ,Juma Njwayo alieleza kuna baadhi ya makampuni hasa yale yanayomiliki mahoteli yamekuwa hayalipi kodi kwa madai wanalipa Dar es Salaam.Njwayo alisema hakuna budi kuwasiliana na kamishna wa TRA ili kubadilisha utaratibu wa usajili kwa wahusika walipie kwenye maeneo ya biashara zao.

Awali meneja wa mamlaka ya mapato (TRA) mkoa wa Pwani, Euvensia Lwiwa alieleza wanakabiliwa na changamoto hiyo ambayo inasababisha kukosa mapato.Lwiwa alisema alifanikisha makampuni matano kati ya 36 kulipa kodi na tozo mbalimbali lakini bado wanaendelea na mikakati kuhakikisha wanalipa ndani ya mkoa.
 Baadhi ya wajumbe wakifuatilia mkutano wa baraza la biashara la Mkoa  wa Pwani
 Mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo amekizungumza wakati wa mkutano wa baraza la biashara la mkoa ,mjini Kibaha. (Picha na Mwamvua Mwinyi)

Mwenyekiti wa wafanyabiashara mkoani Pwani, Abdallah Ndauka ,akionekana pichani akizungumzia masuala mbalimbali ya kibiashara katika mkutano wa baraza la biashara la Mkoa huo.(picha na Mwamvua Mwinyi)

No comments: