Wednesday, January 17, 2018

SERIKALI YATOA SHILINGI BILIONI 24.4 KUJENGA NA KUKARABATI MELI

 Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye akipata maelezo kutoka kwa Kapteni Desiderius Chuwa wa Meli ya MV. Clarias kuhusu usalama wa chombo hicho na abiria wake kabla ya kuanza safari ya kutoka Mwanza kwenda Kisiwa cha Ukerewe wakati wa ziara yake mkoani Mwanza.
 Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye akitoa maelekezo kuhusu usalama wa abiria na matumizi ya vifaa vya uokoaji majini kwa watendaji na abiria wa meli ya MV. Clarias kabla ya kuanza safari ya kutoka Mwanza kwenda Kisiwa cha Ukerewe wakati wa ziara yake mkoani humo.
 Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye (wa pili kushoto) akipatiwa maelezo kuhusu matengenezo ya yaliyofanyika ya mfumo wa mafuta wa meli ya MV. Clarias inayosafirisha abiria kutoka Mwanza kwenda Kisiwa cha Ukerewe wakati wa ziara yake mkoani humo. Wa kwanza kulia ni Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSL) Bwana Eric Hamissi.
 Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye (kulia) akikagua meli ya MV. Clarias inayosafirisha abiria kutoka Mwanza kwenda kisiwa cha Ukerewe wakati wa ziara yake mkoani humo. Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSL) Bwana Eric Hamissi (kushoto) akitoa maelezo kuhusu meli hiyo.
 Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye (hayupo pichani) alipokagua meli ya MV. Clarias inayomilikiwa na Kampuni ya Huduma za Meli (MSL) ikiwa tayari kusafirisha abiria kutoka Mwanza kwenda kisiwa cha Ukerewe wakati wa ziara yake mkoani humo.
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye (aliyesimama) akiwasilisha taarifa ya Kampuni ya Huduma za Meli kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu (hawapo pichani) kuhusu ujenzi na ukarabati wa meli katika maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa wakati wa kikao na Kamati hiyo kilichofanyika bungeni mjini Dodoma. Wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa wa Bodi wa Kampuni hiyo Bi. Rose Lugembe.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa shilingi bilioni 24.496 kwa ajili ya kujenga meli mpya mbili na kukarabati meli tano ili ziweze kutoa huduma ya uchukuzi wa kusafirisha abiria na mizigo katika maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu ujenzi wa meli katika maziwa makuu kwenye kikao kilichofanyika bungeni mjini Dodoma. Mhe. Nditiye aliongeza kuwa fedha hizo tayari zimeshatolewa na Serikali na kupatiwa Kampuni ya MSCL kwa ajili ya kuanza ujenzi wa meli 2 mpya za kubeba abiria na mizigo katika ziwa Tanganyika na Victoria na kukarabati meli 5 ambazo ni MV. Victoria, MV. Butiama, MV. Liemba, MV. Umoja na MV. Serengeti.  
Mhandisi Nditiye aliongeza kuwa lengo la Serikali la kutoa fedha hizo ni kuboresha huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo katika maziwa makuu ili wananchi waweze kupata huduma za usafiri wa uhakika; kwa wakati na zinazozingatia usalama wa abiria na mizigo yao; kuiwezesha Serikali kupata mapato na kukuza uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla; na kwa kutambua fursa ya biashara iliyopo kwenye maziwa hayo kwa kuzingatia kuwa meli hizo ni kiungo kikubwa baina ya nchi yetu na nchi za jirani za Uganda, Kenya, Zambia, Malawi na DRC Congo kwa kuwa zinatumia meli zetu kusafirisha abiria na mizigo yao kupitia maziwa hayo.
Aidha, Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya MSCL Bwana Eric Hamissi alifafanua kuwa tayari Kampuni yake kwa kushirikiana na wataalamu wa Kampuni hiyo na wengine kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) na Jeshi la Wananchi Kitengo cha Wanamaji (TPDF Navy Command) wamekamilisha taratibu za kumpata mkandarasi wa kujenga meli mpya ya Ziwa Victoria ambaye ni mkandarasi wa Kampuni ya STX Engine Co. Ltd na STX Offshore & Shipbuilding Co. Ltd Joint Venture; na mkandarasi wa Kampuni ya KTMI kwa kushirikiana na Kampuni ya Yuko’s Enterprises Co. Ltd  kwa ajili ya kukabarati meli za MV. Victoria na Butiama ambapo kampuni zote ni za kutoka nchi ya Korea ya Kusini. Bwana Eric alisema kuwa Kampuni hizo zimekidhi vigezo vya mahitaji ya meli ya kubeba abiria na mizigo na zina teknolojia ya kisasa ya ujenzi na ukarabati wa meli ili kufikia azma ya Serikali ya kutoa huduma nzuri kwa abiria na wananchi wake. Mkataba wa ujenzi wa meli mpya unatarajiwa kusainiwa mwezi Februari, 2018 na wa ukarabati utasainiwa mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Prof. Norman Sigalla King ameiipongeza Serikali kwa kutoa fedha za kujenga na kukarabati meli za maziwa makuu ya Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa. Aidha, Prof. Norman Sigalla King ameishauri Serikali iajiri wafanyakazi wa meli wenye vigezo vya kimataifa kwa kuwa wengi waliopo wanakaribia kustaafu na ameitaka MSCL kutumia fedha hizo kama zilivyopangwa na kwa wakati ili wananchi wapate huduma za usafiri bora zaidi kwenye maziwa makuu.
Mhandisi Nditiye alifafanua kuwa Serikali inakabiliana na changamoto ya upungufu wa manahodha wa meli kwa kuzalisha wataalamu hao wenye weledi wa kisasa kutoka kwenye Chuo cha Bahari cha Dar es Salaam (DMI na Jeshi la Wananchi Kitengo cha Wanamaji (TPDF Navy Command). Katika hatua nyingine, Mhandisi Nditiye aliwataarifu wajumbe wa Kamati hiyo kuwa Mwezi Januari mwaka huu alifanya ziara ya kikazi mkoani Mwanza ambapo alitembelea na kukagua utendaji kazi wa Kampuni ya MSCL ikiwa ni pamoja na kukagua meli ya MV. Clarias ambayo imeanza kazi ya kusafirisha abiria na mizigo kutoka Mwanza kwenda kisiwa cha Nansio-Ukerewe baada ya kufanyiwa ukarabati wa mfumo wa mafuta, injini na sehemu za kukaa abiria ikiwa ni pamoja na kuwataka watendaji wa meli hiyo wazingatie usalama wa abiria na mizigo na kuwapatia elimu ya vifaa vya uokoaji majini wanapokuwa safarini ili waweze kujiokoa na kujinga na ajali wakiwa safarini pindi itakapotokea.
Bwana Eric Hamissi alifafanua kuwa Mamlaka ya Bandari Tanzania imetoa shilingi milioni 300 ambazo zimetumika kukarabati meli nne za Kampuni ya MSCL za kubeba mizigo na abiria ambazo ni MT. Sangara, MV. Clarias, ML. Wimbi na MV. Umoja ambazo zimeanza kazi na zitaiwezesha Kampuni ya MSCL kujiendesha, kufanya kibiashara na kuongeza mapato ya Serikali kwa kutoa huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo kwenye mwambao wa maziwa makuu na nchi za jirani.
Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) ina jukumu la kutoa huduma za usafiri wa majini kwa kutumia meli zake katika Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa na kujiendesha kibiashara kupitia huduma zake. Kampuni hii inasafirisha abiria na mizigo kwa safari za ndani na nje ya nchi zilizoko katika mwambao wa maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.

No comments: