UCHAGUZI WA MARUDIO KATIKA KATA NNE ZA MANZASE (CHAMWINO), KIMAGAI (MPWAPWA), ISAMILO (MWANZA) NA MADANGA (PANGANI)
PAMOJA NA MAJIMBO YA SIHA (KILIMANJARO) NA KINONDONI (DAR ES SALAAM)
PAMOJA NA MAJIMBO YA SIHA (KILIMANJARO) NA KINONDONI (DAR ES SALAAM)
____________________
Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kinapenda kuujulisha umma wa wanachama wa CCM kuwa
kimepokea taarifa kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwa kutakuwa
na uchaguzi wa marudio katika Kata na Majimbo yaliyotajwa hapo juu.
Wanachama
wote wenye sifa za msingi kwa mujibu wa Katiba ya Nchi na waliokidhi
vigezo vya uanachama kwa mujibu wa Katiba ya CCM na Kanuni zake
wanahamasishwa kujitokeza ili kuomba ridhaa ya Chama kupeperusha bendera
ya CCM katika Uchaguzi huu wa marudio isipokuwa na kama
inakavyoelekezwa na taarifa hii.
Aidha Chama kimejipanga kufanya
kampeni za kistaarabu na kisayansi, na zilizosheheni siasa za hoja na
zinazojikita katika kushughulika na shida za wananchi na hatimaye
kushinda kwa kishindo katika uchaguzi huu wa marudio. Kwa maana hii,
msisitizo unawekwa kwa wanao omba ridhaa ya kugombea, vikao vya uchujaji
na mapendekezo, na vikao vya uteuzi kuzingatia Misingi ya Maadili na
kuhakikisha waombaji wana akisi uaminifu, uadilifu, uchapakazi, heshima
kwa watu, ukubalifu wa imani, siasa na itikadi ya CCM, nidhamu kwa chama
na wawe watu ambao umma wa wananchi unawatambua kwa nafasi yao katika
jamii inapokuja katika kushughulika na shida zao.
KWA WAOMBA
DHAMANA YA UDIWANI
Wana CCM ambao wamejipima na kujitafakari na kuona wanatosha,
wanakumbushwa kwamba kuchukua fomu ya ugombea udiwani katika Ofisi za Kata
tajwa hapo juu ni tarehe 8-11 Januari 2018. Mwisho wa kurudisha fomu ni tarehe
11 Januari 2018 saa 10:00 jioni. Gharama ya fomu ni Shilingi 10,000/- tu za
Kitanzania.
Wajumbe wa Mikutano Mikuu ya Kata watapiga kura za maoni
tarehe 12 Januari 2018. Kamati za Siasa za Kata zitajadili na kutoa mapendekezo
kwa Kamati za Siasa za Wilaya tarehe 13 Januari 2018.
Kamati za Siasa za Wilaya zitajadili na kutoa mapendekezo
yake kwa Kamati za Siasa za Mkoa tarehe 14 Januari 2018. Kamati za Siasa za Mikoa
zitajadili na kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu za Mikoa tarehe 16
Januari 2018. Halmashauri Kuu za Mikoa zitajadili na kufanya uteuzi wa mwisho tarehe 17 Januari 2018
Wagombea walioteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushiriki
katika uchaguzi wa Udiwani katika Kata nne watachukua fomu kutoka kwa Msimamizi
wa Uchaguzi ngazi ya Kata katika kata husika tarehe 18-19 Januari 2018 na zoezi
hili litafanyika chini ya usimamizi wa Katibu wa CCM wa Wilaya.
UCHAGUZI WA
MARUDIO KWA MAJIMBO YA SIHA NA KINONDONI
Baada ya tafakuri na tathimini ya kina, Kamati Kuu ya
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kwa mamlaka
iliyokasimiwa kwake na Kikao cha Halmshauri Kuu ya Taifa (NEC) imemteua Ndg. Dkt. Godwin Mollel kusimama na
kugombea Jimbo la Siha, Mkoa wa
Kilimanjaro na Ndg. Maulid Mtulia
kusimama na kugombea Jimbo la Kinondoni,
Mkoa wa Dar es Salaam.
Aidha
wagombea wa Ubunge wanaelekezwa kufika katika Ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM)
katika Mikoa husika na kupokea maelekezo yahusuyo Uchaguzi kutoka kwa Makatibu
wa CCM wa Mikoa hiyo siku ya Jumanne, tarehe 9 Januari 2018 bila kukosa.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Imetolewa na,
HUMPHREY POLEPOLE
KATIBU WA NEC – ITIKADI NA UENEZI
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)
06 Januari 2018
No comments:
Post a Comment