Monday, February 5, 2018

CCM PWANI YAPOKEA WAPINZANI 31,WANACHAMA WAPYA 331 RUFIJI NA MKURANGA


Na Mwamvua Mwinyi,Pwani

VIGOGO 27 kutoka chama cha wananchi (CUF) na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)waliotikisa uchaguzi mkuu 2015,maeneo mbalimbali wilayani Rufiji Mkoani Pwani ,wamevihama vyama vyao na kukimbilia CCM.

Aidha wanachama wapya 120 wamejiunga na CCM wilayani Rufiji huku wengine 211 wamejiunga na chama hicho wilayani Mkuranga.Hayo yalijiri katika msafara wa Chama Cha Mapinduzi mkoani Pwani ,kuadhimisha miaka 41 ya CCM katika wilaya hizo ambapo pia walishiriki katika shughuli za kimaendeleo.

Akiongea kwenye maadhimisho hayo ,Utete ,mwenyekiti wa CCM wilaya ya Rufiji ,Kaswakala Mbonde alisema wapambe na baadhi ya viongozi hao wa upinzani wamekikubali chama tawala kutokana na mabadiliko ya maendeleo  na uchumi yanayofanywa na serikali yake .

Alisema serikali ya awamu ya tano imefanya mambo mengi makubwa katika sekta ya miundombinu ,afya,elimu,uwekezaji hivyo wapinzani hawana la kukosoa.Pamoja na hayo ,Mbonde alieleza wapo wanachama wengine wapya 255 waliojiunga na jumuiya ya wanawake (UWT) na 25 wamejiunga jumuiya ya wazazi Rufiji .

Mwenyekiti Wa kitongoji cha Nyangwai kata ya Chemchem aliyekuwa (CUF) Jafar Mpunjo alisema ,wapinzani kazi yao kukosoa na kubeza lakini kwasasa  wanakosa la kukosoa .Mwingine aliyehamia CCM Ashura Sultan alisema ,upinzani ukifika 2019-2020 utakuwa umekufa .

Akipokea wanachama hao ,mwenyekiti wa CCM mkoa wa Pwani Ramadhani Maneno alisema, CCM ni chama chenye sera makini na kinachotatua kero za wananchi .Alielezea walipokea wapinzani wengine wanne Mkuranga,na kudai kwamba wote hawajafanya makosa kujiunga na katu hawapaswi kujutia.

Katika hatua nyingine,Maneno alisema chama hicho mkoa kimetoa misaada mbalimbali katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Malaika na kutembelea na kutoa msaada kwa akinamama waliojifungua katika wodi ya uzazi hospitali ya wilayani Mkuranga.

"Tumechangia damu itakayowezesha kuwasaidia wagonjwa wenye mahitaji hayo na kukabiliana na tatizo la upungufu wa damu " alisema Maneno.Alieleza ,wameamua kutoka kutembelea mambo yanayogusa jamii ili kujua changamoto zinazowakabili wananchi ,wayachukue na kwenda kuzifikisha idara na wizara husika ziweze kupatiwa ufumbuzi.

Nae mjumbe wa halmashauri kuu ya Taifa ya CCM (MNEC) Mkoani Pwani, Hajji Jumaa alisema wametembelea kituo cha kulelea watoto kutokana na sera ya CCM ya elimu bure ambapo kituo hicho kinatoa msaada wa kielimu kwa watoto hao .Hajji alisema wameshiriki kusaidia pale walipoweza ili kuunga mkono juhudi za walioanzisha kituo hicho .

Kwa upande wake ,Mganga mfawidhi wa hospital hiyo ,dk.Shaban Yanda alisema wodi ya uzazi katika hospital ya wilaya ya Mkuranga, ni ndogo haikidhi mahitaji.Alisema jengo hilo linauwezo wa kuchukua akinamama wanaojifungua 60-70 kwa mwezi lakini kwasasa inahemewa kwani inahudumia akinamama hao 350-400 kwa mwezi .

Walipotembelea kituo cha kulelea watoto yatima cha Malaika ,meneja wa kituo hicho James Kalinga ,alisema wanachangamoto ya uhaba wa maji na upungufu wa raslimali fedha ili kuendesha kituo kwa ufanisi .
 ALIYEKUWA mwenyekiti  wa  serikali ya kitongoji cha Nyangwai Kata ya Chechem wilayani Rufiji ,mkoani Pwani mwenye  miwani nyeusi ,ameiacha nafasi hiyo na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mkutano wa  maadhimisho ya miaka  41 ya CCM huko Utete ,ambapo msafara wa  CCM Pwani ,ulipokea wapinzani 27 na wanachama wapya 120 katika maadhimisho hayo.(Picha na Mwamvua Mwinyi)
 WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Utete wilayani Rufiji wakisheherekea baada ya kupokelewa wapinzani 27 waliotikisa uchaguzi mkuu 2015 wilayani hapo,katika mkutano wa  maadhimisho ya miaka  41 ya CCM ,ambapo msafara wa  CCM Pwani ,ulipokea pia wanachama wapya 120 katika maadhimisho hayo.
 MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Pwani Ramadhani Maneno akikabidhi kadi kwa  wanachama wapya katika mkutano wa  maadhimisho ya miaka  41 ya CCM huko Utete ,pia alipokea wapinzani 27 na wanachama wapya 120 katika maadhimisho hayo
Wakila kiapo.

No comments: