Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akizungumza Mtawala wa Ras-Al-Khaimah Mtukufu Sheikh Saud Bin Saqr Al Qasimi na kufanya nae mazungumzo yaliolenga kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya pande mbili hizo.
Mazungumzo hayo yaliofanyika katika makaazi ya Sheikh Saud Bin Saqr Al Qasimi mjini Ras-Al-Khaimah, ambapo viongozi hao kwa pamoja walieleza haja ya kuendeleza uhusiano na kuimarisha mashirikiano katika kuinua sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya mafuta na gesi asilia.
Aidha, viongozi hao walizungumza juu ya hatua zinazoendelea katika suala zima la utafiti wa mafuta na gesi asilia ambapo katika mazungumzo hayo walieleza haja ya kuimarisha zaidi ushirikiano wa pamoja ili kufikia lengo la kuipaisha Zanzibar kiuchumi na kimaendeleo.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alitoa shukrani kwa kiongozi huyo kutokana na juhudi zake za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na kumpongeza kiongozi huyo kwa mafanikio yaliopatikana nchini humo katika kipindi kifupi.
Rais Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo kuwa Zanzibar ina mengi ya kujifunza kutoka kwa ndugu zao wa Ras Al Khaimah na iko tayari kupanua wigo wa maendeleo kutoka nchini humo kwani inatambua mafanikio yaliopatikana kutokana na mikakati iliyowekwa.
Pamoja na hayo, viongozi hao kwa pamoja walizungumzia hatua zaidi zinazohitajika katika kuimarisha ushirikiano kati ya Zanzibar na Ras Al Khaimah katika sekta za maendeleo ikiwa ni pamoja na kupanga mipango madhubuti katika malengo yaliokusudiwa ya hapo baadae.
Nae Kiongozi huyo alieleza kuwa Ras Al Khaimah itaendeleza uhusiano na ushirikiano wake na Zanzibar hasa katika sekta hizo za maendeleo na kusisitiza kuwa uhusiano na ushirikiano huo utaletea maendeleo makubwa Zanzibar hasa kwa kutambua kuwa jambo hilo limo kwenye dhati ya moyo wake.
Alieleza kuwa uhusiano na ushirikiano huo wa kihistoria uliopo una malengo ya kuhakikisha wananchi wa Zanzibar wanapata maendeleo endelevu huku akizipongeza juhudi na kasi za Rais Dk. Shein za kuhakikisha Zanzibar inapiga hatua za kiuchumi.
Katika maelezo yake Mtawala wa Ras Al Khaimah alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa atandelea kumuunga mkono ili kuhakikisha malengo yaliokusudiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kupambana na umasikini na kukuza uchumi yanatekelezeka kwa vitendo kwani kuna kila dalili za kuyatekeleza kutokana na juhudi anazoziona ambazo zinafanywa na Dk. Shein pamoja na Serikali anayoiongoza.
Wakati huo huo, Dk. Shein alikutana na uongozi wa Kampuni ya Kimataifa ya Utafiti na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia ya Ras Al Khaimah “Rak Gas”, iliyopo mjini Ras Al Khaimah ambapo katika maelezo ya uongozi wa Kampuni hiyo walimueleza Dk. Shein hatua zilizofikiwa za utafiti wa mafuta na gesi asilia Zanzibar.
Nae Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Kimataifa ya Utafiti na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Kamal Ataya alimpongeza Dk. Shein kwa ziara yake hiyo na kuahidi kuendeleza ushirikiano uliopo huku akisisitiza kuwa Kampuni yake itahakikisha utafiti unaofanyika unakuja na majibu mazuri.
Dk. Shein kwa upande wake alitoa pongezi zake kwa Mtawala wa Ras Al Khaimah pamoja na kuipongeza Kampuni hiyo kwa jitihada zake inazochukua katika kuhakikisha malengo yaliokusudiwa yanafikiwa na hatimae kuleta tija.
Mapema, Rais Dk. Shein akiwa na ujumbe wake akiwemo Mama Mwanamwema Shein, walitembelea eneo la Kisiwa cha Al Marjan ambacho kimetengezwa baada ya kufukiwa kwa bahari na kuwa mji wa kisasa wa kitalii na uwekezaji.
Akiwa katika eneo hilo, Dk. Shein alipata maelezo juu ya hatua zilizochukuliwa katika kulitengeneza eneo hilo la bahari na sasa kuwa ardhi iliyojengwa hoteli za kisasa ambazo zimekuwa ni kivutio kikubwa cha watalii kutoka sehemu mbali mbali duniani.
Aidha, uongozi wa Kisiwa hicho ulimueleza Rais Dk. Shein hatua zilizochukuliwa katika kuhakikisha hata watalii wakiwemo wananchi wa Ras Al Khaimah wanapata fursa ya kutalii katika eneo hilo kwa kuweka viwango vya chini vya malipo ya hoteli hizo ili kuhakikisha wenye vipato vya chini nao wanafaidika.
Dk. Shein akiwa nchini Dubai pia, alipata fursa ya kukutana na ujumbe wa Utaratibu wa Mfuko unaojulikana kwa jina la “Khalifa Fund” ambapo uongozi wa Mfuko huo ulimueleza Rais Dk. Shein namna unavyotoa fursa zake na kuahidi kutoa ushirikiano kwa Zanzibar hasa katika mpango wa kuwawezesha vijana kujikomboa na ajira na kuahidi miongoni mwa nchi zitakazowapa kipaumbele Zanzibar itakuwa ni ya mwanzo.
Rais Dk. Shein amemaliza ziara yake ya wiki moja katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na anatarajiwa kurejea nchini kesho Jumamosi, tarehe 27 Januari, 2018.
Ziara hiyo ya Dk. Shein ilianza kwa kufanya mazungumzo na Mtukufu Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan, Mrithi wa Mtawala wa Abu Dhabi na Naibu Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya (UAE) nchini Abu Dhabi ambapo pia,alifanya mazungumzo na Mohamed Saif Suwaid, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Abudhabi “Abudhabi Fund for Development”, na kutembelea mji wa Nishati, Masdar, msikiti wa Shaikh Zayed pamoja na sehemu ya kihistoria ya Wahat Al Karama.
Aidha, Dk. Shein alifanya ziara nchini Dubai kufanya mazungumzo na Mtukufu Sheikh Mohammed bin Rashid Al Makhtoum, Makamo wa Rais na Waziri Mkuu wa (UAE) na Mtawala wa Dubai, alitembelea Bandari ya Jebel Ali, alikutana na Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wawekezaji na Wenyeviwanda wa Dubai na kutembelea Mji mpya wa kisasa wa Nakheel pamoja na Mradi wa Palm Jumeirah.
Dk. Shein alifanya ziara mjini Sharjah na kukutana pamoja na kufanya mazungumzo na Mtukufu Dk. Shaikh Sultan Mohammed Al Qasimi, Mtawala wa Sharjah,akiwa Sharjah, alitembelea eneo la shughuli za uvuvi la ‘East Fishing Processing LLC” pamoja na shamba la ngombe wa maziwa la Al Rawabi.
Pia, Dk. Shein alifanya ziara Ras Al Khaimah na kukutana pamoja na kufanya mazungumzo na Mtukufu Shaikh Saud Saqr Al Qasimi, Mtawala wa Ras Al Khaimah pamoja na kutembelea Makao Makuu ya Kampuni ya Kimataifa ya Utafiti na Uchimbaji wa Mafuta na gesi asilia ya Ras Al Khaimah “Rak Gas” pamoja na kutembelea kisiwa cha Al Marjan.
Katika ziara hiyo, Dk. Shein alifuatana na viongozi mbali mbali akiwemo Mkewe Mama Mwanamwema Shein, Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Salama Aboud Talib, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Khalid Salum Mohamed, Waziri Asiyekuwa na Wizara Maalum Juma Ali Khatib,pamoja na Mshauri wa Rais Masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa, Uchumi na Uwekezaji Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa.
Wengine ni Katibu Mkuu Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, Juma Ali Juma, Balozi Mohamed Haji Hamza Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa upande wa Zanzibar, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), Salum Khamis Nassor pamoja na watendaji wengine wa Serikali.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment