Monday, January 29, 2018

Jafo Apiga Marufuku Madarasa ya Udongo na Tembe

Na: Lilian Lundo - MAELEZO, Dodoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo amewaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halamshauri zote nchini kuhakikisha wanajenga madarasa yenye ubora na Viwango kuondokana na tatizo la baadhi ya Wilaya kuwa na majengo ya udongo na tembe.

Jafo ametoa agizo hilo leo Mjini Dodoma alipokuwa akifungua mafunzo ya uongozi ya siku tano kwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi toka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara yanayondelea katika ukumbi wa Hazina mkoani humo.

"Sitaki kuona madarasa ya udongo, tembe na watoto kusomea nje, hakikisheni matumizi ya mapato ya ndani yanagusa na kujibu matatizo ya wananchi," alisisitiza Jafo.Jafo amewataka Wakuu wa Wilaya kuhakikisha matumizi ya mapato ya ndani katika Halmashauri zao yanatumika katika miradi mbalimbali ya wananchi ikiwemo ujenzi wa madarasa ili kuondokana na uwepo wa madara ya udongo na tembe katika halmashauri zote hapa nchi.

Aidha amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kufanya maamuzi ya haraka mara wanapopokea fedha za miradi ya maendeleo, kauli hii imetokana na baadhi ya wakurugenzi kuwa na uzembe katika kufanya maamuzi hivyo kuchelewesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika wilaya zao na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Naibu Waziri TAMISEMI Josephat Kandege amesema anaamini Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wataenda kutekeleza yale ambayo watajifunza katika mafunzo hayo."Naamini kwa fursa hii ya mafunzo mtakuwa vinara mara mbili au tatu ya mlivyokuwa katika kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM)," alisema Kandege.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa wa Taasisi ya Uongozi Prof. Joseph Semboja amesema lengo la mafunzo hayo ni kuimarisha uwezo wa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri katika kufanya maamuzi ya kimkakati, kuwapa uwezo wa kuongoza watu na rasilimali nyingine pamoja na kuimarisha uwezo wao katika sifa zao binafsi.

Prof. Semboja amesema awamu hii ya nne ya mafunzo ya Uongozi kwa viongozi hao inakamilisha idadi ya viongozi 324 wa Wilaya na Mamlaka ya Serikali za Mitaa waliotarajiwa kupata mafunzo hayo kwa nchi nzima.

Mafunzo ya uongozi kwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri yalizinduliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa tarehe 9/5/2017 ambapo yameendeshwa kwa awamu tatu tofauti na awamu hii ya nne ndio awamu ya mwisho inayofunga mafunzo hayo kwa viongozi hao wa Wilaya na Mamlaka ya Serikali za Mitaa.

No comments: