*Wanafunzi wa kike kuanzia darasa la nne kupewa chanjo
Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
TAASISI ya Saratani ya Ocean Road imesema imekuwa ikipokea wagonjwa wapya wa saratani 50,000 kila mwaka huku ikielezwa saratani ya shingo ya kizazi ndio inayoonekana kuongeza.
Pamoja na hali hiyo, imeelezwa jitihada mbalimbali zinafanywa na Serikali kwa kushirikiana na taasisi hiyo ambapo wameweka mkakati wa kuhakikisha wanafunzi wa kike waliopo kuanzia dasara la nne nchi kote watapatiwa chanjo itayakayosaidia kuwakinga na aina hiyo ya saratani.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Kinga katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dk.Chrispin Kahesa wakati wa semina iliyoandaliwa na taasisi hiyo kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini.
Lengo la semina hiyo ilikuwa ni kutoa elimu kuhusu ugonjwa wa satarani, hali ilivyo kwa sasa nchini, sababu zinazosababisha ugonjwa huo na pamoja na jitihada zinazochukuliwa kupunguza kasi ya saratani nchini.
WATANZANIA 50,000 KILA MWAKA HUPATA SARATANI
Akizungumzia ugonjwa huo ,Dk.Kahesa amesema kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani(HWO), Tanzania kila mwaka kunakuwa na wagonjwa wapya 50,000 wa saratani na hivyo unaweza kuona ukubwa wa ugonjwa huo nchini kwetu.
"Kila mwaka Tanzani wagonjwa wapya wa saratani ni 50,000.Ni idadi kubwa ambayo lazima tuweke mikakati ya pamoja kuhakiksha tunapunguza idadi hiyo na ukweli tunaweza.
"Ni suala la kuamua tu kuanzia mtu mmoja mmoja, familia na Watanzania kwa ujumla kwani baadhi ya sababu zinazosababisha ugonjwa huu tunaweza kuzikwepa.
"Baadhi ya sababu zinazosababisha saratani ni uvutaji sigara, pombe, vyakula vyenye mafuta mengi, kutofanya mazoezi ya mwili,unene na taka sumu.Hivyo ukiangalia hizo sababu unaweza kuziepuka na ukishindwa zote basi chagua hata sababu mbili zieupuke,"amesema.
Amefafanua zipo saratani ambayo hutokana na kirusi ambacho hubebwa na mwanaume na kisha kukiacha kwa mwanamke kupita tendo la ndoa na aina hiyo ya kirusi ndicho kinachosababisha saratani ya shingo ya kizazi.
WANAFUNZI WA KIKE KUPEWA CHANJO
Wakati huohuo Dk.Kahesa amesema ili kukabiliana na saratani hiyo, Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto kwa kushirikiana na taasisi hiyo wameandaa mkakati utakawezesha wanafunzi wa kike kuanzia dasara la nne wote nchini wapate chanjo ya saratani ili kuwakinga.
"Watoto wa kike ambao wapo dasara la nne tunaamini hawajaanza kujihusisha na tendo la ndoa kwani kirusi ambacho kinasababisha saratani ya shingo ya kizazi inatokana na tendo hilo,"amesema.
WATU WAPIME SARATANI MAPEMA
Dk. Kahesa ameeleza umuhimu wa watanzania kuwa na uratatibu wa kuangalia mapema kama wana dalili za saratani kwani hiyo itasaidia kujitambua mapema na hivyo kupata ushauri wa kitaalamu pamoja na tiba.
Amesema changamoto kubwa wagonjwa wengi wa saratani ambao wanafika kwenye taasisi hiyo na Hospitali za Rufaa ambazo zinatoa huduma za ugonjwa wanafika wakiwa wako katika hatua za mwisho.
"Ni muhimu kuangalia afya yako mara kwa mara kwani hii itasaidia kubaini ugonjwa mapema.Ukiwahi kupima na ukabainika kuwa na saratani upo uwezekano wa kuishi muda mrefu tu.
"Wapo wanaoamini saratani ni ugonjwa wa ajabu, hapana bali ni ugonjwa kama magonjwa mengine na ndio maana tupo kwa ajili ya kuwahudumia,"amesema Dk.Kahesa.
SARATANI NI UGONJWA WA PILI KWA KUUA
Akizungumza kwenye semina hiyo Mwakilishi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto Dk.Mariam Kalola pamoja na kueleza mambo mbalimbali amesema pia magonjwa yasiyoambukiza ambayo yamekuwa yakiwasumbua watanzania walio wengi ni saratani, kisukari ,shinikizo la damu na moyo.
Pia kwa sasa kuna tatizo la ugonjwa wa figo ambalo nalo limekuwa liigharimu Serikali fedha nyingi kwa ajili ya matibabu kwa wagonjwa wa figo.
"Magonjwa ambayo si ya kuambukiza yamekuwa yakichangia vifo vya Watanzania kwa asilimia 31 na huo ni kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2015.Saratani inashika nafasi ya pili ukiondoa ya magonjwa ya moyo na ajali za barabarani kwa kusababisha vifo,"amesema.
Ameeleza Februari 4 mwaka huu itakuwa siku ya magonjwa ambayo si ya kuambukiza ukiwamo ugonjwa wa saratani, hivyo akashauri vyombo vya habari vikaendelea kutoa elimu kuhusu magonjwa hayo ili kuisaidia jamii kuwa na uelewa mpana.
Pia amesema Serikal inajitahidi kuhakikisha wagonjwa wanaostahili kupata huduma ya tiba na dawa wanaipata kwa wakati na ndio maana bajeti ya Wizara ya Afya mwaka jana imeongezeka.
No comments:
Post a Comment