Wafanyabiashara wakubwa wa mbolea Mkoani Rukwa pamoja na wakulima wameridhishwa na upatikanaji wa mbolea na kusifu juhudi za serikali baada ya kupaza sauti zao na kusikika na Rais Dk. John Pombe Magufuli na jambo hilo kufanyiwa kazi ndani ya muda mfupi.
Wafanyabiashara hao wamesema kuwa wakulima hivi sasa hawapangi tena foleni kusubiri mbolea iliyokuwa ikipatikana kwa taabu na kwa kunyang’anyiana na kuwa foleni hizo zimekwisha na wakulima hawana haja ya kutoka Kijiji kuja mjini kufuata mbolea kwani mbolea hizo zinawafuata huko waliko hasa baada ya marekebisho ya bei elekezi iliyotolewa na Uongozi wa mkoa wa Rukwa chini ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo.
Mmoja wa Wafanyabiashara hao wakubwa Mohamed Rashid Mdangwa wa Kampuni ya ETG amesema “Sasa wakulima wameanza kupata mbolea kwa wingi, mwanzo walikuwa wanapanga foleni hapa lakini kuanzia ile Jumatatu agizo la Rais kuwa mbolea iende Mkoa wa Rukwa, sasa hivi population (wingi) ya watu imepungua sana, sasa hivi mahitaji ya mbolea sio makubwa sana kama miezi miwili iliyopita,na mbolea ipo nyingi njiani inakuja, na bei elekezi aliyoitoa Mkuu wa Mkoa imesaidia mbolea kufika vijijini kupitia wakala wadogo wa mbolea.”
Yamewsemwa hayo baada ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akiongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kupitia maghala makubwa ya mbolea yaliyopo Sumbawanga Mjini pamoja na baadhi ya wasambazaji wadogo ili kujionea upatikanaji wa mbolea hizo tangu kutolewa kwa agizo la Rais Dk. John Pombe Magufuli la kusambaza mbolea hizo katika Mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa chakula nchini tarehe 8.1.2018.
Mh. Wangabo aliwasihi wasambazaji wadogo wa mbolea kuendelea kujitokeza na kununua mbolea hiyo ambayo bei iliyopo sasa imezingatia maoni yao na haiumizi, hivyo kufanya hima kuhakikisha kuwa mkulima hakosi mbolea ili kuweza kubaki katika lengo la kuzalisha chakula kwa wingi na kuleta ushindani na mikoa mingine inayozalisha chakula.
“Mimi nitoe wito tu kwa wale Agrodealers (wasambazaji wadogo wa mbolea) wafike kuendelea kununua mbolea, hata bei tumekwishazifikiria tena upya, kila Halmashauri katika Wilaya wamekwisha kaa na kutoa mapendekezo yao halisi ya kiusafirishaji, kwahiyo wafike wanunue mbolea na kutakuwa na faida, bei imezingatia hadi miundombinu iliyoharibika hakutakuwa na usumbufu,” Mh. Wangabo alifafanua.
Mh. Wangabo alitembelea maghala matatu ya wafanyabiashara wakubwa waliopo mjini sumbawanga, TFC pamoja na maduka ya wasambazaji wadogo matatu na kuongea na baadhi ya wakulima ili kujithibitishia upatikanaji wa mbolea hiyo kwa maeneo ya mjini na inayopelekwa vijijini.
Kwa msimu wa 2016/2017 Mkoa wa Rukwa ulilima Hekta zipatazo 556,975.9 na kuvuna tani 1,109,055.6 za mazao ya chakula kati ya hizo mahindi yalikuwa tani 710,602. Kwa msimu huu wa Kilimo wa 2017/18 Mkoa umelenga kulima jumla ya eneo la Hekta 554,310.6 na kuvuna tani 1,669,746.2 za mazao ya chakula.
Mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya ulinzi na Usalama ya Mkoa, Kamanda wa Zimamoto Mkoani Rukwa akikagua mbolea katika ghala la Kampuni ya Mbolea ya Taifa (TFC) lililopo Sumbawanga Mjini.
Mmoja wa Wasambazaji wakubwa wa mbolea Mkoa wa Rukwa Mohamed Mdanga (Kulia) akitoa maelezo ya upatikanaji wa mbolea Mkoani humo mbele ya Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo(kushoto) alipokwenda kumtembelea kwenye ghala lake na kukuta mbolea zai ya tani 300.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa mbele wa kwanza kushoto)alipokuwa akipita mtaa kwa mtaa katika mji wa Sumbawanga kujionea biashara ya mbolea inavyokwenda katika maduka ya mbolea (hayapo pichani) huku akiwa ameambatana na Meya wa manispaa ya Sumbawanga Mh. Justin Malisawa (koti la Draft).
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa pili kutoka kulia) akiwa amesimama mbele ya duka la mbolea kuulizia upatikanaji wa bidhaa hiyo katikati ya mji wa sumbawanga, Mkoani Rukwa.
Timu ya wataalamu wa Kilimo, Kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa na Viongozi wa Manispaa ya Sumbawanga, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kupita duka hadi duka kujionea upatikanaji wa mbolea katika mkoa wa Rukwa.
No comments:
Post a Comment