Wednesday, January 24, 2018

MRADI WA MAJI NA JENGO LA UZAZI ZAHANATI YA YOMBO/BAGAMOYO YAKWAMA

Na Mwamvua Mwinyi,Bagamoyo.

Wakazi wa kijiji cha Yombo kata ya Yombo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wamelalamikia mradi wa maji uliofadhiliwa na Bank ya Dunia na kugharimu milioni 297, ambao haufanyikazi huku wakiwa hawanufaiki nao tangu ukamilike.

Aidha wamelalamikia kukwama kwa mradi wa jengo la uzazi, katika zahanati ya Yombo,ambalo limetumia kiasi cha sh.mil.55 na kuwekwa jiwe la  msingi na katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Taifa,Abdulrahman Kinana tangu mwaka 2014.

Kilio hicho kimetolewa na baadhi ya wakazi wa kijiji hicho ,wakati wa mkutano wa wananchi uliomwita diwani wa kata ya Yombo ,Mohammed Usinga kwenda kuwaeleza hatua zinazochukuliwa ili kukamilisha miradi hiyo .

Mkazi wa Yombo,Jabir Omary ,alisema inasikitisha kuona serikali na wafadhili wanatumia mamilioni ya fedha kwenye miradi ya maendeleo lakini haiendelezwi na haifanyikazi.

Alieleza mradi huo wa maji umetumia fedha nyingi ,hivyo ni jukumu la serikali kuisimamia ili ilete tija ndani ya jamii.Mkazi mwingine ,Abubakar Harubu alimtaka diwani wa kata hiyo pamoja na bodi ya maji ya kata kufuatilia na kusimamia kero hizo kwa maslahi ya wakazi hao.

"Mradi huu ni donda ,hauna manufaa ,;"Sisi hatutaki kusikia sijui mradi umerithishwa kutoka kwa diwani aliyepita ,tunachotaka kuona ni muendelezo wa miradi iliyoanzishwa kipindi cha nyuma iendelezwe na sio vinginevyo"

"Mradi huu umetumia mamilioni ya fedha ,jamani hata hamsikii uchungu wa fedha hizi ,yaani tanki la maji hadi linaweka uchafu ndani kutokana na kukosa maji,tunaomba viongozi wetu kutatua kero hizi za maji na afya" alisema Harubu.Kuhusu kukwama kwa jengo la uzazi kwenye zahanati ya Yombo,Jabir alisema akinamama wanadhalilika na kukosa huduma hiyo muhimu .

Alielezea kuwa ,zahanati hiyo pia ilikuwa kwenye mpango wa kupandishwa hadhi na kuwa kituo cha afya lakini wanashangaa ujenzi hauendelezwi na kuelezwa kuna muongozo uliotolewa kuwa kunatakiwa hekari sita ndipo kujengwe kituo hicho.

Nae afisa tatibu wa zahanati ya Yombo,Donald Malamsha ,alisema makisio ya ujenzi ya jengo la uzazi ilikuwa ni sh.milioni 87 na hadi kufikia ujenzi ulipokomea imeshatumika milioni 55.

Malamsha alielezea fedha iliyokwisha tumika ni nyingi hivyo halmashauri na serikali iangalie changamoto zinazokwamisha mradi na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka.Akielezea juu ya kero hizo,diwani wa kata ya Yombo,Usinga aliitaka bodi ya maji kusimama kidete ili watu wapate huduma ya maji.

Alisema atasimamia tatizo la transformer liweze kufanya kazi na kuagiza vituo vichache vyenye tija vifunguliwe na visivyofaa viache kwa sasa.Usinga ,aliwaasa wananchi kuacha kuhujumu mradi huo kwa kukata mabomba ,kuiba baadhi ya vifaa na kuharibu miundombinu na badala yake walinde miundombinu ya mradi ili udumu kwa muda mrefu.

Akizungumzia kuhusu jengo la uzazi ,Usinga alisema halmashauri imeshatenga sh.milioni 20 ili kukamilisha ujenzi huo wakati ikisubiri kupatikane eneo lenye hekari 4-6 la kujengwa kituo cha afya cha Yombo kwani eneo la sasa halikidhi mahitaji.

Mwenyekiti wa bodi ya maji ,Yombo ,Yahaya Omary alisema mradi huo umetekelezwa kwa fedha kutoka bank ya dunia ,ulianza ujenzi July 2013 na kukamilishwa Octoba 2015 lakini haufanyi kazi iliyotarajiwa .

Alikiri mradi huo kukumbwa na changamoto nyingi ikiwemo transformer kutokuwa imara,pump kuwa na shoti za mara kwa mara ,mabomba kupasuka na kuibwa kwa baadhi ya vifaa.Yahaya aliongeza, bomba zilizotumika ni ndogo kulingana na mradi wenyewe na endapo mradi huo ungekamilika ungeweza kulisha watu zaidi ya 2,000.

Alifafanua kuwa ,mradi wa maji bado haujakabidhiwa rasmi kwa wananchi ila ulikabidhiwa kwa majaribio kwa miezi sita ambayo imepita huku kukiwa na changamoto lukuki ambazo zinapaswa kutatuliwa kabla ya kukabidhi .

Mwandishi wa habari hii,alimtafuta kwa mara kadhaa kwa njia ya simu mkurugenzi wa halmashauri ya Bagamoyo, Fatuma Latu,kutolea ufafanuzi zaidi juu ya miradi hiyo ,hakupokea wala kujibu sms.

Mkutano huo uliazimia kuunda timu ya watu kumi ,ambayo itakwenda kufuatilia suala hilo katika ngazi na idara husika ili kupata ufumbuzi.
 Diwani wa kata ya Yombo wilayani Bagamoyo, Mohammed Usinga akizungumza na wakazi wa kijiji cha Yombo kuhusiana na baadhi ya miradi ya maendeleo isiyofanyakazi na mengine kushindwa kuendelezwa.(picha na Mwamvua Mwinyi)
 Jengo la wodi ya uzazi katika zahanati ya Yombo, Bagamoyo likiwa limekwama kwenye ujenzi na kuwekwa jiwe la msingi na katibu mkuu wa CCM Taifa ,Abdurahman Kinana mwaka 2014 .

Mradi wa maji uliofadhiliwa na bank ya dunia na kugharimu mamilioni ya fedha huko kata ya Yombo Bagamoyo, ambao haufanyi kazi iliyotarajiwa na wananchi hawanufaiki nao tangu ukamilike 2015.

No comments: