Na Said Mwishehe, Globu ya Jamii.
KAMANDA wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Muslimu amesema hakuna sheria inayoruhusu askari polisi kupiga wanaotumia vyombo vya usafiri barabarani wakiwamo waendesha bodaboda huku akielezea kuwa atafuatilia ili kubaini iwapo kuna askari wenye tabia ya kupiga waendesha bodaboda.
Muslimu ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati akielezea mafanikio yaliyopatikana kwenye kupunguza ajali za barabarani ambapo Baraza la Taifa la Usalama Barabarani limetoa tathmini ya mpango mkakati wa awamu ya kwanza na awamu ya pili unaonesha ajali za barabarani zimepungua kwa kiasi kikubwa nchini.
Hivyo ameelezea pia umuhimu wa watumiaji wa barabara wakiwamo waendesha pikipiki maarufu bodaboda kuzingatia sheria za usalama na kuelezea kuwa wanapaswa kufuata sheria bila shuruti. Hata hivyo waandishi wa habari waliokuwa kwenye mkutano huo walitaka kufahamu ni kwanini baadhi ya askari polisi hasa maeneo ya makutano ya Tazara, Ubungo, Mwenye na Daraja la Salenda wamekuwa wakiwapiga waendesha bodaboda na kusababisha hali ya sintofahamu.
“Sheria hairuhusu mtu yoyote kumpiga mwingine na kama kuna makosa yamefanyika hatua za kisheria zinastahili kuchukuliwa lakini si kupiga mtu.Hii ya kwamba askari wanawapiga bodaboda tutafuatilia lakini nachofahamu hakuna askari anayeweza kumpiga mtu wa bodaboda.
“Pia ifahamike tunazo sheria za usalama barabarani ambazo tunazisimamia na wakati huohuo zipo sheria ndogondogo za Jiji ambazo nazo kuna watu wanaozisimamia na kuzitekeleza.Suala la bodaboda kukamatwa hilo lipo chini ya Jiji na Tambaza ndio wanaohusika na waendesha bodaboda,”amesema Kamanda Muslimu.
Amefafanua licha ya kwamba hakuna askari anayeweza kupiga waendesha bodaboda barabarani ameahidi kufuatilia kwa kwenda maeneo yanayolalamikiwa kupata ukweli wake na ikibainika atachukua hatua. Ameongeza wao wanalojukumu la kusimamia sheria za usalama barabarani na pia wanalo jukumu la kukabiliana na wahalifu.
No comments:
Post a Comment