Na Said Mwishehe, Globu ya jamii.
KAMPUNI ya Reli Tanzania (TRL) imesema imeamua kuhamishia huduma ya usafiri wa treni kutokea Dodoma kuanzia kesho.Uamuzi huo unakuja kipindi ambacho TRL imesitisha huduma za usafiri huo kutokea Dar es Salaam baada ya miundombinu ya reli kuharibika kati ya stesheni za Kilosa na Gulwe kutokana na mafuriko ya mvua zinazonyesha maeneo hayo kuharibu miundombinu.
Akizungunza Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mkuu Msaidizi (uendeshaji) kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuuu wa kampuni hiyo, Focus Sahani amesema wakati wanaendelea na matengenezo ya miundombinu iliyohariviwa na mafuriko eneo hilo wameona ni vema usafiri huo ukaendelea kwa kuanzia Mkoa wa Dodoma.
Amesema uongozi baada ya kutathimini hali ya miundombinu ya maeneo mengine yaliyo salama imeamua kuhamishia huduma ya usafiri huo wa treni kutokea Dodoma. Sahani amesema ratiba ya huduma ya muda wa kuanzia Dodoma ni kwamba treni ya abiria itaondoka saa moja usiku kesho Jumanne na Ijumaa kwenda Kigoma, Mwanza Name Mpanda ambako inatarajiwa kuwasili Mwanza saa 12 jioni siku ya Jumatano na Mpanda saa 12 jioni na Kigoma saa 12 jioni.
"Treni kutoka Mpanda, Mwanza na Kigoma zitatoka huko siku za Jumapili na Alhamis tu. Mpanda inatoka saa moja asubuhi, Mwanza inatoka saa mbili asubuhi na Kigoma inatoka saa1:30 asubuhi.Treni hizo zinafika Dodoma siku ya Jumatatu na Ijumaa saa 1:00 asubuhi, "amesema.
Wakati huohuo Sahani amesema treni pekee ya kutoka Tabora kwenda Mpanda itafanya safari zake siku za Jumanne, Alhamisi na Jumapili na itatoka Mpanda kurejea Tabora katika siku za Jumatatu, Jumatano na Jumamosi.
"Itakuwa inaondoka Tabora saa 12 asubuhi na kuwasili Mpanda saa 12:32 na itaondoka Mpanda kurejea Tabora saa 1:00 asubuhi na kuwasili saa 12:32 jioni. Uongozi WA TRL bado unaendelea kusimamia kazi ya ukarabati wa eneo lililoharibika Kati ya Kilosa na Gulwe, "amesema Sahani.
Alipoulizwa itachukua muda gani kurekebisha eneo lililoharibika, Sahani amejibu ni mapema mno kwani jitihada zinaendelea na kazi inafanyika usiku na mchana, na kwa kuwa bad maji yameja ni ngumu kufanya matengenezo zaidi ya maeneo ambayo yameanza kukauka maji.
Kuhusu abiria ambao waliokuwa wamekata tiketi kwa ajili ya kusafiri na treni na sasa wamesitisha huduma kwa treni ya kuanzia Dar es Salaam, amejibu tayari wamerudisha nauli za abiria waliokuwa na tiketi.
Pia uongozi wa TRL umesema moja ya sababu inayochangia reli kuharibika kwa maji ya mvua inatokana baadhi ya wakulima kulima katika maeneo ya reli,hivyo wamehimiza walnaolima pembezoni kwa reli kuacha kwani madhara yake ni pamoja na kuharibu miundombinu ya reli.
"Wakulima wamelima sana kiasi cha kusababisha maji kwenda kwenye reli na matokeo yake ni kuharibika kwa miundombinu, "umesema uongozi wa TRL.
Kaimu
Mkurugenzi Mkuu ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu Msaidizi (Uendeshaji) wa
Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) Focus Sahani akizungumza leo jijini Dar
es Salaam kuhusu uamuzi wa kampuni hiyo kutangaza ratiba ya usafiri wa
treni kuanzia Mkoa wa Dodoma kwenda mikoa mingine baada ya huduma ya
usafiri huo kusitishwa kwa stesheni ya Dar es Salaam.Pichani kushoto ni
wengine ni maofisa wa kampuni hiyo
No comments:
Post a Comment