Monday, February 26, 2018

KATIBU CHADEMA KATA YA MAILMOJA ATIMKIA CCM

Na Mwamvua Mwinyi,Pwani

WIMBI la baadhi ya viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) limezidi kuwakumba hapa nchini baada ya katibu wa CHADEMA kata ya MailMoja Mjini Kibaha Mohamed Hashim kuhamia CCM.

Pamoja na hayo wanachama wengine wa CHADEMA na ACT Wazalendo wapatao tisa nao walirejea CCM na kukabidhi kadi zao kwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Pwani Ramadhan Maneno.

Hayo yalijiri Kongowe wilayani Kibaha wakati Maneno alipokuwa akizungumza na viongozi na wanachama wa wilayani humo.Maneno alisema, kwa sasa wapinzani wameshatambua vyama hivyo kuwa hakuna jipya hivyo wameamua kumuunga mkono Rais Dk John Magufuli ambaye anatatua kero na changamoto zilizokuwa zinawasumbua wananchi.

“Hichi ndicho kielelezo cha kumkubali kiongozi wetu wao wenyewe wameona kinachofanyika na kasi na mabadiliko ya kimaendeleo iliyopo,” alisema Maneno.Alisema kuwa wanaCCM wanapaswa kukiimarisha chama kwa kuhakikisha wanalipa ada zao kwa wakati kwani ili mwanachama awe hai lazima alipe ada zake .

“Tunawanachama 38,000 kwenye Mji wa Kibaha lakini waliolipa ada ni wanachama 8,000 pekee ,,:;si sawa lazima wanachama watakeleze jukumu lao hilo ili kujenga chama,” alisisitiza Maneno.Alielezea kwa sasa viongozi waendelee kuhamasisha wananchi kujiunga CCM kwani mtaji wa chama ni kuongeza wanachama wapya.

Maneno alibainisha mkoa umejipanga kushika dola kwenye uchaguzi wa serikali za Vijiji na Mitaa mwaka 2019 ikiwa kama sehemu ya kujipima kabla ya mwaka 2020 kwenye uchaguzi mkuu.Aidha aliwataka viongozi kuanzisha madawati ya kusikiliza malalamiko ya wanachama na wananchi ili wapate mahali pa kutoa madukuduku yao na kueleza changamoto mbalimbali zikiwemo zile za kimaendeleo.

Maneno alitoa rai kwa viongozi wake kwenye wilaya za mkoa huo kuisimamia serikali ili iweze kutekeleza ilani ya chama kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi.Kwa mujibu wake, wasimamizi wakuu wa ilani ni viongozi ambao wanapaswa kushirikiana na watendaji wa serikali katika kukabili na kutatua changamoto za wananchi.

“Kwa sasa ilani inayotekelezwa ni ya CCM hivyo sisi ndiyo wasimamizi wakuu tunapaswa kuisimamia na kuhakikisha ahadi zote tulizo ahidi wananchi zinatekelezwa ili kuwaletea maendeleo wananchi,” alisema Maneno.Maneno alisema kuna miradi mingi ambayo endapo haitasimamiwa au kufuatiliwa na viongozi wa chama tawala inaweza isikamilike kwa wakati endapo hakutakuwa na ushirikiano na viongozi wa chama.

Nae Hashim alisema ameamua kurudi CCM baada ya kuona kuwa kwenye chama hicho hakuna demokrasia ya kweli na kujaa malumbano ambayo hayana tija kwa wananchi.Kwa upande wake ,mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini Maulid Bundala alieleza ,viongozi wa ngazi za juu tayari wameshafanya kazi kubwa ya kukijenga chama pamoja na serikali na wao wajibu wao ni kuendeleza maboresho.

Bundala alisema mbali ya kuhimiza maendeleo kwa kushirikiana na chama wanaendelea kushirikiana vema na Halmasahuri ambao ndiyo watekelezaji wa miradi ya maendeleo.Akiwa wilayani hapo ,Maneno alitembelea soko la vyakula na bidhaa mbalimbali la Maili Moja maarufu kama Loliondo pamoja na ujenzi wa stendi mpya ya mabasi ambayo iko kwenye hatua za mwisho.
 Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Pwani, Ramadhani Maneno akizungumza jambo na baadhi ya  viongozi ,wa CCM Mjini Kibaha na halmashauri ya mjini hapo wakati wa ziara yake mjini humo .
 Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Pwani, Ramadhani Maneno akisalimiana na  baadhi ya  viongozi ,wa CCM Kata ya Kongowe na Mjini Kibaha kabla ya mkutano nao ,kuzungumzia masuala mbalimbali ya Chama wakati wa ziara yake mjini humo .(picha na Mwamvua Mwinyi)
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Pwani, Ramadhani Maneno akipokea kadi kutoka kwa katibu wa CHADEMA kata ya MailMoja Mohamed Hashim aliehamia CCM wakati mwenyekiti huyo alipokuwa akizungumza na baadhi ya wanachama na viongozi ,katika mkutano huo wanachama wengine Tisa kutoka upinzani walijiunga na Chama hicho.(picha na Mwamvua Mwinyi)

No comments: