Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa mwaka wa 2017 imeona jumla ya
wagonjwa 64,093 kati ya hawa wagonjwa wa nje ni 60,796 na waliolazwa
3297. Wagonjwa waliolazwa 3010 waliruhusiwa baada ya hali zao kuwa nzuri
na wagonjwa 287 walipoteza maisha hii ikiwa ni sawa na asilimia 8.7.
Wagonjwa
225 walifanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua ambapo wagonjwa 200
waliruhusiwa na wagonjwa 25 walifariki Dunia hii ikiwa ni sawa na
asilimia 11 (wastani wa kimataifa ni asilimia 13). Kati ya wagonjwa 225
waliofanyiwa upasuaji wa kufungua kifua wagonjwa 105 walifanyiwa
upasuaji na madaktari wetu bingwa wa magonjwa ya moyo watoto wakiwa ni
60 na watu wazima 45.
Upasuaji
wa moyo wa bila kufungua kifua (Catheterization) kwa kutumia mtambo wa
Cathlab ulifanyika kwa wagonjwa 800 kati ya hao 798 wanaendelea vizuri
na wagonjwa wawili (2)walifariki hii ikiwa ni chini ya asilimia 1.6.
Kati ya wagonjwa 800 waliotibiwa wagonjwa watu wazima 631 walifanyiwa
upasuaji na madaktari wetu wa ndani.
Tulikuwa
na jumla ya kambi za matibabu 15. Tumefanya matibabu ya pamoja na
washirika wetu kutoka mabara ya Asia, Australia, Ulaya na Amerika.
Katika kambi zote hizo kambi za watoto ni tano na kambi za watu wazima
10. Jumla ya wagonjwa 120 walifanyiwa upasuaji wa kufungua kifua kati ya
hao watoto 80 na watu wazima ni 40. Wagonjwa 169 walifanyiwa upasuaji
wa bila kufungua kifua kati ya hao watoto 92 na watu wazima 77.
Kwa
wagonjwa wote hao 1025 kufanyiwa upasuaji wa kufungua kifua na bila
kufungua kifua hapa nchini Taasisi imeweza kuokoa zaidi ya bilioni 29
(Tshs. 29,725,000,000/=) ambazo Serikali ingezilipa kama wagonjwa hawa
wangefanyiwa upasuaji wa moyo nje ya nchi. Gharama za mgonjwa mmoja
anayetibiwa nje ya nchi ugonjwa wa moyo ni zaidi ya milioni 29.
Tulifanya
upasuaji wa kuunganisha mishipa ya damu (AVF- Arterio Venous Fistula)
kwa ajili ya kusafishia damu kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo
(Hemodialysis) 52.
Wakati
huo huo Taasisi ilishiriki katika utoaji wa huduma ya upimaji afya bila
malipo na kutoa elimu ya afya bora ya moyo kwa wananchi katika mikoa ya
Dar es Salaam, Dodoma, Lindi na Katavi. Katika mikoa hiyo tuliweza
kuwaona na kuwapatia huduma wananchi 8000.
Malengo
tuliyokuwa nayo kwa mwaka huu wa 2018 ni kuona wagonjwa wengi zaidi ya
hawa tuliowaona mwaka 2017 katika kliniki zetu za kila siku na kufanya
upasuaji. Taasisi imejipanga kufanya upasuaji wa kufungua kifua kwa
wagonjwa 400 na bila kufungua kifua kwa wagonjwa 1000.Tunatarajia kuwa
na kambi maalum za upasuaji wa moyo zisizozidi 15.
Aidha
tunawaahidi wananchi kwa mwaka 2018 tutaendelea kutoa huduma katika
kiwango cha kimataifa, kuendelea kupunguza kupeleka wagonjwa nje ya
nchi, kupunguza gharama za tiba katika Taasisi yetu, kuongeza idadi ya
huduma, kuboresha usafi zaidi katika Hospitali yetu na kuzidi
kushirikiana na Serikali na wananchi.
Changamoto
kubwa tunayokabiliana nayo katika kazi zetu za kila siku ni ufinyu wa
chumba cha uangalizi maalum (ICU) kwa wagonjwa wanaotoka katika chumba
cha upasuaji. Hii inatokea wakati ambao tunafanya upasuaji kwa wagonjwa
wengi kwa wakati mmoja hasa kipindi cha kambi za matibabu. Pamoja na
ufinyu wa wodi ya watoto. Asilimia 70 ya wagonjwa tunaowafanyia upasuaji
wa kufungua kifua ni watoto, tunajumla ya vitanda 123 kati ya hivi
vitanda vya watoto ni 24 tu.
Wagonjwa
wengi tunaowapokea mioyo yao kutokuwa katika hali nzuri hii ni
changamoto nyingine tunayokabiliana nayo katika matibabu ya wagonjwa
wetu.
Kwa
upande wa wazazi na walezi tunawaomba wasisahau kupima afya za watoto
wao pale watakapoona kuna hali ya tofauti katika ukuaji wa mtoto kwani
magonjwa mengi ya moyo yanaanzia utotoni. Mtoto akianza kuuguwa magonjwa
ya moyo wazazi wengi wanadhani ni matatizo ya kifua baada ya kumfikisha
Hospitali na kufanyiwa vipimo ndipo inagundulika mtoto anasumbuliwa na
magonjwa ya moyo. Kwa wamama wajawazito wafanye uchunguzi (Fetal
Echocardiography) wa kuangalia kama mtoto aliyeko tumboni anamatatizo ya
moyo.
Tunawashauri
watu wazima kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara hii
itawasaidia kujuwa kama wana matatizo ya moyo au la na hivyo kupata tiba
kwa wakati.
Katika
Bara la Afrika Taasisi yetu iko katika nafasi ya tatu katika utoaji wa
huduma bora za magonjwa ya moyo hasa katika upasuaji wa moyo kwa watoto.
Imetolewa na:
Kitengo cha Uhusiano
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
15/01/2018
No comments:
Post a Comment