Saturday, February 24, 2018

OSHA YASISITIZA KADA YA USALAMA KAZINI KUTAMBULIKA RASMI

Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) unakusudia kuishawishi serikali na waajiri katika sekta binafsi hapa nchini kuitambua kada ya Usalama na Afya mahali pa kazi na kuiweka katika mfumo rasmi wa ajira.

Mpango huo uliwekwa wazi na Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA Bi.Khadija Mwenda, alipowahutubia wahitimu wa Kozi ya Taifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi katika hafla ya kufunga kozi hiyo Februari 23,2018 jijini Dar es salaam. Kozi hiyo pamoja na nyingine zinazohusu Usalama na Afya kazini hutolewa na Wakala huo wa serikali.

Mtendaji Mkuu huyo alisema kwasasa kada ya maofisa Usalama Mahali pa Kazi (Safety Officers) bado haitambuliki katika mfumo rasmi wa ajira hapa nchini jambo linalopunguza ufanisi katika kusimamia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.

”Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003, inawataka waajiri kuunda Kamati za Usalama na Afya katika sehemu zao za kazi ambazo wajumbe wake ni wawakilishi wa wafanyakazi ambao kimsingi wana majukumu yao mengine tofauti na kusimamia masuala ya usalama na afya mahali pa kazi. Hivyo jukumu la kusimamia usalama na afya wa wafanyakazi wenzao katika sehemu za kazi husika linakuwa ni la ziada,” alisema Bi. Mwenda.

Aliongeza: “Hivyo tunaamini kwamba endapo kada hii itaingizwa katika mfumo rasmi wa ajira katika sekta zote, waajiri wote watalazimika kuajiri wataalam wa masuala ya usalama na afya mahali pa kazi ambao jukumu lao kuu litakuwa ni kusimamia afya na usalama wa wafanyakazi wote wanapokuwa kazini.”

Aidha, Kiongozi huyo mkuu wa taasisi aliwaasa wahitimu wa mafunzo hayo kwenda kuwa mabalozi wazuri wa OSHA kwa kutumia ipasavyo elimu waliyoipata katika kuimarisha hali ya usalama na afya kwenye maeneo ya kazi wanakotoka na hivyo kuongeza tija na kukuza pato la Taifa.“Tunatarajia kwamba mtatuwakilisha vema katika sehemu mbali mbali za kazi mnakokwenda kufanya kazi kwa kuyatekeleza yale yote mliyojifunza katika mafunzo haya,” alisema kiongozi huyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mafunzo, Utafiti na Takwimu wa OSHA, Bw. Joshua Matiko, aliwapongeza wahitimu hao kwakujituma na kuwa na nidhamu katika kipindi chote walipokuwa wakipatiwa mafunzo hayo.“Ninawaasa msiridhike na mafunzo haya mliyoyapata kwasasa bali mnapaswa kujiendeleza zaidi kwa kusoma kozi nyingine zitakazowawezesha kutekeleza majukumu yenu kwa ufanisi zaidi. Kwa mfano, kuna mafunzo mengine ya namna ya kufanya utambuzi wa vihatarishi katika sehemu za kazi yatatolewa hivi karibuni huko jijini Mwanza hivyo mnakaribishwa kushiriki,” alieleza Matiko.

OSHA ni msimamzi mkuu wa Usalama na Afya za wafanyakazi wanapokuwa kazini ambapo husajili sehemu za kazi, kufanya kaguzi za usalama na afya katika sehemu husika na kutoa mafunzo ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi.

Habari imeandikwa na Eleuter Mbilinyi
Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, akiwahutubia wahitimu wa Kozi ya Taifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi wakati wa hafla ya kufunga mafunzo hayo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Mafunzo, Utafiti na Takwimu wa OSHA, Bw. Joshua Matiko, akiongea na wahitimu wa Kozi ya Taifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi wakati wa hafla ya kufunga mafunzo hayo jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, akiwahutubia wahitimu wa Kozi ya Taifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi wakati wa hafla ya kufunga mafunzo hayo jijini Dar es Salaam.
Wahitimu wa Kozi ya Taifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi wakifuatilia hotuba ya Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, wakati wa hafla ya kufunga kozi hiyo iliyofanyika katika ofisi za Wakala jijini Dar es Salaam.

No comments: