Monday, January 29, 2018

SERIKALI YAUZA MENO YA VIBOKO KWA SH.30,900,000/= KATIKA MNADA WA HADHARA LEO JIJINI DAR ES SALAAM.

Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imefanya mnada wa hadhara wa kuuza meno ya viboko vipande 12,467 yenye uzito wa kilo 3,580.29 katika ofisi zake ndogo katika Jengo la Mpingo, jijini Dar es Salaam ambapo jumla ya makampuni 19 yenye leseni daraja la kwanza yameshiriki katika mnada huo.

Mnada huo umefanyika chini ya usimamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango ambapo kampuni ya On Tours Tanzania Limited imeibuka mshindi kwa kwa kununua meno hayo kwa jumla ya shilingi 30,900,000/= 

Awali akizungumza katika mnada huo, Mwenyekiti kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Karerema Kwaleh aliwataka wafanyabiashara kuzingatia masharti mnada huo.

Ambapo Karerema alimtaka mfanyabiashara yeyote atakeibuka mshindi kulipia asilimia ishirini na tano (25%) ya bei papo hapo na asilimia sabini na tano (75%) italipwa yote katika muda wa siku kumi na nne (14) baada ya mnada.

Kufuatia sharti hilo baada ya kutangazwa kwa mshindi, Mwakilishi kutoka Kampuni hiyo, Grey Kilas aliweza kulipia asilimia kiasi hicho cha asilimia ishirini na tano (25%) papo hapo na asilimia sabini na tano (75%) atailipia ifikapo Februari 11, 2018.

Wakati huohuo, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu TAWA, Mabula Misungwi amewatoa wasiwasi wananchi kuwa biashara hiyo haiwezi kuchochea ujangili kwa vile meno hayo yanauzwa kwa wafanyabiashara wale tu wenye leseni za nyara daraja la kwanza 

Mabula amesema meno hayo yalianza kukusanywa tangu mwaka 2004 na huko nyuma serikali ilikuwa ikiyauzia makampuni yenye leseni lakini kwa mwaka huo wameanza utaratibu mpya wa kuuza meno hayo kwa njia ya mnada.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Kampuni hiyo, Grey Kilas ameishukuru wasimamizi wa mnada huo kuwa umeendeshwa kwa uwazi wa hali ya juu na umetoa fursa kwa kila mmoja wao.

Akizungumzia kuhusu soko, Kilasi amesema meno hayo huuzwa nchini Japan, Marekani na Hongkong ambapo hutumika katika kutengenezea mapambo kama vile stempu pamoja na vishikizo vya nguo.Itakumbukwa kuwa kwa mara mwisho biashara hiyo ya kuuza meno ya viboko ilifanyika mwaka 2004. 
 Baadhi ya  meno ya viboko vipande  12,467 yenye uzito wa kilo 3,580.29 ambayo yameuzwa kwa njia ya mnada wa hadhara  leo   jijini Dar es Salaam kwa Kampuni ya On Tours Tanzania Limited kwa kiasi cha shilingi 30,900,000/= (Picha na Lusungu Helela-MNRT).

No comments: