Na. Jumbe Ismailly, Hanang
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Hanang,Mkoani Manyara,Bryceson Kibassa amepiga mafuruku walimu wa shule za msingi kuwatoza wazazi na walezi wa watoto michango ya aina yeyote ile na kuwahakikishia kwamba hakuna mtoto wa wilaya hiyo atakayetakiwa kukosa elimu kwa kisingizio cha kutolipa michango.
Mkurugenzi huyo alitoa tahadhari hiyo kwenye mkutano maalumu wa Baraza la madiwani lililokutana kupitisha mapendekezo ya makisio ya mpango na bajeti ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
Akifafanua kuhusu mpango wa elimu ya msingi bila malipo Kibassa alisisitiza kwamba kusiwepo na mtoto yeyote Yule wa Hanang ambaye atashindwa kwenda kusoma shule kwa kisingizio wa mchango wa aina yeyyote ile.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo michango inayoruhusiwa ni ile tu ya kijamii wanayokubaliana kwa ajili ya kuboresha miundombinu bila kugusa ile michango ambayo kwenye waraka inatajwa kwamba msichangishe,isiwe kikwazo cha kuzuia mtoto yeyote kwenda shuleni.
“Tunataka watoto wote wa Hanang kwa agizo na Mheshimiwa Rais na agizo la serikali ya awamu ya tano watoto wote wawepo shuleni na kusijekuwa na mchango wa aina yeyote unaozuia mtoto wa Hanang kwenda shuleni.”alifafanua Mkurugenzi huyo.
Hata hivyo Kibassa alisisitiza kwamba agizo hilo lisije likatafsiriwa kwamba michango ya miundombinu ambayo inapitishwa katika vikao halali ya kijamii imezuiliwa,na badala yake kinachozuiwa ni ile michango ambayo imefafanuliwa vizuri kwenye waraka na endapo hawatakuwa wameuelewa waraka huo wasisite kuomba ufafanuzi.
“Naomba tushirikiane sana kwa hilo ili tusipotoke agizo la Mheshimiwa Rais kama ambavyo baadhi ya watu wanataka kupotosha kwa makusudi na kwamba serikali wilayani hapa haitawavumilia wazazi na walezi watakaokwamisha watoto wao kuanza shule kwa kisingizio cha michango ya shule”aliweka bayana Kibassa.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo,Charles Yona licha ya kuahidi kwa niaba ya madiwani kutoa ushirikiano kwa watendaji wa Halmashauri hiyo,lakini alionyesha kutoridhishwa na hali ya mapato yaliyopatikana mpaka katika kipindi cha robo ya pili ya kwamba kuwa siyo nzuri huku kukiwa kuna changamoto lukuki katika kila kata.
Akisoma mapendekezo ya makisio na bajeti ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 ya jumla aya shilingi bilioni 38,435,735,692,Ofisa Mipango wa Halmashauri hiyo,Pantaleo Mkangara alisema kati ya kiasi hicho cha fedha mapato ya ndani yasiyo na masharti ni 2,493,330,000/= na mapato yenye masharti ambayo ni ruzuku ya matumizi mengineyo ikiwemo fidia ya vyanzo vilivyofutwa ni 470,172,000/=.
Akifunga mkutano huo maalumu wa baraza,Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo,Gorege Bajuta aliwakumbusha watendaji wa Halmashauri hiyo juu ya umuhimu wa kupunguza hoja za ukaguzi na kuonya kuwa hawategemei kuona Halmashauri hiyo ikiendelea kupata hati chafu au hati yenye mashaka,labda tu kuwepo hoja za nyuma zilizokataliwa kupitishwa.
“Lakini hoja zote zinazowezekana kufuta zifutwe tujitahidi sana kuweka nyaraka zetu vizuri pale ambapo wakaguzi wanakuja wanataka kuona nyaraka muhimu kuhusu matumizi ya fedha na miradi zionyeshwe wazi kwa wakaguzi na kwa wakati unaotakika.”alisisitiza Mwenyekiti Bajuta.
No comments:
Post a Comment