Friday, February 9, 2018

KISHAPU KUWAHAMISHIA WALIMU WA SEKONDARI KUFUNDISHA SHULE ZA MSINGI KUONGEZA UFANISI

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga akizungumza katika kikao cha kijadili namna ya kuboresha sekta ya elimu kwa ujumla. Wengine pichani kushoto ni Kaimu Afisa Elimu Sekondari, Paul Kasanda na mwenyekiti wa kikao hicho ambaye pia ni Diwani wa kata ya Mwaweja, Makanasa Kishiwa.2
Washiriki mbalimbali wakiwemo maafisa elimu kata, walimu wakuu shule za msingi na sekondari na baadhi ya wanafunzi wakiendelea kufuatilia kikao hicho.
3
Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye pia ni Diwani wa kata ya Mwaweja, Makanasa Kishiwa akizungumza. Kushoto ni Afisa Elimu Sekondari, Paul Kasanda
4
Afisa Elimu Msingi, Sostenes Mbwilo akisisitiza jambo kwa washiriki wa kikao hicho (hawapo pichani).
5
Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Paul Sheka akichangia katika kikao cha wadau wa elimu.
6
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga akisisitiza  jambo wakati wa kikao cha kujadili namna ya kuboresha sekta ya elimu wilayani humo.
7
Washiriki wakiendelea kufuatilia kikao hicho.
……………..
Na Robert Hokororo, Ofisi ya Mkurugenzi
Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu ipo katika mchakato wa kuwahamishia walimu wa ziada wa masomo ya sanaa wa shule za sekondari kwenda kufundisha shule za msingi zenye upungufu.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Stephen Magoiga wakati akizungumza katika kikao kikao kilichowakutanisha wadau wa elimu wilayani Kishapu kujadili masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya elimu ya msingi na sekondari ili kuboresha viwango vya ufaulu.
Alisema mchakato huo unafanyika kutokana na maelekezo kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kuboresha ikama ya walimu baada ya kubaini upungufu au ziada kwa kila shule.
Kwa mujibu wa takwimu kutokana na uhakiki kuna ziada ya walimu wa masomo ya sanaa kwenye shule za sekondari na upungufu wa walimu wa sayansi na hisabati katika shule za msingi.
Kutokana na changamoto hiyo kwa kuanzia Kishapu itaanza kuwahamisha walimu wa ziada sekondari na kwenda kufundisha shule za msingi zilizo karibu na kuwa uhamisho huo hautaathiri mishahara na stahiki nyingine za walimu.
Akifafanua zaidi Magoiga alisema kuwa hilo ni zoezi la kawaida na kuwa walimu wengi katika shule za sekondari wana vipindi vichache kulinganisha na wale wa msingi na hivyo litasaidia kuleta ufanisi bila kuathiri utendaji.
“Mwalimu wa sekondari nikikuhamishia shule ya msingi kufundisha usijisikie vibaya na kujiona kama nimekushusha bali nimekuongezea majukumu mengine kwa mamlaka niliyo nayo, na ntapita nihakikishe unakuwepo kituo nilichokupangia kufundisha,” alisisitiza.
Aidha alihimiza ushirikiano baina ya wadau wote wa elimu ili kuwepo na maandalizi mazuri kwa wanafunzi wafanye vizuri katika masomo yao huku akisema wazazi wanapaswa kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto wao.
Wakichangia kwa nyakati tofauti baadhi ya madiwani akiwemo Mh. Lucas Nkende wa kata ya Mwamashele alisema mahudhurio hafifu ya wanafunzi ndi changamoto zinazoporomosha kiwango cha ufaulu.
Alishauri pawepo na mfumo mzuri wa kusimamia wanafunzi huku akisisitiza mamlaka iangalie walimu wenye uwezo wa kufundisha wanafunzi wa madarasa ya chini ambapo ndio msingi wa elimu.
Kikao hicho kimehusisha waheshimiwa madiwani, Mkurugenzi Mtendaji, maofisa elimu msingi na sekondari kutoka makao makuu na kata, wakuu wa shule za msingi na sekondari, wanafunzi na wadau kutoka Programu ya Kuinua Ubora wa Elimu (Equip).  

No comments: