Monday, February 5, 2018

Kishapu yafikia lengo la zaidi ya asilimia 75 zoezi la upigaji chapa ng’ombe 225,131


Mkuu wa Idara ya Mifugo Uvuvi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Dk. Alphonce Bagambabyaki akishiriki katika zoezi la upigaji chapa ng’ombe.
Wananchi wakishiriki katika zoezi la upigaji chapa ng’ombe katiia kijiji cha Wishiteleja kata ya Mondo.
Moja wa ng’ombe akiwa tayari amepigwa chapa katika sehemu ya mguu.


Na Robert Hokororo, Ofisi ya Mkurugenzi 

Halmashauri ya wilaya ya Kishapu imeweza kupiga chapa jumla ya ng’ombe 225,131 katika zoezi la utambuzi na usajili wa mifugo linalofanyika katika kata zote zenye wafugaji wilayani humo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Stephen Magoiga amesema kuwa zoezi hilo ni endelevu na limeweza kufanikiwa kwa kiwango kikubwa pamoja na kuwepo kwa changamoto kadhaa.

Alisema zoezi hilo ni agizo kutoka serikalini na kinachofanyika ni kulitekeleza kwa kiwango kinachotakiwa na kuweza kuwafikia wafugaji katika maeneo mbalimbali katika kata za wilaya hiyo.

“Zoezi la upigaji chapa ng’ombe tulilipokea na tumeweza kulitekeleza ingawa zipo changamoto mbalimbali zikiwemo baadhi ya maeneo kutokuwepo kwa wafugaji tumefanikiwa kuifikia mifugo hiyo,” alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Mifugo Uvuvi katika Halmashauri hiyo, Dk. Alphonce Bagambabyaki alisema Wilaya imeweza kufikia lengo hilo kwa zaidi ya asilimia 75 ya lengo ambalo ni ng’ombe laki tatu.

Alisema vijiji lengwa vyote 125 vimeweza kufikiwa na ingawa zipo baadhi ya changamoto kama imani potofu kwa baadhi wafugaji kuwa huenda wakachukuliwa mifugo yao pindi wanapoifikisha vituo vya zoezi la upigaji chapa.

Zoezi hilo lilianza rasmi Oktoba 20 mwaka jana ambapo lilizinduliwa na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mh. Nyabaganga Taraba linataka mifugo yote nchini kutambuliwa kwa kutumia chapa chini ya sheria ya utambuzi namba 12 ya mwaka 2010.

Aidha, zoezi hilo limekuwa likitekelezwa na wataalamu wa mifugo kutoka wilayani makao makuu wakishirikiana na wataalamu wa kata na vijiji mbalimbali ili kuhakikisha limekwenda kwa ufanisi.

Wakati akizindua zoezi hilo Mh. Taraba alibainisha kuwa zoezi la utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa ng’ombe kwa kutumia chapa litapunguza changamoto zinazowakabili wafugaji.

Alibainisha kuwa Kishapu ni miongoni mwa wilaya ambazo baadhi ya wafugaji wake wanakabiliwa na matatizo yakiwemo wizi wa mifugo katika unaoweza kutokea katika maeneo mbalimbali nchini.

Pia linasaidia kupunguza migogoro migogoro baina ya wakulima na wafugaji wanaokuwa wanahama hama bila kufuata utaratibu maalumu kwa lengo la kutafuta malisho kwa ajili ya mifugo yao.

No comments: