Saturday, January 13, 2018

ASILIMIA 80 YA WANAOHITAJI DAMU NCHINI NI WANAWAKE.

Waziri wa afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu aliyesimama akiongea na wananchi hawapo pichani wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuchangia damu iliyoandaliwa na Chama cha wanawake cha Tasania ya Filamu nchini leo jijini Dar es salaam.


NA WAMJW-DAR ES SALAAM

ASILIMIA 80 ya wanaohitaji damu nchini ni wanawake kwa sababu mbalimbali ikiwemo uzazi salama wakati wa kujifungua kwa njia ya kawaida na njia ya upasuaji. 

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuchangia damu ambayo inafanywa na Chama cha wanawake wa Tasnia ya Filamu nchini leo jijini Dar es salaam. 

“Napenda kusisitiza Damu haiuzwi na kwa mgonjwa yeyote atakayeuziwa damu kwenye kituo chochote cha afya cha Serikali atoe taarifa kwenye idara husika na atachukuliwa hatua” alisisitiza Waziri Ummy Mwalimu. 

Aidha Waziri Ummy amesema kuwa Uongozi wa Hospitali au kituo cha Afya cha Serikali wahakikishe kuwa wanaweka matangazo yanayoelimisha wananchi kuwa damu haiuzwi bali inatolewa bila ya malipo na matangazo yaelekeze wananchi sehemu ya kutoa malalamiko. 

Mbali na hayo Waziri Ummy amesema kuwa wananchi hasa wanaume wanatakiwa kujenga utamaduni wa kuchangia damu kwa hiari mara kwa mara ili kuweka akiba ya kutosha katika benki ya damu hatimae kupunguza uhaba wa damu katika benki ya damu na kuokoa vifo vitokanavyo na ukosefu wa damu. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha wanawake wa Tasnia ya Filamu nchini Vanita Omary amesema lengo la kampeni hiyo ni kufikisha chupa 300 za damu katika uzinduzi hyo na tayari washapata chupa 288 mpaka sasa. 

“Tumeanza kampeni hii tangu jumatatu wiki hii na mpaka kufikia leo siku ya uzinduzi tumefanikiwa kupata chupa 288 tunatumaini tutavuka lengo mpaka mwisho wa kampeni hii, alisema Bi Vanita. 

Kampeni hiyo iliyozinduliwa leo na Waziri Ummy imeandaliwa na Chama Cha wanawake wa Tasnia ya Filamu nchini kwa kushikiana na Mpango wa damu salama nchini.
Waziri wa afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu aliyesimama kushoto akimsalimia mwananchi anayepata huduma katika moja ya banda lililokuwa likitoa huduma za afya katika viwanja vya Biafra wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuchangia damu iliyoandaliwa na Chama cha wanawake cha Tasania ya Filamu nchini leo jijini Dar es salaam.

Waziri wa afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu katikati akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wasanii wa kike wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuchangia damu iliyoandaliwa na Chama cha wanawake cha Tasania ya Filamu nchini leo jijini Dar es salaam.
Baadhi ya wasanii wakiwa wanasubiri huduma ya kuchangia damu wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuchangia damu iliyoandaliwa na Chama cha wanawake cha Tasania ya Filamu nchini leo jijini Dar es salaam.

No comments: