WANACHAMA 139 wa Chadema wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro, wamejiunga na CCM na kupokelewa na Mwenyekiti wa UVCCM wa Mkoa wa Manyara Mosses Komba.
Akizungumza wakati wa kuwapokea na kuwakabidhi kadi za CCM wanachama hao wapya, Komba alisema wamefanya uamuzi sahihi kwa wakati sahihi. Komba alisema hawatajuta kujiunga na CCM kwani hivi sasa chama hicho kinachoongozwa na Mwenyekiti wake Rais John Magufuli kinawatumikia wananchi kwa kutatua kero na kuufanikisha maendeleo.
Alisema wanakaribishwa CCM kwa moyo mmoja hivyo washirikiane na wanachama wengine ili kuhakikisha wanalirudisha jimbo hilo na kata sita zinazotawaliwa na Chadema. "Kati ya makosa tuliyofanya kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ni kuachia jimbo la Simanjiro liende Chadema na kata za Mirerani, Naberera, Loiborsiret, Ruvu Remit, Loiborsoit na Endiamtu zichukuliwe na wapinzani," alisema Komba.
Alisema ushabiki wa kufuata mkumbo ndiyo uliowagharimu wananchi wa wilaya hiyo na kata hizo, hadi kusababisha wakapatikana madiwani na mbunge wa kutoka upinzani badala ya CCM."Nakuagiza Mwenyekiti wa UVCCM wa wilaya ya Simanjiro, Thomas Mollel na wenyeviti UVCCM wa kata husika ambazo madiwani wao ni wapinzani, mkishindwa tena 2020 mjiuzulu," alisema Komba.
Mwenyekiti wa UVCCM wa wilaya ya Simanjiro Thomas Mollel alisema kwa kushirikiana na vijana wenzake wa Simanjiro, watahakikisha wanatekeleza agizo hilo la kurejesha jimbo na kata sita zinazoshikiliwa na wapinzani. "Hata hivyo, wananchi wengi wa Simanjiro wana imani kubwa na Rais John Magufuli kupitia CCM mpya, tunatarajia uchaguzi ujao wa mwaka 2020 tutarudisha jimbo na kata hizo sita," alisema Mollel.
Alisema vijana ndiyo nguzo kubwa ya ushindi kwenye chama hicho na wamepata mwamko wa kushiriki kuwajulisha wananchi kuwa CCM ndiyo chama cha kukimbilia. Mjumbe wa baraza la utekelezaji UVCCM mkoa wa Manyara, Elizah Ladis alisema tangu waanze ziara ya kutembelea wilaya za mkoa huo mwezi Desemba mwaka jana, hiyo ndiyo idadi kubwa ya wapinzani 139 kujiunga na CCM.
"Simanjiro wametupokea kwa wapinzani 139 kujiunga na CCM wilaya za Hanang na Mbulu, wapo waliojiunga ila siyo wengi kama hawa, tunaelekea Kiteto na Babati sasa tunatarajia kupata wapinzani wengine," alisema Ladis.
No comments:
Post a Comment