Thursday, January 25, 2018

MHALIFU ATAINGIA DAR AKIWA SALAMA LAKINI HATATOKA SALAMA-MAMBOSASA

Mkurugenzi Mtendaji wa Radio Times FM, Rehule Nyaulawa(aliyesimama)akizungumza leo akiwa katika Ofisi za Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa kabla ya kukabidhi tuzo maalum ambayo inalenga kutambua mchango wa Polisi katika kulinda usalama wa raia na mali zao. 
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa akionesha tuzo maalum ambayo wamepewa na Radio Times FM.Tuzo hiyo ni kutambua mchango wa Polisi katika kulinda usalama wa wananchi wa Dar es Salaam kwa mwaka 2017
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa(aliyesimama) akizungumza leo kabla ya kupokea tuzo maalum ya kutambua mchango wao katika suala la ulinzi na usalama iliyotolewa na uongozi wa Radio Times FM wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Rehule Nyaula(aliyekaa kushoto) .




*Asema wamedhibiti uhalifu, azungumzia Panya road 

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

KAMANDA wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema iwapo kuna mhalifu yoyote na wa kutoka sehemu yoyote anaweza kuingia Dar es Salaam salama lakini ajue hatatoka salama.

Amefafanua kutoka na kujipanga vema kulinda usalama wa raia na mali zao kwa Jiji la Dar es Salaam wamefanikiwa kukomesha uhalifu na hata waliokuwa wanajiita Panya Road na makundi mengine ya kihalifu sasa imebaki historia huku akifafanua jeshi hilo halipo tayari kuchezewa.

Mambosasa amesema hayo leo jijini Dar es Salaam, baada ya kupokea tuzo maalumu iliyotolewa na uongozi wa Redio Times Fm na kukabidhiwa kwa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu kama sehemu ya kutambua mchango wanaoutoa katika kuhakikisha wananchi wanakuwa salama wakati wote.Tuzo hiyo ilitolewa na Mkurugenzi .

Mtendaji wa redio hiyo Rehule Nyaula.Amesema tuzo hiyo imewatia moyo polisi Kanda Maalumu kwani imekuwa ni kawaida kusikia tu wakilaumiwa lakini Redio Times wanatambua kazi ambayo wanafanya na kuomba wengine kuiga mfano huo wa kuthamini kazi zinazofanywa na taasisi mbalimbali nchini.

MHALIFU HATATOKA SALAMA DAR

Akizungumzia namna ambavyo Jeshi la Polisi Kanda Maalumu la Dar es Salaam limejipanga kukabiliana na uhalifu, Kamanda Mambosasa amesema wanao mfumo mzuri wa mawasiliano ambao unasaidia kukabiliana na wahalifu kwa haraka zaidi.

Amesema kuwa ofisi yake kwa kushirikiana na makanda wa polisi Wilaya ya Temeke, Kinondoni na Ilala, maofisa wengine wa jeshi hilo kwa ngazi mbalimbali wamekuwa wakihakikisha usalama unakuwepo kwenye kila eneo na kwa sehemu kubwa wamefanikiwa.

Ameongeza wamefanikiwa kudhibiti wahalifu na anatambua wapo ambao wanaweza kutaka kuendelea kuingia Dar es Salaam kutoka eneo lolote lile kwa lengo la kufanya uhalifu lakini watambue wahalifu wanaweza kuingia lakini hawatatoka salama kwani polisi wako imara.

"Tumejipanga vizuri, kupitia maelekezo na maagizo ambayo tunapokea kutoka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini,IGP Simon Sirro hakika yametuweza kuifanya kazi yetu katika mfumo ambao mhalifu hana nafasi ya kufanya chochote, anaweza kuingia Dar es Salaam akiwa salama lakini hana ujanja wa kutoka akiwa salama,"amesema Kamanda Mambosasa.

AWAZUNGUMZIA PANYA ROAD

Kuhusu makundi ya kihalifu ambayo siku za nyuma yalitikisa Jiji la Dar es Salaam likiwamo la Panya Road na lile la Kumi ndani Kumi nje ,Kamanda Mambosasa amesema wamedhibi makundi hayo na ndio manaa hivi sasa kumekuwa kimya na wananchi wako salama wao na mali zao."Dhima yetu ni kuhakikisha wananchi wa Dar es Salaam wanakuwa salama pamoja na mali zao.Tutaendelea kufuatilia hatua kwa hatua ili mhalifu wa aina yoyote ashughulikiwe mapema.

"Makanda wa polisi Mkoa wa Ilala, Temeke na Kinondoni wamejipanga vema na kila mmoja anahakikisha kipande cha ardhi anachokisimamia kinakuwa salama wakati wote na ikitokea kuna mhalifu amefanya tukio na kukimbilia mkoa mwingine wa kipolisi tunao mfumo mzuri wa kukabiliana na wahalifu,"amesema Mambosasa.

AOMBA USHIRIKIANO.

Wakati huohuo,amesema mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Polisi pamoja na wadau wengine wakiwamo wananchi wa Dar es Salaam."Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam tumekuwa tukipata ushirikiano mzuri kutoka kwa wananchi na wadau wengine.Ushirikiano huo ni msaada mkubwa kwetu,"amesema Kamanda Mambosasa.

AONESHA ULIKO UHALIFU

Kamanda Mambosasa pia ametoa mwito kwa Kampuni binafsi za ulinzi kabla ya kutoa ajira kwa hao ambao wanataka kuwa nao ni vema wakatoa taarifa Polisi ili waweze kuwasaidia katika kuwapa taarifa sahihi iwapo wamewahi kuhusika kwenye matukio ya uhalifu au la.Amefafanua wamebaini kuna baadhi ya walinzi waliko kwenye kampuni binafsi za ulinzi ambao wanashirikiana na wahalifu kufanya uhalifu kwenye maeneo ambayo wafanya ulinzi.

"Tumebaini kuna baadhi ya walinzi wa kampuni binafsi ambao wanatoa taarifa kwa wezi na kisha wanashirikiana kufanya uhalifu.Hivyo nitoe mwito kampuni za ulinzi wawe wanawasiliana na Polisi kwani tutabaini wanayetaka kumuajiri ni raia mwema au ni mhalifu.Tunaweza kuchukua alama za vidole na kubaini kama amewahi kuhusika na uhalifu au laa,"amesema Mambosasa.

MKURUGENZI NYAULAWA AZUNGUMZA

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Redio Times, Rehule Nyaulawa amesema kuwa wameamua kutoa tuzo hiyo kwa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kutokana na kutambua mchango wao katika suala la ulinzi na usalama.Amesema kuwa kwa mwaka 2017, jeshi hilo limefanya kazi nzuri ya kulinda usalama wa raia na mali zao na kwamba wananchi wa Dar es Salaam wamekuwa wakifurahia hali hiyo na kufanya wawe huru kufanya shughuli zao kwa usalama.

"Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam wanafanya kazi kubwa ya kutufanya tuwe salama.Hivyo tumeona ni vema tukatambua mchango wao na ndio maana tumeamua kutoa tuzo hii kwa Kamanda Mambosasa kwa niaba ya polisi wengine wa kanda maalumu,"amesema.

No comments: