Sunday, January 7, 2018

CCM YAWAHAMASISHA NA KUWAUNGA MKONO WANAFUNZI WA UALIMU (DUCE) WANAOJITOLEA KUFUNDISHA KATIKA SHULE ZA SERIKALI

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeipongeza Kamati ya Wanafunzi wanaojitolea kufundisha katika shule za Serikali na wanaosomea Masomo ya Ualimu katika Chuo Kikuu kishiriki cha Elimu (DUCE) pamoja na Uongozi wa Tawi la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) chuoni hapo.

Kamati hiyo ya Wanafunzi wanaojitolea kufundisha katika shule za Serikali imekuwa na utaratibu wake mahususi ambapo wanafunzi wanaosomea ualimu Chuoni hapo hufundisha masomo mbali mbali ikiwamo yale ya Sayansi, Hisabati, na Uchumi katika shule za Serikali kuanzia shule za msingi na sekondari.

Awali akitoa neno la utambulisho na ufunguzi Mwenyekiti wa Kamati ya Wanafunzi wanaojitolea Ndg. Emijidius Cornel alieleza ushirikiano ambao wameupata kutoka kwa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke na kwamba walichukua hatua hiyo ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za ujenzi wa Taifa katika sekta ya elimu zinazofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya Uongozi wa Ndg. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Naye Mwenyekiti wa Tawi la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Ndg. Tweve Enock la Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE) alipongeza Kamati ya Vijana wanaojitolea na kufafanua programu hiyo ya kujitolea ni sehemu ya mipango ya Tawi la Chama chuoni hapo kuunga mkono uharakishaji wa utekelezaji wa Sera za CCM na Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015-2020.

Katika nasaha zake Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Mwenye dhamana ya Itikadi na Uenezi amesema kitendo cha kutoa elimu na kupeleka maarifa kwa kujitolea ni kitendo cha Kijamaa na kinakwenda sambamba na misingi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akiifafanua baadhi ya misingi hiyo amegusia Ahadi za mwanachama wa CCM zinazosema nitaitumikia nchi yangu na watu wake wote, nitajitolea nafsi yangu kuondosha umasikini, ujinga, magonjwa na dhuluma na nitajielimisha kwa kadiri ya uwezo wangu na kuitumia elimu yangu kwa faida ya wote.

Aidha ndugu Polepole amesisitiza Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitaendelea kuunga mkono jitihada na harakati za watu na makundi ambayo yanatumia muda wao kushughulika na shida za watu kwa sababu kufanya hivyo ni sehemu ya utume wa mageuzi makubwa yanayofanywa na CCM katika Uongozi wake wa awamu ya Tano.

Katika Mkutano huo, aliyekuwa Mshauri na Mlezi wa Taasisi ya CHASO-DUCE Ndg. Gracious Mwanguya ameomba kujiunga na Chama Cha Mapinduzi, na ameshauriwa kufuata utaratibu katika Tawi lililo karibu naye.

Wakati uo huo, Seneti ya Mkoa wa Dar es Salaam imekuwa na kikao chake cha kazi kwaajili ya kupanga mikakati ya ujenzi wa Chama mwaka 2018. Akizungumza na Seneti hiyo Ndg. Polepole amewakubusha umuhimu wa kuwa mabalozi wazuri wa CCM na kuyaishi masharti ya Uanachama

Mwanachama mwaminifu ni yule anayeyaishi masharti ya uanachama kama yalivyoainishwa katika Katiba ya CCM Ibara ya 8(2) Kuwa awe mtu anayefanya juhudi ya kuielewa, kuielezea, kuitetea na kutekeleza Itikadi na Siasa ya CCM na awe mtu 8(4)… anayependa kushirikiana na wenzake na 8(5) kuwa mtu ambaye siku zote yuko mstari wa mbele katika utekelezaji wa mambo yote ya umma kulingana na Miongozo ya CCM, alisema Ndg. Polepole akinukuu vifungu hivyo vya Katiba.

Shughuli hizi mbili ni mwendelezo wa vikao vya ndani na sehemu ya kazi ya Ujenzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambazo zimeshaanza kwa mwaka 2018 na zitaendelea katika Mikoa na Wilaya zote nchini huku msisitizo ukiwa ni kufanya kazi kwa bidii ikiwamo kwa kujitolea, kuendelea kushughulika na shida za watu na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM

Imeandaliwa na,

IDARA YA ITIKADI NA UENEZI
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)
OND LUMUMBA





No comments: